Kombe la vijana la Afrika laanza Kigali. | Michezo | DW | 16.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la vijana la Afrika laanza Kigali.

Mabingwa mara 5 Nigeria ni miongoni mwa timu uwanjani Kigali.

default

Ronaldo-jogoo la mwaka

Katika La liga-Ligi ya Spain, jogoo la Kamerun, Samuel Eto-o lilionya klabu yake ya FC Barcelona, kabla haikuingia uwanjani jioni hii kwa changamoto na Depotivo la coruna kutofanya uzembe.Manchester United imeziambia Chelsea na Liverpool "kutangulia si kufika" baada ya kuziba mwanya wake na Liverpool hadi pointi 1 .

Kombe la vijana la Afrika chini ya umri wa miaka 20 linaanza jumapili mjini Kigali,Ruanda -wiki baad ya ya Ugandan Cranes kutawazwa mabingwa wa Kombe la "Challenge Cup" la kanda ya Afrika Mashariki na Kati. FIFA yamtawaza wiki hii mreno, Cristiano Ronaldo ,"mwanasoka wa mwaka".

Firimbi italia kesho(jumapili) mjini Kigali,Ruanda kuanzisha kinyanganyiro cha kombe la vijana la Afrika chini ya umri wa miaka 20-la kwanza la aina hii kanda ya Afrika mashariki.Kinyanganyiro hiki kinafuatia kile kilichomalizika jumaane cha Kombe la CECAFA-kombe la Afrika Mashariki na kati mjini Kampala. Wenyeji Ugandan Cranes walilibakisha Kombe nyumbani walipoitimua nje Harambee Stars ( Kenya) bao 1:0.

Nigeria, ni mabingwa mara 5 wa Kombe hili la vijana la Afrika na imekuwa ikitamba katika Kombe la dunia la vijana pamoja na wenzao Ghana.Miongoni mwa timu zilizowasili Kigali ni pamoja na Mali inayofungua dimba kesho na wenyeji Ruanda.

Wanasoka 2 waligonga vichwa vya habari wiki hii:kwanza Cristiano Ronaldo wa Ureno -jogoo la mabingwa wa dunia,ulaya na Uingereza-manchester united na Kaka,jogoo la Brazil linalocheza dimba Itali kwa AC Milan.

Jane Nyingi anatusimulia kuchaguliwa kwa Cristiano Ronaldo "mwanasoka wa FIFA 2008" baada ya kumpiku muargentina Lionel Messi wa FC Barcelona.

Cristiano Ronaldo,tayari amevikwa taji la "mwanasoka bora wa Ulaya na kutunzwa "Ballon d-Or" la mwanasoka bora wa Ulaya.Jumatatu alizima changamoto kutoka mastadi kama Kaka wa Brazil na Lionel Messi wa Argentina ,Fernando Torres wa Spain ili kuvaa taji hilo la pili.

Baadae,Ronaldo alisema,

"Ni tokeo muhimu katika maisha yangu ya dimba na ningependa kujitolea tajio hili kwa ukoo wangu,marafiki na wachezaji wenzangu."

Ronaldo hakusahau kutoa pongezi zake kwa kocha wa MANCHESTER UNITED Sir Alex Ferguson, licha ya kuwa usuhuba wao uliathirika majira ya kiangazi ya mwaka uliopita ilipovuma kuwa Ronaldo angehamia Real Madrid,nchini Spian.

"Ni kweli kwamba makocha daima wanatoa mchango muhimu."-alisema Ronaldo.

Chipukizi huyu wa Ureno, mwenye umri wa miaka 23,alitia mabao 42 mwaka 2007-8 na alikuwa mmoja wa mafundi wakubwa wa Manchester United kuweza kutwaa vikombe vyote 2 - kombe la ubingwa la Premier League na lile la Champions League.Hatahivyo, Ronaldo hakutamba na timu yake ya Taifa ya Ureno mbele ya Ujerumani wakati wa Kombe la ulaya la Mataifa mwaka jana.Ujerumani iliizaba Ureno mabao 3-2 wakati wa mpambano wao wa robo-finali.

Ronaldo, amekuwa mreno wapili kuvaa taji hili la FIFA baada ya Luis Figo 2001 na ni mchezaji wa kwanza anaecheza katika Premier League-Ligi ya Uingereza.

Cristiano Ronaldo alijipatia pointi 935 katika uchaguzi uliofanywa na makocha na manahodha wa timu za taifa 155 walioshiriki. Lionel Messi wa Argentina akatokea wapili kwa kura 678.Torres alijipatia kura 203 wakati kakya aliekwishachaguliwa kuvaa taji hilo mwaka juzi aliondokea mara hii na kura 183.

