1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe Biden: Mgombea mwenza wa Barack Obama

Othman, Miraji27 Agosti 2008

Jee Joe Biden atakuwa makamo wa rais wa baadae wa Marekani?

https://p.dw.com/p/F5o4
Joe Biden(kushoto) na Barack Obama, kila mmoja akimkumbatia mkewePicha: AP

Miezi miwili kutoka sasa, Wamarekani watamchagua rais mpya wa nchi yao, na hivi sasa katika mji wa Denver, katika Mkoa wa Colorado, kunafanyika mkutano mkuu wa Chama cha Democratic ambapo wajumbe 4,000 wanamchagua Barack Obama kuwa mtetezi wa urais kwa niaba ya chama hicho. Lakini kabla ya tokeo hili, mwisho wa wiki iliopita katika mji wa Springfield, katika mkoa wa Illinois, ambapo karibu miaka 150 iliopita mwanasiasa kijana, kwa jina la Abraham Lincoln, alionya juu ya matokeo mabaya ya kuendelea na biashara ya utumwa, Barack Obama alitangaza jina la mtu atakayekuwa mgombea wake mwenza wa urais wa chama chake. Springfileld ni mahala hapo hapo ambapo Barack Obama mnamo Februari mwaka 2007 alianzisha kampeni yake ya kutaka kuwa rais. Mtu aliyemtangaza kuwa makamo wa rais wa Marekani, pindi yeye atashinda kuwa rais, ni Joe Biden, seneta wa Mkoa wa Delaware, wakili ambaye ametumika katika Baraza la Senate kwa miaka 36, tena mzoefu aliyebobea katika masuala ya siasa za kigeni. Kwa mbwembewe Obama aliwaambia hivi washabiki wake:

"Hebu nikujulisheni makamo wa rais wa baadae wa Marekaní- Joe Biden ( Applaus)."

Barack Obama akaongeza:

"Zaidi ni kwamba nimemtafuta kiongozi ambaye aliye tayari kuingia na kuwa rais. Leo nimerejea hapa Springfiled kukwambieni kwamba nimempata kiongozi huyo."

Naye Joe Biden hajajivunga, alijibu namna hivi juu ya heshima hiyo aliyotunukiwa:

"Akina Mama na akina baba, huu sio uchaguzi wa kawaida, na hii inaweza kuwa ni nafasi yetu ya mwisho ya kuidai tena Marekani tunayoipenda, kuurejesha moyo wa Marekani. Marekani imempa mke wangu, Jill, pamoja na mimi, nafasi yetu. Imempa Barack na mkewe, Michelle, nafasi yao ya kusimama hapa siku hii ya leo. Ni jambo la ajabu! Hizi thamani, nchi hii imetupa nafasi hii. Na sasa ni wakati kwa sisi sote, kama vile alivosema Abraham Lincoln, kuweka nyao zetu mahala ndipo na kusimama kidete. Ni wakati wa kumfanya Barack Obama kuwa rais. Ni wakati wetu, ni wakati wa Marekani. Mwenyezi Mungu aibarike Marekani na ayalinde majeshi yetu."

Akiwa ni kijana, mwenye umri wa miaka 47, tena akiwa na uzoefu wa miaka minne tu katika Baraza la Senate, bila ya uzoefu katika masuala ya uchumi na siasa za kigeni, Barack Obama alikuwa hana njia nyingine ila kutafuta mgombea mwenza atakayeziba mapengo hayo. Licha ya kuweko bungeni kwa miaka 36, Joe Biden aliwahi kujaribu mwenyewe kutaka kuwa mtetezi wa urais katika chaguzi za mwaka 1988, na pia mwaka huu wa 2008.Yeye. mwenye umri wa miaka 65, anaijuwa dunia kuliko mwanasiasa yeyote mwengine wa Kimarekani, ni hodari, tena mwenye ufasaha wa kuzungumza; hivi sasa akiwa mwenye kiti wa kamati ya masuala ya kigeni ya baraza la Senate. Joe Biden anaungwa mkono sana na tabaka la wafanya kazi, watu wanaomuona Obama kama ni msomi mno, na pia na wakatholiki ambao hawako karibu sana na Barack Obama.

