kombe la dunia 2010 | Michezo | DW | 08.10.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

kombe la dunia 2010

Kinyanganyiro cha kuania kufuzu kwa kombe la dunia Afrika kusini kitakuwa uwanjani mwishoni mwa wiki:

default

Ballack akipozwa moyo na Merkel

Wakati FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni likiwatawaza tena Spain-mabingwa wa ulaya, pia timu bora ya dimba ulimwenguni na Brazil ikichupa nafasi 2 usoni katika ngazi hiyo ya timu bora,timu kadhaa za Taifa zinajiwinda kwa changamoto za kuania tiketi zao za kombe lijalo la dunia mwishoni mwa wiki.

Michael Ballack,nahodha wa Ujerumani, anaevutana na meneja wa timu ya Taifa Oliver Bierhof,ni wa kwanza kuwasili Dusseldorf jana kujitayarisha kwa mchuano na Urusi na baadae Wales.Katika kanda ya Afrika, Simba wa nyika -Kamerun wanatamba nyumbani dhidi ya Mauritius huku Taifa Stars-Tanzania, wana miadi na Cape Verde ingawa hawana tena matumaini ya kwenda Afrika Kusini 2010.

Katika orodha mpya ya FIFA ya timu 20 bora za dimba ulimwenguni-simba wa nyika-Kameroun ni timu pekee ya Afrika katika klabu hiyo.Kileleni lakini,FIFA imewatawaza mabingwa Ulaya-Spain wakifuatwa na mabingwa wa dunia Itali huku Ujerumani ikiipiku Brazil nafasi ya 3 .Brazil iko nafasi ya 4.

Simba wa nyika -Kameroun wako nafasi ya 12 huku Uruguay -mabingwa wa kwanza wa dunia,wakishika mkia wa timu 20 bora.

Brazil imechupa nafasi 2 baada ya kutoka sare na Bolivia na kuishinda Chile katika mchuano wa kufuzu kwa kombe lijalo la dunia kanda ya Amerika kusini.Ni mwezi wa 4 mfululizo ,Spian ni namba one.

Iwapo timu hizo mwezi ujao zitasalia nafasi zao itaamuliwa na changamoto zijazo mwishoni mwa wiki hii za kufuzu kwa kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini.Ujerumani ina miadi na Urusi na baadae Wales na nahodha wake anaeichezea Chelsea,Michael Ballack ameshawasili kwa mazowezi mjini Dusseldorf.

Alipowasili, kocha wa taifa Joachim Loew alijaribu kuzima mvutano ulioibuka kati ya nahodha Ballack na meneja wa timu ya Taifa Oliver Bierhoff uliozuka pale Ujerumani iliposhindwa na Spian katika finali ya kombe la ulaya la mataifa hapo Juni.

Hatima ya kocha wa Ufaransa-makamo-bingwa wa dunia Raymond Dominique inategemea sana ushindi jumamosi hii dhidi ya Rumania.Dominique lakini hataweza kumtegemea Nicolas Anelka wa Chelsea kwani ameumia .Ilikua Anelka alilifumania lango la Aston Villa kwa bao la pili juzi jumapili kabla hakuchechemea na kutoka nje ya uwanja.

Ufaransa inajikuta nafasi ya 4 katika kundi lake kufuatia mapambano 2 na baada ya mpambano na Rumania jumamosi hii, ina miadi na Tunisia kwa mapambano wa kirafiki katika Stade de France,mjini Paris siku 3 baadae.

Katika kanda ya Amerika kusini,Brazil wanahitaji ushindi kwa kila hali ili kumpunguzia kocha wao dunga mzigo mzito mabegani mwake.Kwani, Brazil haikuwa ikicheza uzuri karibuni na mwishoe ilimudu sare tu ya 0:0 nyumbani na Bolivia mwezi uliopita.Brazil iliopo nafasi ya 2 katika orodha ya timu 10 za kanda ya Amerika Kusini, ni timu pekee isiowahi kukosa kucheza katika kila kombe la dunia tangu Montevideo,Uruguay, 1930.

Brazil itamtegemea Kaka wa AC Milan endapo atarudi katika timu ya taifa jumapili hii dhidi ya Venezuela. Mahasimu wao wakubwa Argentina watakuwa uwanjani tayari jumamosi wakichuana na Uruguay huku Columbia wanacheza na Paraguay.Bolivia mahasimu wao ni Peru.

Ama katika kanda ya Afrika ,timu kadhaa zitakuwa uwanjani hapo jumamosi: Kamerun inacheza nyumbani na Mauritius wakati katika kundi hili la kwanza, Taifa Stars-Tanzania wako pia nyumbani wakiikaribisha Cape Verde.

Katika kundi la 2,Kenya-"Harambee Stars" wako Guinea wakati Waganda wanabaki nyumbani wakicheza na Benin.Wenyeji "Bafana Bafana" watafunga safari hadi Guinea ya Ekweta.Nigeria itaumana na Sierra Leone.Ghana inatamba nyumbani mbele ya Lesotho huku Tembo wa Ivory Coast bila ya nahodha wao Drogba alieumia wanacheza na Madagascar.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com