Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 10.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri

Wahariri wanaizungumzia ziara ya Barroso katika kisiwa cha Lampedusa, pia wanatoa maoni juu ya mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani na juu ya mwenyekiti mpya wa Benki kuu ya Marekani.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso(kushoto)na Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso(kushoto) na Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta

Gazeti la " Stuttgarter" linaanza kwa maoni juu ya ziara ya Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Manuel Barroso pamoja na Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta kwenye kisiwa cha Lampedusa kufuatia maafa yaliyowafika wakimbizi.

Mhariri wa gazeti hilo anasema ziara hiyo ni kitendo cha dhihaka.Mhariri huyo anaeeleza kuwa Bwana Barroso ametoa mwito wa kuhimiza moyo wa kibinadamu na kuwapa wakimbizi matumaini.Lakini mhariri wa gazeti la "Stuttgarter" anasema Barroso ndiye mwakilishi mkuu wa jumuiya ambayo kwa muda wa miaka mingi imekuwa inachukua kila hatua kuwanyima wakimbizi matumaini.

Hakuna hatua thabiti ya mawaziri wa Umoja wa Ulaya

Gazeti la"Osnabrücker" pia limeandika juu ya maafa yaliyowafika wakimbizi.Na pia limeitilia maanani ziara ya Barroso na Waziri Mkuu wa Italia Enrico Letta katika kisiwa cha Lampedusa ambako walizomewa na watu.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba ni vigumu kuamini, kwamba kwa mujibu wa Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International, katika karne hii ya 21 wapo wakimbizi karibu milioni 18 duniani. Kila mmoja wa watu hao anaweza kufikwa na maafa. Na kwa hivyo ni aibu kubwa kama alivyosema Papa Francis ,kwa watu mia tatu kuangamia baharini.Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya walikutana, lakini hakuna hatua thabiti walioamua.

Mhariri wa gazeti la "Osnabrücker"anasema kwamba licha ya nchi za Ulaya kukabiliwa na mgogoro wa madeni na ukosefu mkubwa wa ajira nchi hizo bado zina afadhali kubwa.

Mazungumzo juu ya serikali ya mseto

Gazeti la "Badische" linazungumzia juu ya mkutano wa kuangalia uwezekano wa kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani baina ya vyama vya kihafidhina na chama cha watetea mazingira cha kijani. Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anaziona dalili kwamba mseto umeshapikwa baina ya chama cha Kansela Merkel,CDU, chama ndugu cha CSU na chama kikuu cha upinzani SPD.

Mhariri huyo anaeleza.kuwa japo Kansela Merkel anajaribu kuwa kimya, dalili zinaonyesha kuwa moyoni vyama vya CDU na CSU vimeshaamua kuunda serikali ya mseto ya vyama vikuu,yaani na chama cha SPD. Mazungumzo ya leo baina ya vyama vya kihafidhina na chama cha kijani ni hatua ya kutimziza mradi tu.Baadhi ya wanachama wa CDU na wengi wengine wana mashaka juu ya chama cha kijani.

Mwenyekiti mpya wa Benki Kuu ya Marekani

Gazeti la "Süddeutsche" linatoaa maoni juu ya kuteuliwa kwa mwenyekiti mpya wa Benki kuu ya Marekani, Janet Yellen. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba mwenyekiti huyo mpya anatetea sera ya fedha ya wastani ,kwani anaamini kwamba kiwango cha riba kinachowekwa na Benki Kuu kinapaswa kuambatanishwa na kiwango cha ukosefu wa ajira. Sera hiyo inasaidia katika juhudi za kupunguza ukosefu wa ajira.

Mwandishi.Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Yusuf Saumu