Bila ya shaka, Chama cha Republican, ambacho mtetezi wake wa urais ni John McCain, kitamlaumu Obama kwamba yeye aliahidi kuibadilisha serekali ya Marekani na sura ya bunge la nchi hiyo, lakini sasa anamchagua mtu ambaye amekuwa seneta kwa miaka 36. Hata hivyo, Barack Obama anadai Biden ataweza kumsaidia katika kutekeleza ahadi zake za kuleta mabadiliko nchini Marekani:

"Kwa miongo Biden ameleta mabadiliko Marekani, lakini Marekani haijambadilisha."

Akimgeukia McCain, mwenyewe Joe Biden alisema hivi:

"Lazima nikwambieni wazi. Ninavunjika moyo sana kwamba rafiki yangu, John McCain, ambaye amesalimua amri kwa mrengo wa kulia wa chama chake na kukumbatia siasa za vita ambazo hapo kabla alikua akizilaani."

Wahakikia wa mambo wanasema pindi Barack Obama atashinda urais mwezi Novemba, watu watasema kwamba uamuzi wake wa kumteuwa Jose Biden kuwa ubavuni mwake ulikua mzuri, lakini ikiwa atashindwa, basi atajuta kwanini hajamteuwa Bibi Hilary Clinton kuwa mgombea wake mwenza.

Lakini inafaa tukumbuke kwamba katiba ya Marekani haimpi madaraka makubwa makamo wa rais, ila tu umuhimu wake ni pale rais anapokuwa hawezi kutimiza majukumu yake, labda kutokana na sababu za kiafya, au pale rais anapojiuzulu. Yeye hujaza nafasi hiyo kwa muda uliobakia wa urais. Mfano ni mwaka 1945 pale Harry S. Truman alichukua nafasi ya Rais Franklin D. Roosevelt aliyekufa. Mwaka 1963 Lyndon Johnson aliziba nafasi ilioachwa na Rais John F. Kennedy aliyeuliuwa, na tusimsahau Gerald Ford mwaka 1974 alipokikalia kiti cha urais kutokana na kujiuzulu kwa Richard Nixon katika kashfa ya Watergate.

Hapo zamani, makamo wa rais alikuwa hashiriki katika mikutano ya baraza la mawaziri, hivyo hata watu walifika hadi ya kukidharau cheo hicho. Lakini katika miaka ya karibuni, tunaona makamo wa rais wa sasa, Dick Cheney, ameibuka kuwa mwenye madaraka makubwa kuwahi kuonekana.

Mchanganyiko mzuri wa sura, tabia na siasa za mgombea wa urais na aliye mwenza ni muhimu katika mafanikio yao kwenye kampeni ya uchaguzi na pia wakiwa madarakani.

Watu wengi walifikiria Barack Obama angemteuwa Seneta Bibi Hilary Clinton kama mgomebea wake mwenza, na kwamba timu hiyo ya mchanganyiko wa mwanamume na mwanamke ingekuwa nanafasi nzuri zaidi ya kushinda. Kama madume wawili watupu watafanikiwa, nililitupa suala hilo kwa Alu Nyangoro, Mswahili anayesihi katika Mkoa wa Corolina ya Kaskazini,Marekani, aliyeniambia yuko mabarabarani akimfanyia kampeni Barack Obama:

Kwa maoni ya Mswahili huyo anayeishi Marekani ndio nakamilisha makala haya ya DARUBINI, uchambuzi wa kisiasa wa kila wiki kutoka Deutsche Welle, mjini Bonn, Ujerumani. Hadi mara nyingine ni Othman Miraji...





Mgombea mwenza anatakiwa ajalize mapungufu aliyekuwa nayo mgombea wa urais. Kama Joe Biden atafanikiwa kufanya hivyo kwa Barack Obama itajulikana mwezi Novemba, wakati wa uchaguzi.