Kombe la dunia 2010 | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 14.06.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Kombe la dunia 2010

Timu ya taifa ya Ujerumani yatoa matumaini mema kwa mashabiki wake nyumbani na ugenini

default

Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Philipp Lahm

Baada ya Ujerumani kuichapa Australia 4-0 jana mjini Durban,vyombo vya habari tangu vya Ujerumani mpaka vya kimataifa vinaisifu timu ya Ujerumani-Die Mannschaft kwa jinsi walivyolisakata dimba ."Tutakutimueni nyote" limeandika gazeti linalosomwa na wengi humu nchini Die Bild" likichambua magoli manne kwa bila ya Ujerumani.

"Wameanza vizuri kabisa wajerumani" ndio maandishi yaliyokua yakitolewa na kituo cha televisheni cha Ujerumani N24 huku kikionyesha picha za mashabiki zaidi ya 34 elfu waliokua wakipepea bendera za Ujerumani katika uwanja mkuu wa michezo mjini Berlin.

Kufuatia ushindi huo wa mabao manne kwa bila,nahodha wa timu ya taifa Philipp Lahm amesema ingawa ni muhimu kwamba wameshinda katika pambano la kwanza na kwamba wana nafasi ya kutamba,lakini amekumbusha kuwa bado kuna safari ndefu.

Mashabiki wamesherehekea katika kila pembe ya Ujerumani-mjini Hambourg walikuwa 60 elfu na sherehe hizo kuendelea hadi alfajiri ya leo huku nzumari-vuvuzela zikihanikiza viwanjani na majiani.

Deutsche Fußballfans in Hamburg WM 2010 Flash-Galerie

Mashabiki waliokusanyika katika uwanja wa mpira wa Hamburg kujionea pambano kati ya Ujerumani na Australia

Walikuwa Lukas Podolski,Miroslav Klose,Thomas Müller na Cacau walioipatia Ujerumani magoli hayo-la kwanza dakika nne tuu tangu firimbi ya mwanzo kulia.

"Tunachokiona hapa hakina mfano-Hili ni dimba la hali ya juu kabisa.Timu ya Ujerumani iko katika hali nzuri na imeanza vyema kabisa mashindano haya" Amesema mlinzi wa zamani wa lango la timu ya taifa Oliver Kahn kupitia kituo cha televisheni cha ZDF.

Vyombo vya habari nchini Uengereza mpaka kufikia Brazil bingwa mara tano wa kombe la dunia wamesifu jinsi vijana wa Joachim Löw walivyolisakata dimba.

"Hawa ni wajerumani lakini sio wale tuliokua tukiwajua" limeandika gazeti la Uengereza The Times.

Nalo The Daily Telegraph likiungama "wakati umewadia kuwacha nyuma fikra kuhusu kabumbu la zamani la Ujerumani."

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani lakini Joachim Löw ingawa ameridhika na kuanza vyema vijana wake,hata hivyo anasema "hakuna haja ya kuzama katika bahari ya furaha."

Leo mchana itakua zamu ya majirani wa Ujerumani Uholanzi kuteremka uwanjani mjini Johannesburg kupimana nguvu na Danemark kabla ya Japan kutoana kijacho na Cameroun huko Blumfontaine ,simba wa nyika watakapojaribu kuipatia ushindi mwengine Afrika baada ya ule wa Ghana wa moja kwa bila dhidi ya Serbia.Mabingwa wa dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani-Italy wanalitia rehani taji lao leo usiku dhidi ya timu ndogo ya Paraguay.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir/dpa,afp

Mpitiaji:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 14.06.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NqF8
 • Tarehe 14.06.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NqF8

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com