1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Ulaya

17 Juni 2008

Ujerumani imekata tiketi yake ya robo-finali kwa kuwalaza wenyeji Austria bao 1:0

https://p.dw.com/p/EL3K
Ballack akipongezwa kwa bao lake maridadi.Picha: AP

Ujerumani jana iliifuata Croatia duru ijayo ya robo-finali ya kombe la ulaya la mataifa baada ya kuwapiga kumbo wenyeji Austria kwa bao 1:0 la nahodha Michael Ballack, mjini Vienna.Ujerumani sasa ina miadi alhamisi hii ijayo na Ureno kuania tiketi ya nusu-finali.

Leo jioni, ni marudio ya finali ya kombe la dunia 2006 :Itali -mabingwa wa dunia, wanapigana kufa-kupona na makamo -bingwa wa dunia -Ufaransa kuepuka kupigwa kumbo nje ya mashindano katika duru ya kwanza.Holland,iliokwishakata tiketi ya robo-finali ina miadi na Rumania.

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew, ameshusha pumzi kama vile ilivyofanya Ujerumani nzima kuiona Ujerumani ikimtuliza shetani jana usiku na kutwaa tiketi ya robo-finali ya kombe hili la Ulaya.Kocha Loew ametanabahi pia ili Ujerumani itambe alhamisi ijayo dhidi ya Ureno na kusonga mbele zaidi, itabidi kucheza bora zaidi.

Nahodha wa Ujerumani,anaeichezea Chelsea, Michael Ballack aliliiokoa jahazi lake lisiende mrama pale mnamo dakika ya 49 ya mchezo alipovunja ubishi wa wenyeji Austria kwa mkwaju wake mkali na maridadi ajabu wa 'freekick" ambao kipa wa Austria hakuona:

Kocha wa Ujerumani aliechukua usukani baada ya kombe la dunia kutoka kwa Jürgen klinsmann,Joachim Loew, alinukuliwa kusema,

"Tumewapiga kumbo nje ya mashindano wenyeji,tumeingia duru ijayo na tumenyakua pointi 6. Lakini, ni wazi pia inatupasa kucheza bora zaidi katika robo-finali."

Aliongeza kusema kwamba , amefurahishwa kuonesha jana kwamba Ujerumani imestahiki kuingia robo-finali ingawa haikucheza kwa nguvu zaidi kama ilivyobidi kucheza.

Nahodha Michael Ballack alisema:

"Baada ya mpambano na Croatia, tuliingia katika utata huu na hivyo , hungetaraji kujikwamua kirahisi.Muhimu ,ni kuwa leo tumepigana kidume na tumeingia duru ijayo."

Akijiandaa sasa kwa changamoto na Ureno hapo alhamisi, kocha wa Ujerumani Joachim Loew alisema,

"Ureno ni timu kali kiufundi,tangu kwa mchezaji mmoja moja na hata kama timu.Wana uchu wa kutia magoli na bila shaka, ni moja ya timu zinazoweza kuibuka mabingwa,lakini, na sisi hatutaki kuachwa nyuma."-alisema Loew.

Katika changamoto ya pili jana, Croatia iliizaba Poland bao 1:0 na hivyo, imeibuka kileleni mwa kundi hili la 2 ikiwa na jumla ya pointi 9.Croatia ina miadi na Uturuki hapo alhamisi .

Leo ni marudio ya finali ya kombe la dunia 2006 hapa Ujerumani,bila ya Zidane na Materezzi-mabingwa wa dunia-Itali wanaumana na makamo-bingwa Ufaransa.Na wanapopigana mafahali 2 ,ziumiazo ni nyasi. Holland inacheza na Rumania.