Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ziarani China | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.07.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ziarani China

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameitaka China ishirikiane na mataifa mengine duniani katika juhudi za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira

default

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa-Ban Ki-moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ameitaka China ishirikiane na mataifa mengine duniani katika juhudi za kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira.

Ki-moon amesema mpango mpya wa kimataifa kukabiliana na uharibifu wa mazingira hauwezi kufikiwa pasipo ushirikiano wa China.

Katibu Mkuu huyu ameyasema hayo wakati akizindua programu mpya ya kuhamasisha uboreshaji wa mazingira nchini China.

Amesema china ni mdau mkubwa duniani katika kufanikisha makubaliano ya Copenhagen.

Katibu Mkuu Ki-moon anatarajiwa kuongoza mkutano wa kimataifa wa wadau wa mazingira nchini Denmark,Desemba mwaka huu wenye lengo la kudhibiti gasi zinazolalamikiwa kuchafua mazingira.

Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo amesema kitendo cha China kuonesha umadhubuti kwa vitendo katika kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa ni jambo litakalosaidia kufikia makubaliano kabla ya mkutano wa Copenhagen.

Aidha itasaidia kuonesha njia ya uwajibikaji kwa nchi nyingine husika na pengine kufanya zaidi ya hivyo.

China na nchi nyingine zinazoendelea zinapinga kupunguza matumizi ya gesi zinazidaiwa kuchafua mazingira kwa kudai kuwa jukumu la kudhibiti uharibifu huo ni la nchi zilizoendelea ambazo zimechangia kuweko tatizo hilo kwa muda mrefu.

Lakini Ki-moon anasema China ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa uchafuzi wa mazingira na kwamba inapaswa kujitolea kwa hali na mali kukabiliana na tatizo hilo.

Amesema nchi hiyo imefanya juhudi kadhaa katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa kutumia nishati ya jua na upepo, lakini pia ametaka kupunguzwe matumizi ya makaa ya mawe ambayo yanachangia uharibifu mkubwa wa hali ya hewa.

Makaa ya yanachukua asilimia 70 ya nishati zinazotumiwa viwandani nchini China na kusababisha asilimia 85 ya hewa chafu.

Mdau mwingine kutoka Taasisi ya Kukabiliana na Uharibifu wa Mazingira nchini China-Green Peace, Li Yan, amesema kuna ishara ya China kupunguza matumizi ya gesi zinazochafua mazingira kutokana na shinikizo la kimataifa na kitaifa kutokana na athari za ndani.

Mwanaharakati huyo amesema kutokana na hali ilivyo sasa, kuna mategemeo makubwa ya China kuleta mapendekezo mapya kuhusu ustawi wa mazingira.

Green Peace ilitoa wito kwa serikali ya China kutaka kupunguza matumizi ya gesi zinazoleta athari za kimazingira kwa kiwango cha asilimia 15 mpaka 30 ifikapo mwaka 2020.

Ripoti za Serikali ya nchi hiyo kwa mwaka huu zinadai China imeanza kufanya juhudi za kupunguza vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kutumia nishati mbadala, ingawa hazijawa wazi kama mpango huo umefikia hatua gani.

Ban-Ki-moon amesema matakwa ya China yakiendelea basi nchi hiyo na jirani zake zitegemee kuongezeka kwa hali ya jangwa, kupoteza ujoto wa asili na kuyeyuka kwa theluji katika maeneo ya milima ya Himalaya.

Marekani yenyewe imeahidi kupunguza matumizi ya hewa zinazoharibu mazingira kwa asilimia 17 kuanzia mwaka 2005 mpaka 2020 lakini China inalalamika kwamba kiwango hicho ni kidogo.

Ban Ki-moon leo hii anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa China Wen Jiabao Pamoja na Rais wa nchi hiyo Hu Jintao.


Mwandishi-Sudi Mnette AFPE

Mhariri-Othman Miraji • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IwbZ
 • Tarehe 24.07.2009
 • Mwandishi Nina Markgraf
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IwbZ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com