Kombe la Afrika la Mataifa | Michezo | DW | 04.02.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Kombe la Afrika la Mataifa

Mabingwa Misri wanaania leo tiketi ya nusu-finali kati yao na Angola wakati Kamerun inaumana na Tunisia.

Mabingwa Misri watateremsha uwanjani kikosi kamili hivi punde kupambana na Angola wakati katika robo-finali ya pili Simba wa nyika Kamerun wanaonana na Tai wa Carthage-Tunisia.

Mashabiki wa Ghana walimiminika jana mitaani kushangiria ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao wa jadi Nigeria huku hatima ya kocha mjerumani Berti Vogts ikinin’ginia hewani.

Katika robo-finali ya pili-Tembo wa Ivory Coast waliwakanyaga Guinea vibaya sana walipowazima kwa mabao 5-0.Mtasikia jinsi mashabiki nchini tanzania wa,livyopigwa na homa ya Africa Cup nchini Ghana.

Katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani Werder Bremen ilichezeshwa jana kindumbwe-ndumbwe nyumbani na kuzabwa mabao 2-1 na Bochum ikiachia bayern Munich kupanua mwanya wake kileleni kwa pointi 3.

Katika medani ya riadha bingwa wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita 100 muamerika Maurice Green atangaza kustaafu nusu mwaka kabla olimpik na malkia wa mbio ndefu wa Ethiopia-bingwa wa Olimpik Meseret Defar,akimbia muda bora kabisa wa masafa ya mita 3000 mjini Stuttgart,Ujerumani.

Katika mapambano 2 ya robo-finali ya Africa Cup-kombe la Afrika la mataifa jioni hii nchini Ghana ,kwanza mabingwa Misri watakua uwanjani hivi punde na Angola kuania tiketi yao ya nusu-finali.Kocha wa mabingwa hao Hassan Shehata ana jumla ya washambulizi kuchagua kwavile sasa mkuki wake Mohamed Aboutrika uko fit sawa sawa na Mohamed Zidane ana uchu pia wa kutia magoli.

Misri lakini haitazamii mtetermko kwa angola, kwani timu hizi 2 zilipokutana mwezi uliopita tu kirafiki zitlitoka suluhu mabao 3:3.jioni hii lakini,hakuna suluhu mjini Kumasi,kwani tangu Misri hata Angola inataka tiketi yake ya kukutana na tembo wa Ivory Coast katika nusu-finali baada ya Ghana jana kuitoa Nigeria na kuchukua tiketi ya kwanza kati ya 4.

Katika mpambano wapili wa robo-finali jioni hii,Tunisia ina miadi na simba wa nyika kamerun.Samuel Eto’o aliekwishapachika mabao 5 katika kombe hili la Afrika na kuweka rekodi mpya ya mabao katika kombe hili kuwa 16,atatarajiwa kuongeza mabao yake.Tunesia itamtegemea leo mzaliwa wa Brazil Dos Santos kuufumania mlango wa simba wa nyika na kuwaadhibu kamerun kama vile wenzao wa Afrika Kaskazini Misri walivyofanya walipowazaba mabao 4-1.

Mshindi katika mpambano huu wapili leo atakutana na wenyeji Black Stars-Ghana:

Waghana jana walimiminika mitaani mjini Accra na kila mahala ilikua shangwe na shamra-shamra baada ya Black Stars kuwapiga kumbo mahasimu wao wa jadi Nigeria kwa mabao 2:1.Licha ya kucheza na wachezaji 10 tu baada ya nahodha wao John Mensah kutolewa nje ya uwanja na rifu kwa kucheza ngware,Ghana iliitoa Nigeria kufuatia mabao la pili la Agogo.Mashabiki wa Ghana walibeba jeneza lililovikwa kitambaa cha rangi ya kijani-yaani jazi ya Nigeria wakiashiria buriani kwa Green Eagles. Kwa ushindi huo,Ghana imelipiza kisasi kwa mapigo kadhaa iliopata miaka ya karibuni kutoka kwa majirani zao Nigeria.

Wakati lakini waghana ,wakisherehekea, wanigeria wakiomboleza mjini Abuja na Lagos.Kwani, ilikua Nigeria iliotangulia kutia bao kabla Michael Essien kusawazisha kwa Ghana.Na licha nahodha wa Ghana John Mensah kutimuliwa nje ya uwanja,Nigeria hawakufua dafu.Mashjabiki wakijuliza ilikuaje kocha wao mjerumani Berti Vogts ,hakufanya mageuzi katika kikosi chake na kuwabadilisha wachezaji waliochoka kama alivyofanya mfaransa Claude Leroy wa Ghana.

Mashabiki wengine wa Nigeria walimtazamia Berti Vogts kuwateremsha uwanjani akina Obafemi Martins na Nwanko Kanu.Hatima ya Berti Vogts iwapo atabakia kuingoza Nigeria hadi kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika Kusini au atafungishwa virago karibuni itajulikana karibuni.

Bundesliga-Ligi ya Ujerumani imerudi uwanjani kwa kishindo mwishoni mwa wiki hii baada ya likizo yax-masi na mwaka mpya.Wakati ilipokwenda likizoni timu 2 zilipishana kwa magoli tu-Munich na Bremen, jana Bremen iliteleza ilipozabwa tena nyumbani mabao 2:1 na Bochum.Daniel Jensen aliufumania kwanza mlango wa Bochum kwa bao la kwanza muda mfupi kabla mapumziko.Benjamin Auer akasawazisha bao hilo mnamo dakika ya 68 ya mchezo.

Halafu mlinzi wa Bremen mbrazil Naldo akapewa kadi nyekundu na rifu kwa kucheza ngware.Dakika 2 tu baadae, Anthar Yahya akalifumania lango la Bremen na Bochum kwa msangao wa wengi ikatoroka na pointi 3 kutoka Bremen.Hii iliiwezesha B.Munich kufungua mwanya wa pointi kileleni kati yake na Bremen .Munich iliizaba Hansa Rostock jumamosi kwa mabao 2-1.

Katika premier League-Ligi ya Uingereza,Arsenal ilibadilisha nafasi kati yake na Manchester United kileleni mwa Ligi hiyo hapo jumamosi.Arsenal ilikomea Manchester City mabao 3-1 wakati Manchestzer United ilimudu suluhu tu ya bao 1:1 na Tottenham Hotspurs.Chelsea inajikuta nafasi ya 3 nyuma ya Manchester united na Arsenal.

Nje ya dimba ,wanariadha 2 wamegonga vichwa vya habari mwishoni mwa wiki hii: Bingwa wa olimpik wa Ethiopia-Meseret Defar alishinda jana mbio za masafa ya mita 3000 kwa muda bora kabisa ulimwenguni.Bingwa huyo wa Olimpik wa mita 5000 alichukua muda wa dakika 8 na sek. 27.93.Defar alikimbia muda bora zaidi wa dakika 8 na sek. 23.72 mwaka uliopita.

Bingwa mwengine wa olimpik na wa dunia wa masafa ya mita 100 Maurice Green wa Marekani,aliamua kustaafu kutokana na kuumia.Green mwenye umri wa miaka 33 amearifu kwamba sasa anatazamia kuwa kocha na kufanya biashara nchini Marekani.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com