Kiongozi wa Sudan Kusini atangaza msamaha kwa wanamgambo | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Kiongozi wa Sudan Kusini atangaza msamaha kwa wanamgambo

Hatua hiyo ni kwa ajili ya kuweka kando tofauti zao wakati ambapo kura ya maoni kuhusu uhuru wa eneo hilo ikiwa inakaribia mwanzoni mwa mwaka ujao.

Kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir.

Kiongozi wa Sudan Kusini, Salva Kiir.

Viongozi wa Sudan Kusini wanaweka kando tofauti zao pamoja na makundi ya waasi na mahasimu wao katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika wakati ambapo kura ya maoni kuhusu uhuru wa eneo hilo inakurubia kuitishwa mwezi Januari mwakani.

Rais wa eneo la kusini mwa Sudan, Salva Kiir ametangaza kuwasamehe wanamgambo na anapanga kufanya suluhu pamoja na hasimu wake mkubwa wa kisiasa, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Lam Akol, katika juhudi za kumaliza mivutano wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi. "Kuna haja ya kuwa na mshikamano kama wakaazi wa kusini mwa Sudan, "amesema Kiir mbele ya wajumbe waliohudhuria mkutano wa siku tatu wa chama cha Muungano wa wasudan wa kusini-ASSPP, ulioanza hapo jana mjini Juba, mji mkuu wa jimbo hilo.

Bwana Kiir amesema yanahitajika kuwepo makubaliano kati ya wananchi kwa ajili ya kuufanya uchaguzi huo wa kura ya maoni uwe huru, wa haki, uwazi pamoja na wa amani. Uchaguzi huo ni kilele cha mpango wa amani wa mwaka 2005 uliofikiwa kati ya kundi la zamani la waasi wa kundi la Sudan People's Liberation Movement-SPLM na serikali inayotawaliwa na Waarabu ya Khartoum na kumaliza vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe vilivyowaua kiasi watu milioni mbili.

SPLM inaongoza serikali ya eneo linalojitawala lenyewe ambalo lilianzishwa kwa kuzingatia mpango wa amani, lakini limeendelea kukabiliwa na upinzani kutoka kwa makundi ya wapiganaji ambayo yanaliunga mkono eneo la kaskazini ka

tika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miongo miwili. Akimkaribisha Bwana Akol katika mkutano huo, Kiir alimwambia mpinzani wake huyo kuwa tofauti za kisiasa zisiwe kikwazo kwa maslahi ya umma. Akol, ambaye aliliasi kundi la SPLM wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 1983 hadi 2005, alikuwa ni mpinzani pekee kwa Bwana Kiir katika uchaguzi wa urais wa Sudan Kusini wa mwezi Aprili, mwaka huu.

Mwaka uliopita, Bwana Akol alianzisha chama kingine cha SPLM-Democratic Change na mara kwa mara amekuwa akishutumiwa na chama tawala cha Kiir kwa kujaribu kudhoofisha kura ya maoni hapo mwakani. Akol ameliambia shirika la habari la AFP kuwa jambo muhimu kwa wote ni kujenga mazingira mazuri ya kufanyika kwa uchaguzi huo. Bwana Kiir ametangaza msamaha huo kwa viongozi wa makundi yote ya wapiganaji, akiwemo Gabrial Tang, ambaye sasa ni afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la kaskazini. Wengine ni Kanali Gatluak Gai na George Athor.

Kiongozi huyo wa Sudan Kusini ameyataka makundi yote hayo kuweka silaha chini ambazo wamekuwa wakizitumia dhidi ya uongozi wa kusini na kuwataka waelezee tatizo wanaloliona ambalo bado halijatatuliwa. Akizungumza na redio inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya Miraya FM, Bwana Athor alisema wameukubali msamaha huo na kuongeza kusema kuwa watapeleka ujumbe kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wa kusini. Bwana Kiir amesema kuwa hakuna tone la damu litakalomwagika tena.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 14.10.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PeMU
 • Tarehe 14.10.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PeMU
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com