Upande wa wasichana,taji la mchezaji soka bora wa mwaka lilivaliwa na mbrazil Marta na hii ni kwa mwaka 3 mfululizo. Marta alitamba maridadi ajabu wakati wa dimba la Olimpik mwaka jana huko China na hivyo amesawazisha rekodi ya msichana wa Ujerumani Birgit Prinz kwa kushinda taji hilo pia mara 3.Katika upande wa wanawake, makocha na manahodha wa timu za taifa 139 walipiga kura na Marta akashinda wazi kwa kura 1,002.Mjerumani Birgit Prinz alitokea mara hii wapili kwa kura 328.

Miongoni mwa washindi wa taji hili la mwanasoka bora wa mwaka wa FIFA tangu kuanzishwa 1991 ni aliekua nahodha wa Ujerumani lothar Mattaues,alieichezea Bayern Munich, mholanzi Marco van basten,aliekua kocha wa Holland katika kombe lililopita la Ulaya,1992 na Roberto baggio wa Itali 1993. George Weah wa Liberia,alivaa taji hilo 1995 alipokuwa akiichezea AC Milan. Miaka ya karibuni,wamevaa taji hilo akina kaka wa Brazilna mwenzake Ronaldinho.Mtaliana Fabio Cannavaro na mfaransa Zinedine Zedane.

Asante Jane Nyingi. mwanasoka wa zamani wa mwaka aliegonga nae vichwa vya habari vya aina yake ni mbrazil Kaka. Manchester City ya uingereza imemdodesha kitita cha rekodi cha dala milioni 150 ikiwa ataiachamkono AC Milan anakocheza na Ronaldinho na kujiunga na Manchester City.

Ujumbe wa watu 4 kutoka Manchester City ulifunga safari hadi Milan mapema wiki hii ukiongozwa na Garry Cook,mkurugenzi wake.ulikutana na wakuu wa AC Milan na kujitolea kumlipa Kaka binafsi kitita cha pauni milioni 15 kwa mwaka baada ya kukatwa kodi.

AC Milan imethibitisha kuwa ujumbe huo wa Manchester city ulifika Milan ,lakini ulidai kwa sasa hakuna mazungumzo ya kumuuza Kaka.

Waziri mkuu wa Itali,Silvio Berlusconi, anaemiliki klabu ya AC Milan, akipinga majaribio ya hapo kabla ya kumtorosha Kaka kwenda klabu nyengine.Kaka binafsi lakini, amesema hapendezwei na mchezo wake katika AC Milan na angehiyari kucheza katika Ligi ya Uingereza.

Mshauri wa Kaka ameionya Manchester City kuthibitisha nia yao ya kumuajiri Kaka kama kweli wana azma hiyo.

Kaka anataka changamoto.Anataka kucheza katika Kombe la UEFA la Champions League na anataka kuibuka tena "mchezaji bora wa dimba wa dunia".Wiki hii,Kaka aliangukia nafasi ya tatu katika kuania taji hilo akija nyuma ya Mreno Christiano ronaldo na Muargentina,lionel Messi huko Uswisi,nyumbani mwa FIFA.

Ligi ya Uingereza-Premier League kama ile ya Spain, La Liga imerudi uwanjani jioni hii:

Manchester United ina nafasi leo (jumamosi) kuparamia kabisa kileleni mwa Premier League ikiondoka na ushindi kutoka Bolton Wanderes.Manu lakini inabidi kucheza bila ya jogoo lao Wayne Rooney,ambae anatazamiwa kuwa nje ya chaki ya uwanja kwa wiki 3.Rooney, aliumia baada ya kutia bao katika lango la Wigan Athletic juzi jumatano .Kwahivyo, Rooney anajiunga na safu ndefu ya wachezaji wa Manu walioumia kama vile Rio Ferdinand,Wes Brown,Owen Hargreaves na mlinzi Patrice Evra.

Mpambano mwengine katika premier league ni kati ya Blackburn Rovers na Newcastle United; Chelsea na Stoke City.

Arsenal london inaitembelea Hull City.Viongozi wa Ligi Liverpool watajua jumatatu iwapo wamesalia kileleni au la au Manu imechukua usukani.Liverpool ina miadi na Everton hapo jumatatu.

katika La liga -Ligi ya spian ,jogoo la Kamerun, Samuel eto-o lilitoa na mapema salamu zake kwa timu yake ya FC barcelona isifanye uzembe ikiwa inataka kweli kutawazwa mabingwa msimu huu.FC Barcelona yenye miadi leo na Depotivo la Coruna ,iliokolewa mwishoni mwa wiki iliopita na bao la dakika ya mwisho la Lionel Messi, walipoitandika Osasuna mabao 3-2. FC Barcelona, inaongoza Ligi ya Spain wakati huu kwa jumla ya pointi 12 na Eto-o hataki wenzake kudhani wameshalitia taji mfukoni.

 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Ramadhan ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ga0Y
 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Ramadhan ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ga0Y
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com