Kombe la klabu bingwa | Michezo | DW | 14.04.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la klabu bingwa

Munich na FC Barcelona: Chelsea na Liverpool

default

Klinsmann ataliokoa leo jahazi ?

Kinyanganyiro cha kombe la klabu bingwa barani Ulaya-champions League, kinarudi uwanjani jioni hii:Wakati mabingwa wa kombe hili Manchester United wanafunga safari hadi Porto,Ureno kwa duru ya pili ya robo-finali,mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich, wameahidi kufuta aibu waliopakwa mjini Barcelona, wiki iliopita walipokomewa mabao 4:0 na akina Lionel Messi,Samuel Eto-o na Thiery Henry.

Chelsea iliokomea Liverpool mabao 3:1,inatumai leo kuzima vishindo vya Liverpool kufuta mabao hayo 3 ikidai jogoo la shamba (Liverpool) halitawika mjini London leo.

Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich wana mlima mrefu zaidi kuupanda leo kuliko mabingwa wa ulaya Manchester United.Munich wanapaswa kufuta mabao 4 waliochapwa na FC Barcelona katika duru ya kwanza ya robo-finali ya Champions League wiki iliopita.Na ingawa mpira unadunda, jinsi Munich walivyochezeshwa klindumbwe-ndumbwe na akina Lionel Messi wa Argentiona na wenzake Samuel Eto-o wa Kamerun na Thierry Henry wa Ufaransa, hakuna anaewaekea tamaa sio tu kusinda leo na kufuta aibu seuze kufuta mabao hayo 4 na kusonga mbele.Bayern Munich imeshpewa mkono wa buriani katika Kombe la ulaya msimu huu na kaburi walikwishachimbiwa huko Barcelona, leo ni kuwazika tu olimpik Arena.

Walipozabwa mabao 4 wiki iliopita, vilio vilisikika kuwa kocha wa Bayern Munich,Jurgen Klinsmann, atimuliwe.Ushindi wa mabao 4 :0 dhidi ya Frankfurt katika Bundesliga Jumamosi iliopita ulimuokoa na kuipa Munich tamaa hii leo,alao kufuta aibu ya wiki iliopita.Fununu zinasema kwamba Barcelona huenda ikampumzisha Mkamerun Samuel Eto-o na hata Thierry Henry, alieumia kidogo.Lionel Messi, ni hatari vya kutosha kuzusha misukosuko katika lango la Munich.

Katika mpambano wapili leo, Liverpool,waliopo nafasi ya pili katika ngazi ya opremier League nyuma ya manchester united, wanawatembelea jioni hii Chelsea,mjini London.Kocha wa Chelsea mdachi guus Hiddink, ameionya timu yake ichunge kwani, LIverpoool iliwahi kutoka nyuma mabo 3:0 katika kipindi cha mapumziko na mwishoe ikaifunga AC Milan na kutwaa Kombe ,2005.

Kinyume na mpambano wa kwanza Liverpool ilipoadhibniwa na Chelsea kwa mabao 3-1, jogoo lao Steven Gerrad linarudi loe uwanjani.Sababu nyengine kwa Chelsea kuwa macho zaidi.

Kesho itakua zamu ya mabingwa Manchester united kuteremka uwanjani huko Porto,Ureno.Mabingwa MANU walimudu sare tu ya 2:2 na wareno Porto wakati wa changamoto yao ya duru ya kwanza huko Manchester.Kesho wanacheza ugenini na wareno wamepania kuwavua taji Manu na mapema.Usisahau pia kwamba Manu haikuwahi kushinda ilipotembelea Porto mara tatu zilizopita.Labda, halali mara ya nne.

Manchester ilitiwa shime kwa mpambano wa leo ilipotamba tena dakika ya mwisho mwishoni mwa wiki ilipoilaza Sunderland mabao 2:1.Isitoshe, mastadi wake 2 wamerejea uwanjani-Jonny Evans na mbulgaria Dimitry Berbatov.

Manu inaweza pia kuanza leo bila mreno wao Cristiano Ronaldo,ingawa angependa kutamba nyumbani.

Kesho pia ni zamu ya Arsenal kuikaribisha timu ya pili ya Spain katika robo-finali:Vilarreal.Wakiwa hawakushindwa mapambano 23 ya Champions League,Arsenal ndio wanaopigiwa debe kushinda nyumbani na kucheza duru ijayo.Na hasa kwavile, Vilarreal itacheza kesho bila Marcos Senna alietia lile bao lao wsalipotoka sare nyumbani na Arsenal.Mla lakini, mla leo,mla kesho kala nini-tuangalie basi nini tena watafanya Barcelona mjini Munich na Liverpool, huko Chelsea,London.

Muandishi : Ramadhan Ali

Mhariri:M.Abdul-rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com