Jeshi la Syria laanzisha msako Jisr al Shangour huku maelfu wakiandamana | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jeshi la Syria laanzisha msako Jisr al Shangour huku maelfu wakiandamana

Wanajeshi nchini Syria leo walianzisha msako uliohofiwa kwa muda mrefu katika mji wa Jisr al Shangour, huku maelfu ya waandamanaji wanaodai demokrasia wakijitosa katika barabara za miji kote nchini humo kwa maandamano.

default

Mwanajeshi wa Syria akishika doria

Televisheni ya taifa imesema vikosi vya jeshi vilianza operesheni yao katika mji wa Jisr al Shangur pamoja na vijiji jirani ili kuyakamata magenge ya watu waliojihami. Televisheni hiyo imeongeza kuwa uvamizi katika mji huo wa Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo ulitiokana na kilio cha wakaazi.

Wanaharakati wamesema kiasi ya wakaazi 50,000 wa Jisr al Shangur wamekimbia na wengi wao kuvuka hadi nchi jirani ya Uturuki, wakati ambapo vifaru na majeshi yalipoanza kukusanyika katikati ya wiki hii katika mji huo wa kaskazini magharibi na ambao tayari ulikuwa bila watu wengi.

Syrien Demonstration Assad Gegner

Vikosi vya ulinzi vikiwa mbele ya waandamanaji nchini Syria

Na habari za hivi punde zinaarifu kuwa wanajeshi wa Syria hii leo wamewapiga risasi watu wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa katika mkoa wa kusini Daraa. Wanaharakati wa haki za binadamu wamesema risasi kutoka magari ya kijeshi zilifyatuliwa katika eneo la al Harir, katika mkoa wa Bosra. Nayo televisheni ya kitaifa imesema watu waliojihami waliwafyatulia risasi wanajeshi katika eneo la Bosra al Harir, na kumuuwa mwanajeshi mmoja pamoja na raia.

Mwanaharakati mmoja kwa jina Hassan Berro amesema zaidi ya waandamanaji 8,000 waliandamana kaskazini mwa Syria, baada ya sala ya Ijumaa kupitia miji mitatu ya Kikurdi wakitaka mageuzi ya kisiasa na pia kama ishara ya kuonyesha mshikamano na mji uliozingirwa na jeshi wa Jisr al Shangour. Waandamanaji katika eneo la Ras al Ain lililo mpakani na Uturuki, waliimba na kusema…..“na damu yetu, na nafsi yetu, tunajitoa kafara kwa mji wa Jisr al Shangour“. Maandamano pia yamefanyika katika miji ya Qashmili na Amuda.

Hayo yanajiri huku Waziri wa ulinzi wa Marekani, Robert Gates, hii leo akiongeza shinikizo dhidi ya rais Bashar al Assad, akisema uhalali wa rais huyo sasa unatiliwa shaka. Gates alisema baada ya mkutano mjini Brussels kuwa mauaji ya kikatili ya Wasyria wasio na hatia yanapaswa kuwa tatizo la kuzua wasiwasi kwa kila mtu. Pia Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, ambaye ni rafiki wa karibu wa Assad, pia amemshtumu rais huyo kutokana na jinsi anavyoishughuli hali ya nchini mwake.

Flash-Galerie Syrien Assad Anhänger

Bango lenye picha ya rais wa Syria Bashar al Assad

Kundi la kutetea haki za binadam la Syrian Observatory lililoko mjini Nicosia, limesema maandamano mengine yalifanywa na milio ya risasi kusikika katika mji wa Horms, kaskazini mwa Damascus. Pia limedai wakaazi wamesema maafisa wa usalama waliyazuia makundi ya zaidi ya watu 7,000 waliokusanyika katika ukumbi wa Al Assi katika mji wa Hama, wa eneo la kaskazini, ambako kiasi ya raia 60 waliuwawa tarehe 3 Juni.

Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Kifaransa, AFP kuwa Mkuu wa usalama wa jeshi, Mohammed Mufleh, alikamatwa katika mji wa Hama hapo jana pamoja na wanajeshi wengine 20 na kuhamishwa hadi Damascus kutokana na amri za wizara ya mambo ya ndani.

Duru hiyo imesema Mufleh alitoa amri za mauaji ya kikatili yaliyofanywa wiki iliyopita katika mji wa Hama. Maandamano pia yaliripotiwa hii leo katika mji wa Dael, katika mkoa wa Daraa, ambao ndiko kulianzia maandamano ya kutaka utawala mpya nchini Syria katikati ya mwezi Machi, na maelfu ya watu walikusanyika katika mji mkuu wa wilaya hiyo, Midan, pamoja na viunga vya Harasta na Barzeh. Upinzani nchini humo uliitisha maandamano ya leo yaliyoitwa…“Ijumaa ya mshikamano wa makabila“.

Zaidi ya raia 1,100, wakiwemo watoto, wameuwawa katika misako ya serikali iliyofanya mnamo miezi mitatu iliyopita, kwa mujibu wa makundi ya haki za kibinadam.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Miraji Othman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com