1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Ulaya la Mataifa uwanjani kesho.

6 Septemba 2010

Kombe la Afrika:tanzania na Algeria (I:1)

https://p.dw.com/p/P5WL
Miroslav Klose, wapili kulia.Picha: AP

Kinyan'ganyiro cha Kombe la ulaya la Mataifa kinaendelea Ujerumani kesho ina miadi na Azerbaijan baada ya kuitoa Ubelgiji juzi kwa bao 1:0.

Taifa Stars-Tanzania, yatoka suluhu bao 1:1 na Algeria kuania kufuzu kwa Kombe la Afrika 2012

-Uganda, iliichezesha Angola kindumbwe-ndumbwe na kuiabisha kwa mabao 3:0.

Mkenya Daniel Rudisha, atia tena fora kwa Afrika katika mashindano ya riadha ya Kombe la dunia huko Zagreb,Croatia.

Wakati Ufaransa, imeteleza tena mara hii katika duru ya kwanza ya kufuzu kwa Kombe la Ulaya la Mataifa,pale chini ya uongozi wa kocha mpya na nahodha mpya ilipokandikwa bao 1:0 nyumbani na Belorussia, Ujerumani, iliipiga kumbo Ubelgiji mjini Brussels kwa bao la Miroslav Klose na kuondoka na pointi zote 3.

Kesho, Ujerumani, inarudi uwanjani katika kinyan'ganiro hiki ikiwa na miadi mjini Cologne na Azerbaijan:Miroslav klose, anatarajia mpambano wa kesho na chipukizi Azerbaijan kuwa mgumu zaidi kuliko ile changamoto kati ya Ujerumani na Uingereza au Argentina katika Kombe lililopita la dunia huko Afrika Kusini.Kwani, Ujerumani, huenda isivinjari vya kutosha kuifunga Azerbaijan kuliko inavyovinjari ikiwa inazikabili England na Argentina.

Kwahivyo, Klose amewaonya wenzake kuwa macho,kwani Azerbaijan, itataka kuwatia munda kama Ufaransa ilivyotiwa munda na Belorussia,juzi mjini Paris.

Ujerumani, ilitokea 3 katika Kombe lililopita la dunia,nyuma ya Spain na Holland na iliitimua nje Azerbainjan nyumbani na ugenini katika kinyan'ganyiro cha kuania tiketi za Kombe lililopita la duinia.Kesho, timu hizi mbili zinakutana tena.

Ufaransa, ikiongozwa na kocha mpya Laurent Blanc , alieshika usukani kutoka kocha alieaibishwa Raymond Dominique,ilianza vibaya Kombe hili kama ilivyoanza kampeni yake ya kufuzu kwa Kombe la dunia Afrika Kusini ilipolazwa na Austria mabao 3:1 .Juzi, Ufaransa ikiongozwa na nahodha mpya Florent Malouda,ilifedheheshwa kwa bao 1:0 tena nyumbani.

Belorussia inasimama nafasi ya 78 ya ngazi ya timu bora za FIFA.Matokeo kama hayo anaungama Malouda, yanabainisha sura halisi ya Ufaransa wakati huu. Anasema, "Nafasi ya 21 ya Ufaransa katika ngazi ya FIFA inaonesha hali halisi ilivyo."

Stadi wa zamani wa Ufaransa na rais wa sasa wa UEFA-Shirikisho la dimba la Ulaya, Michel Platin, anasema Ufaransa ,nchi yake hivi sasa haina mastadi wakubwa wa dimba na Malouda alievaa utambi mkononi kama nahodha mpya dhidi ya Belorussia, anakubaliana nae.

Hata barani Afrika mwiwhoni mwa wiki, kilianza kinyan'ganyiro cha kufuzu kwa Kombe lijalo la Afrika la Mataifa 2012 litakaloaniwa Gabon kufuatia lile lililoaniwa Angola, mapema mwaka huu:

Wakati Spain imeanza uzuri kutetea taji lake la ulaya ,mabingwa wa Afrika Misri, wameteleza tena kama walivyofanya katika Kombe la dunia.Misri,ilimudu sare ya bao 1:1 tena nyumbani na chipukizi Sierra Leone.

Mnamo dakika ya 56 ya mchezo, Alhassan Bangura, alihanikiza kwa shangwe katika Uwanja wa Cairo,alipoipatia timu yake bao.Jibu la (mafiraouni) lakini, halikukawia, kwani , mlinzi wa Misri,Fathallah, alisawazisha dakika 4 tu baadae.Misri ikitamba na wachezaji 6 wa timu ilioilaza Ghana katika finli ya Kombe la Afrika,huko Angola, haikuweza kufua dafu na kuondoka na ushindi nyumbani.

Kocha wa Misri, "sultani "wa dimba Hassan Shehata aliionya timu yake kutofanya uzembe wa kuanza kinyan'ganyiro hiki vibaya kama ilivyoanza Kombe la dunia 2010 ilipotoka sare pia na Zambia tena nyumbani.

Misri, ndio timu nambari one barani Afrika katika orodha ya FIFA ya mwezi huu wakati Sierra Leone, imeangukia nafasi ya 36.Sierra Leone ilicheza bila ya stadi wao anaecheza China, Mohammrd Kallon.

Ghana,Black Stars, nyota yao ilinawiri tena huko Swaziland pale ilipoitimua Swaziland huko King Mswati Stadium ,mjini Mbabane kwa mabao 3-0.Alikua mwana wa Abedi Pele, Andrew Ayew, alielifumania kwanza lango la Swaziland mnamo dakika ya 13 ya mchezo na baada ya kuzima vishindo vya waghana dakika za kwanza, waswazi waliachia mabao zaidi kutoka kwa Prince Tagoe na Hans Sarpei,mastadi wa Bundesliga.

Nigeria, iliopigwa kumbo duru ya kwanza tu katika kombe la dunia Afrika Kusini na kurudi nyumbani na pointi 1 tu waliondoka na ushindi wa mabao 2:0 dhidi ya Madagascar.Senegali imetoa ishara kwamba, enzi yake ya dimba waliponawiri katika Kombe la dunia 2002,huenda ikarudi tena:

Senegal, iliwatafuna simba wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa mabao 4-2.Wakitiwa shime na El Hadj Diouf, wasenegal walifika robo-finali ya Kombe la dunia 2002 kama Ghana, mwaka huu 2010.Zambia , ilitamba nyumbani na kuilaza Comoro mabao 4-0 mjini Lusaka .Cedric Amissi, aliipatia Burundi bao la kusawazisha 1-1 huko Benin, kama vile Zimbabwe na Liberia zilivyoachana sare.

Taifa Stars,Tanzania ikitamba na kocha wake mpya, iliitoa jasho Algeria, mjini Algiers na licha ya kutoridhishwa na rifa alivyoendesha mchezo huo, Tanzania imerudi Dar-es-salaam na pointi 1.Kenya, imelazwa bao 1:0 na Guinea-Bisau katika kinyan'ganyiro hiki cha kuania tiketi za Kombe la Afrika, 2012.

Katika uwanja wa riadha, mkenya Daniel Rudisha, anaendelea kutamba.Mwishoni mwa wiki,huko Zagreb,Croatia, alikimbia muda nje ya rekodi yake ya dunia kushinda mbio za mita 800 kwa dakika 1:43,37 katika mashindano ya Kombe la riadha la dunia akiiwakilisha Afrika.

Ama katika mita 3000 wanaume kuruka viunzi-steeplechase,Richard Kipkemboi Mateelong, aliipatia Afrika ushindi huku mwenzake pia kutoka Kenya,Benjamin Kiplagat, alitokea 4.

Ushindi katika mita 3000 bila ya viunzi, ulikwenda kwa muamerika,mzaliwa wa Kenya, Bernard Lagat,alishinda mbio hizo kwa niaba ya Amerika.Moses Kipsiro, alifuata nafasi ya pili kwa Afrika huko Byron Piedra,akitokea 3 kwa Amerika.Ulaya ilimaliza mshindi jumla wa Kombe hilo la dunia la riadha .

Mwandishi:Ramadhan Ali/ AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman