Magazetini: Wahariri wameandika kuhusu Puigdemont, Israel na Saudia na Mkutano wa kilele kuhusu Syria | Magazetini | DW | 04.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Magazetini: Wahariri wameandika kuhusu Puigdemont, Israel na Saudia na Mkutano wa kilele kuhusu Syria

Magazeti ya Ujerumani yamezungumzia kuhusu Saudi Arabia kukaribiana na Israel, kurejeshwa Uhispania rais wa zamani wa  jimbo la Catalonia Puigdemont na mkutano wa kilele wa mataifa ya Urusi, Uturuki na Iran kuhusu Syria.

Bildkombo Mohammed bin Salman, Kronprinz Saudi-Arabien & Benjamin Netanjahu, Ministerpräsident Israel (Reuters/A. Levy & A. Cohen)

Mwanamfalme Mohammed bin Salman (kushoto) Benjamin Netanyahu (kulia)

Tukianza  na  mada  kuhusu  kukaribiana  kati  ya  Israel  na  Saudi Arabia  baada  ya  mwanamfalme Mohammed  bin Salman  kusema kwamba  Israel inahaki  ya  kuishi  kama  taifa , mhariri  wa  gazeti  la Reutlinger General-Anzeiger anaandika:

Kwa upande  wa  kijeshi  na  mashirika  ya  ujasusi  kumekuwa na ushirikiano  baina  ya Israel  na  Saudi  Arabia. Adui yao  wa  pamoja Iran  inaliunganisha  taifa  hilo  la kifalme la  Kiarabu  la  kisunni  na taifa  hilo la  Kiyahudi, licha  ya  kuwa  hadi  sasa  hakuna  uhusiano wa  kidiplomasia  kati  yao. Mwanamfalme Mohammed  bin Salman anaonekana  kuwa  ni  mtu  mwenye nguvu  katika  ufalme  huo  wa Saudia.  Ni mshangao  mkubwa , kwamba  ameweza  hadharani kusema  kwamba  Israel  inahaki  ya  kuishi  kama  taifa, ikiwa pia kwasababu Saudi Arabia  ndio nchi  takatifu  mlinzi wa  Uislamu. Hatua  hiyo  hata  hivyo  inapaswa  kuchukuliwa  kuwa  kama tahadhari  kwa  Wapalestina. Kuuchochea  tena  mzozo  wake  na Israel  hakutaleta  manufaa, kwa  kuwa  uhusiano  wa kimkakati kati ya  Tel Aviv  na  Riadh  una jukumu  kubwa  la maamuzi.

Mhariri  wa  gazeti  la Badisches Tagblatt  la  mjini  Baden-Baden akiandika  kuhusu  mada  hiyo  anasema:

Mwanamfalme Mohammed  amechagua  njia  ya  siasa  makini na kujitoa  kutoka  kupuuzia  kile  ambacho  hadi  sasa  kimekuwa  hali halisi  duniani. Anataka  mkataba  wa  amani  na  taifa  la  Israel, ambao  hadi  hivi  karibuni  haukuwapo  nchini  humo, na  Saudi Arabia  hivi  sasa  inaunga  mkono  mapambano  dhidi ya  Iran, lakini pia  kwa  matumaini  ya  kiuchumi. Saudi  Arabia  inabakia  hata hivyo mtetezi  wa  suluhisho  la  mataifa  mawili  katika  mzozo  kati ya  waisrael  na  Wapalestina. Juhudi  za  hivi  karibuni  za  kupata makubaliano  ya  amani  zina muelekeo  wa  uwezekano kwa  kiasi fulani. Mkaribio  huu  kati  ya  Israel  na  Saudi  Arabia  ni  fursa inayofaa  kuchukuliwa.

Mahakama  imeamua  rais  wa  zamani  wa  jimbo  la  Catalonia nchini  Uhispania  Carles Puigdemont  arejeshwe  nchini  mwake kwa  mashitaka  baada  ya  kukamatwa  nchini  Ujerumani. Mhariri wa  gazeti  la  Suedwest Presse  la  mjini  Ulm  anaandika:

Mahakama  imekwisha  tamka, lakini  mtazamo  wa  msingi  wa uamuzi  wa  mwendesha  mashitaka  ni  kwamba  kuna  mwelekeo wa  uhalifu  katika  uasi uliotokea  nchini  Uhispania na kufananishwa  na  uhaini.  Hali  inaonekana  kwamba Carles Puigdemont atarejeshwa  nchini  mwake  Uhispania  na  ambako anakabiliwa  na  kifungo  cha  hadi  miaka  30  jela. Inaonekana sheria  hii  kuwa  ni  kali  kwa wale wote  wanaounga  mkono  uasi huo. Mafanikio  ya  jimbo  hilo kujitenga  yangekuwa kioo  cha majimbo  mengine , ambayo  yangependa  leo  na  sio  kesho kusitishwa  hali  ya  kuutukuza  Umoja  wa  Ulaya.

Gazeti  la  Mannheimer Morgen   likizungumzia  kuhusu  mkutano  wa kilele  wa  viongozi  wa  Urusi, Uturuki na  Iran  kuhusu  Syria linaandika:

Si  Putin ama  Erdogan  wangependa  kuachia  misimamo  yao kuhusiana  na  udhibiti  wa  Syria  na  utawala  wake. Mkutano  mjini Ankara , kama  ilivyokuwa  katika  mkutano  uliopita  kati  ya  nchi hizo  mjini  Sochi  karibu  miezi mitano  iliyopita, ni  mfumo  mwingine , wa  kupata  suluhisho  la  amani  nchini  Syria.  Hakuna  zaidi.

Hayo  ni  baadhi  ya  maoni  ya  wahariri  wa  magazeti  ya Ujerumani , kama  yalivyokusanywa  na  Sekione  Kitojo.

Mwandishi:  Sekione  Kitojo  / Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com