1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Afrika-robo-finali kesho

22 Januari 2010

Angola na Ghana

https://p.dw.com/p/Ledj
Mashabiki wa Angola waanza kushangiria.Picha: AP

Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola linaanza kesho Ijumapili duru ya pili ya kutoana kwa wenyeji Angola wakichuana na Black Stars Ghana bila ya jogoo lao Michael Essien.

Mabingwa mafiraouni Misri, wanaotapia taji hili kulitwaa kwa mara ya 3 mfululizo wana miadi mengine na Simba wa nyika-kameroun, marudio ya finali ya Kombe lililopita nchini Ghana.Je, simba wa nyika waliomudu sare kwa taabau na Tunisia, wataweza kunguruma mbele ya mafiraouni ?

Nini hatima ya Nigeria mbele ya chipolopolo-Zambia na vipi Algeria ?

Bundesliga nayo inaendelea leo kwa mapambano yalio uwanjani wakati huu kati ya Bremen na Bayern Munich. Nani ataondoka na pointi 3 ?

Timu zote 5 za Afrika zitakazocheza katika Kombe lijalo la dunia hapo Juni nchini Afrika Kusini, zimekata tiketi zao ingawa baadhi kwa taabu kwa duru inayoanza kesho ya robo-finali ya kombe hili la Afrika.

Kameroun, ilikuwa timu ya mwisho kufuzu kwa duru hiyo ya timu 8 kutoka 15 zilizoanza kuania kombe hili,Juni 10.Simba wa nyika walikata tiketi yao chupuchupu kwa wingi wa bao 1 tu walipoipiga kumbo tunisia.Timu 4 kati ya hizo 5 za kombe la dunia-yaani Algeria,Cameroun,Ghana na Nigeria zilishindwa mpambano wao wa kwanza wa kuania Kombe hili na wakalazimika kutoka nyuma kuwa mojawapo ya timu 2 za kileleni mwa makundi yao.

Tembo wa Ivory Coast ,ni timu pekee kati ya hizo za Kombe la dunia nchini Afrika kusini isioshindwa hadi sasa katika kinyan'ganyiro hiki. Tembo lakini wamecheza mechi 2 tu nchini Angola kutokana na kujitoa kwa Togo katika kundi lao.Ivory Coast iliteleza ilipomudu sare tu na chipukizi Burkina Faso katika mpambano wao wa awali nchini Angola huko Cabinda.hii ilikuwa kabla Ivory Coast ikiongozwa na nahidha wao didier drogba haikuichapa Ghana.

Algeria ilikata tiketi yake ya robo-finali kwa kutegemewa bao 1 tu lililotiwa kimiyani na Rafik Halliche walipoitimua nje Mali wakati wa mpambano wao wapili wa kundi A. Algeria, ilianza kwa pigo kali la mabao 3:0 kutoka chipukizi Malawi na imefuzu kwa duru hii ya pili -shukurani kwa kutoka sare 0:0 na wenyeji Angola.Simba wa nyika wanashukuru kwa kutia bao 1 zaidi kuliko Gabon .

Black Stars Ghana wenye miadi kesho ya kuanza duru hii ya pili na Angola ,walipaswa kungoja wiki nzima kabla ya kuanza kampeni yao halafu wakakandikwa mabao 3:1 na Tembo Ivory Coast. kama msumari juu ya donda, wakampoteza stadi wao wa kiungo Michael Essien alieumia kabla kuitimua nje Burkina faso kwa bao 1:0 la mwana wa Abedi Pele.

Nigeria, walichezeshwa kweli kindumbwe-ndumbwe na mabingwa Misri katika mpambano wao wa kwanza lakini mwishoe, walimaliza wapili katika kundi lao baada ya kuilaza Benin na mwishoe Msumbiji.

Misri,mafiraouni, wanaotapia taji lao la 3 mfululizo na la 7 kwa jumla ,hadi sasa imetamba mbele ya timu zinazokwenda Afrika kusini kwa Kombe la dunia na watakaponana na simba wa nyika -Kameroun keshokutwa Jumatatu huko Benguela, itakua marudio ya finali ya kombe lililopita nchini Ghana.Siku hiyo hiyo, Chipolopolo-Zambia, itaifyatulia risasi zake Nigeria huko Lubango.Nusu-finali itachezwa alhamisi ijayo wakati finali ni Januari 31 mjini Luanda, ambako wenyeji Angola, wanaahidi baada ya kuitimua Ghana kesho,watawasubiri mahasimu wao-ama Misri,Ivory Coast au Kameroun na hata Nigeria.

Ama katika changamoto za Bundesliga, uwanjani dakika za mwisho hivi sasa (Jumamosi) , mabingwa mara kadhaa Bayern Munich, wana kibarua kigumu kuondoka na pointi zote 3 kutoka mahasimu wao Werder Bremen.Huu ndio mpambano unaokodolewa macho sana kujua iwapo Munich, yaweza kuwapiku viongozi wa Ligi Bayer Leverkusen,inayofuatwa nyuma na Schalke.FC Cologne, inacheza na mabingwa Wolfsburg ambao lazima washinde leo nyumbani ili kumnusuru kocha wao.

Kesho Jumapili,Bundesliga itaendelea kwa mapambano 2.

Mwandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Uhariri: