Jeshi la Nigeria laimarisha ulinzi katika mji wa Jos. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 09.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Jeshi la Nigeria laimarisha ulinzi katika mji wa Jos.

Jeshi la Nigeria limepiga doria katika vijiji vilivyo karibu na mji wa Jos, kufuatia mapigano ya kikabila na ya kidini yaliyozuka mwishoni mwa wiki iliyopita na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Majeruhi katika mapigano ya kikabila na ya kidini yaliyotokea Jumapili iliyopita katika vijiji karibu na mji wa Jos nchini Nigeria akipatiwa matibabu.

Majeruhi katika mapigano ya kikabila na ya kidini yaliyotokea Jumapili iliyopita katika vijiji karibu na mji wa Jos nchini Nigeria akipatiwa matibabu.

Wakati nwito ukitolewa kuitaka Nigeria kuwachukulia hatua watu waliohusika na ghasia hizo, jeshi la ulinzi la nchi hiyo limeimarisha ulinzi katika maeneo yalikotokea machafuko hayo, na kwamba tayari limewakamata watu 93 wanaodaiwa kuhusika katika ghasia hizo.

Aidha, Kaimu Rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, amemfukuza kazi mshauri wake wa masuala ya usalama.

Nigeria Jonathan Goodluck

Kaimu Rais wa Nigeria Jonathan Goodluck.

Mamlaka za Nigeria lawamani: Watu walionusurika katika mapigano hayo ya kikabila na ya kidini, yaliyozuka mwishoni mwa wiki, ambayo wanawake na watoto walipigwa mpaka kufa ama kuchomwa wakiwa hai ndani ya nyumba zao, wamezishutumu polisi wa nchi hiyo kwa kushinda kuzuia ghasia hizo katika muda muafaka.

Baraza la Wazee wa Kikristo lenye kutoa ushauri katika jimbo la Plateau limedai kuwa ilichukua muda wa saa mbili kwa jeshi kuchukua hatua baada ya kupewa taarifa za mapigano hayo na kwamba muda walipofika katika tukio tayari wavamizi walikuwa wamemaliza kazi yao na kuondoka.

Wakizungumzia zaidi tukio hilo la Jumapili, wakaazi katika vijiji vya Dogo Nahawa, Zot na Ratsat, ambavyo vinakaliwa zaidi na Wakristo, wamesema washambuliaji walizingira maeneo hayo toka milimani mapema siku ya jumapili na kuanza kufanya mashambulio.

Nigeria Massaka März 2010

Wanawake wakilia kwa uchungu katika eneo la Dogo Nahwa, Nigeria, jana wakati wa mazishi ya pamoja ya watu waliouawa katika ghasia hizo.

Shambulio ladaiwa kuwa ni la kulipiza kisasi: Kwa upande wake, msemaji wa polisi katika jimbo hilo, Jos Mohamed Lerama, amelielezea tukio hilo kuwa ni la kulipiza kisasi, kufuatia lile lililotokea mwezi Januari mwaka 2010 katika mji wa Jos, ambako watu wa kabila la Fulani waliuawa.

Katika shambulio hilo lililotokea mwezi Januari zaidi ya watu 300 waliuawa, wengi wao wakiwa ni Waislamu.

Kamishna wa masuala ya habari katika jimbo la Plateau, Gregory Yenlong, amefahamisha kuwa watu 500 wameuawa, lakini kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi idadi ya watu waliouawa ni 55, huku miili bado ikiendelea kuhesabiwa.

Wakati huohuo, ndugu za watu waliouawa jana walihudhuria mazishi ya jamaa zao hao yaliyofanyika katika vijiji vitatu vilivyo karibu na mji wa kaskazini wa Jos, ambavyo wakazi wake ni Wakristo.

Watu wengine 200 waliojeruhiwa katika ghasia hizo bado wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Mashirika ya haki za binadamu yataka wahusika wakamatwe: Nalo Shirika la Haki za Binadamu la Human Right Watch limeitaka serikali ya Nigeria kufanya uchunguzi na kuwashtaki wale wote waliohusika katika mauaji hayo

Shirika hilo limesema kwamba kaimu rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, anapaswa pia kuwapa ulinzi wa kijeshi na polis wale wote wanaoishi katika maeneo ya mji huo wa Jos ulioko katikati mwa Nigeria.

Akizungumzia ghasia hizo zinazotokea nchini humo, mtafiti wa shirika hilo la haki za binadamu katika eneo la Afrika Magharibi Corinne Dufka amesema machafuko kama hayo ambayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu yametokea katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, lakini hakuna mtu aliyewajibishwa.

Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters, afp)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 09.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MNmT
 • Tarehe 09.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MNmT
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com