Macron akutana na Merkel | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.06.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

MACRON NA MERKEL

Macron akutana na Merkel

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amemkaribisha Rais Emmanuel Macron kwenye mazungumzo yanayolenga kuimarisha mageuzi yanayoweza kuzuia kusambaratika kwa Umoja wa Ulaya, huku mzozo wa uhamiaji ukiendelea.

Viongozi hao wawili wa mataifa yenye chumi kubwa zaidi barani Ulaya wanasaka muafaka kati ya mtazamo wa Macron kuelekea mageuzi makubwa kabisa ndani ya Umoja wa Ulaya na ule wa Ujerumani ambayo inataka pachukuliwe hadhari kubwa, hasa linapokuja suala la fedha.

Merkel na Macron, kwa pamoja, wamesisitiza kwamba Rais Donald Trump wa Marekani anaonekana waziwazi kuutishia Umoja wa Ulaya kwa vita vya kibiashara na sera za ulinzi na mabadiliko ya tabia nchi na hivyo Umoja huo unapaswa kujifunza namna ya kusimamia misimamo yake kwenye siasa za kilimwengu.

Mkutano kati ya viongozi hao wawili ulitanguliwa na vikao vya mawaziri kwenye kasri ya Meseberg karibu na mji mkuu, Berlin, ambako kulijadiliwa msimamo wa pamoja kati ya Ujerumani na Ufaransa kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaofanyika tarehe 28 hadi 29 mwezi huu, na ambao utazungumzia suala la Uingereza kujiondoa kwenye Umoja huo - Brexit, katika wakati ambapo vyama vya siasa vinavyoelemea hamasa za umma na vinavyopinga Umoja wa Ulaya vikizidi kupata nguvu.

Upinzani mkali dhidi ya Merkel, Macron

Spanien «Aquarius»-Migranten in Valencia (Getty Images/AFP/P. Barrena)

Meli yenye wahamiaji 630 ikitia nanga Uhispania baada ya kukataliwa Italia na Malta tarehe 17 Juni 2018.

Wakiwa wasemaji watetezi wakubwa wa muungano wa Ulaya, Merkel na Macron wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wa siasa kali kwenye mataifa yao na kwenye serikali za Italia, Austria, na nyengine kadhaa za Ulaya Mashariki.

Kabla ya mkutano huo, Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire, alionya kwamba "Ulaya ipo njiani kuelekea kusambaratika", akiongeza kwamba sasa panashuhudiwa mataifa yakielekea kusaka suluhisho la matatizo ya Ulaya kwenye ngazi ya taifa, badala ya ngazi ya bara zima.

"Ni muhimu kupendekeza mpango mwengine wa Ulaya juu ya uhamiaji, masuala ya kiuchumi na kifedha ili kuwa na Ulaya katika dunia yenye Marekani upande mmoja, China upande mwengine nasi tumenasa katikati," alisema Le Maire.

Sualli la wahamiaji wangapi Umoja wa Ulaya unapaswa kuwachukuwa lilirejea upya wiki iliyopita, baada ya Italia na Malta kuirejesha meli ya uokozi iliyokuwa imechukuwa wakimbizi 630, ambao baadaye, hata hivyo, walipokelewa na Uhispania.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com