1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ulaya yagawanyika kuhusu mpango wa Marekani.

Sekione Kitojo28 Machi 2007

Mfumo wa ulinzi dhidi ya makombora ambazo zinatarajiwa kuwekwa katika maeneo ya Ulaya ya mashariki ni suala linaloleta wasi wasi mkubwa katika eneo lote la Ulaya. Mfumo huo wa ulinzi dhidi ya makombora, unaodaiwa kuwa una lengo la kuyalinda mataifa ya magharibi dhidi ya mashambulio ya makombora kutoka kwa mataifa yenye ushari, utakuwa na sehemu mbili ifikapo mwaka 2011; rada katika jamhuri ya Cheki na kituo dhidi ya makombora nchini Poland

https://p.dw.com/p/CHHG

.

Wajumbe wa baraza la mawaziri katika jamhuri ya Cheki na Poland wenye kufuata mrengo wa kulia wanakubaliana na wazo la kuwa na kituo hicho na hivi sasa wanaangalia ni masharti gain waiwekee Marekani, ambapo wanachama wa NATO wamegawanyika na bado wanafikiria mikakati yao pamoja na athari za kiuchumi.

Mataifa makubwa ya umoja wa Ulaya yanaweza kufikia hatua ya kuangalia upya majukumu yao ya kisiasa. Ufaransa na mataifa mengine makubwa ya umoja wa Ulaya , yalikuwa na matumaini hadi hivi karibuni kuwa kama wapatanishi kati ya Iran na jumuiya ya kimataifa , pamoja na kuendelea kuweka ushawishi wao katika mashariki ya kati , ameeleza Svetlozar Andreev , mtaalamu wa sayansi ya kisiasa katika kituo cha masomo ya siasa na katiba mjini Madrid ameliambia shirika la habari la IPS.

Tatizo kuu la msingi ni jinsi gain ya kulinganisha maslahi ya nchi kubwa kama Ufaransa, Ujerumani , Itali na Hispania pamoja na yale ya Marekani, Andreev amesema.

Rais wa Ufaransa Jacques Chirac ameonya kuwa kituo hicho kinaweza kuleta hali mpya wa mtengano katika Ulaya.

Wakati wa ziara yake nchini Poland , kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia alisisitiza kupatikana suluhisho ndani ya NATO na mjadala wa wazi na Russia kuhusu suala hilo, wakati waziri wake wa mambo ya kigeni Frank-Walter Steinmeier alionya juu ya hatari ya kuwa na mashindano mapya ya silaha.

Bunge la Ukraine pia limeshutumu mipango hiyo ya Marekani, lakini maafisa wa serikali wanaamini kuwa nchi hiyo inapaswa kushiriki kikamilifu katika mazungumzo kutokana na kuwapo kwake katika eneo ambalo ni kati ya mataifa ya magharibi na Russia.

Kwa mujibu wa wadadisi wa masuala ya kisiasa wa Russia na Ukraine, waziri mkuu Viktor Yanukovich anaweza kuwa mtu ambaye anaweza kuiingiza Russia katika hatua hizo za majadiliano hayo yenye utata.

Hata hivyo , rais wa Ukraine ambaye anaelemea zaidi upande wa mataifa ya magharibi Viktor Yushchenko amesema suala la kituo hicho linazihusu zaidi nchi ambazo zinahusika, na kumaanisha kuwa mradi huo unaweza kuzifaidia nchi za Ulaya kwa jumla katika ulinzi.

Russia inatoa hisia kali kutokana na taarifa hizo za kukisia, lakini Svetlozar anadhani kuwa Moscow huenda itakuwa tayari kwa ajili ya Ulaya tofauti kabisa.

Warusi watataka kutumia kujijenga huko kwa NATO pamoja na uwezo wa kijeshi wa Marekani karibu na mpaka wake wa magharibi kama nafasi ya kuboresha mfumo wake wa ulinzi na kuionyesha Marekani kama dola yenye madaraka makubwa kijeshi na pengine kupata maridhio katika medani ya kimataifa.

Kushindwa kwa serikali za Poland na jamhuri ya Cheki kutoa taarifa zaidi kuhusiana na mipango hiyo pia kumesababisha ukosoaji, hata miongoni mwa watu ambao wanaunga mkono uwekwaji wa vituo hivyo.