1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawarudisha makwao wanaharakati wa meli ya MV Rachel Corrie

Josephat Nyiro Charo7 Juni 2010

Viongozi wa Iran, Syria na Palestina wanakutana kesho jijini Istanbul kujadili masuala ya kiusalama katika ukanda huo kufuatia tukio la Israel kuwaua wanaharakati 9 Waturuki

https://p.dw.com/p/Njsb
Meli ya MV Rachel Corrie, iliyokamatwa na Israel wakati ikielekea GazaPicha: AP

Wanaharakati wote 19 waliokamatwa na wanajeshi wa Israel wakati walipokuwa njiani kupeleka misaada katika Ukanda wa Gaza wakiwa katika meli ya MV Rachel Corrie, wamerudishwa makwao. Raia 6 wa Malaysia na raia mmoja wa Cuba walirudishwa kwao hapo jana, kupitia kivuko cha daraja ya Allenby kwenda Jordan, huku wanaharakati wengine 6 Wafilipino na Muingereza mmoja wakiondoka usiku wa kuamkia leo.

Makomando wa Israel waliikmata meli hiyo siku ya Jumamosi wakati ilipojaribu kuingia Ukanda wa Gaza. Operesheni hiyo inaelezwa kufanyika kwa amani kabisa, ikilinganishwa na operesheni ya wiki iliyopita ambapo wanaharakati 9 Waturuki waliuwawa, wakati wanajeshi wa Israel walipoivamia meli ya misaada ya Uturuki iliyokuwa miongoni mwa msafara wa meli zilizokuwa zikipeleka misaada katika Ukanda wa Gaza.

Israel imekataa hatua ya kufanyika uchunguzi wa kimataifa katika hatua yake ya kuwavamia na kuwaua wanaharakati wa Kituruki waliokuwa njiani wakipleka misaada kwa ajili ya Wapalestina huko Gaza.

Viongozi wa Iran, Syria na Palestina wanakutana kesho jijini Istanbul kujadili masuala ya kiusalama katika ukanda huo kufuatia tukio la Israel kuwaua wanaharakati 9 Waturuki

Marais Mahmoud Ahmednejad wa Iran, Bashar Al Assad wa Syria, Hamid Karzai wa Afghanistan pamoja na kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas na Waziri mkuu wa Urusi, Vladmir Puttin, wametajwa kuhudhiria mkutano huo, ambapo Uturuki imeazimia kuutumia kushinikiza kulaaniwa kwa shambulio la Israel la wiki iliyopita na lilosababisha kuuawa Waturuki 9.

Taarifa zinaeleza kuwa kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas, ameshawasili Uturuki kwa ajili ya mkutano huo, akiwa njiani kuelekea Marekani kukutana na Rais Barack Obama. Ameelezwa kuwa na mazungumzo ya faragha na Rais wa Uturuki, Abdullah Gul, kabla ya rais huyo kuzungumza na marais Assad na Ahmednejad baadaye hii leo kujadili masuala kadhaa ya kiusalama.

Katika kile kinachoelezwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa ni kuangalia uwezekano wa kuibana zaidi Israel kufuatia shambulio la wiki iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje ya Afghanistan, Uturuki na Pakistan watakutana kwa faragha ili kumaliza mzozo baina ya majirani hao, ili kuweza kupambana na Waislamu wenye siasa kali katika ukanda huo.

Israel imealikwa katika mkutano huo, lakini imeelezwa kuwa balozi wake nchini Uturuki ndio pekee atakayeshiriki.

Wakati hayo yakijiri, majeshi ya Israel, yakiongozwa na helikopta, yamesema kuwa yamewaua makomandoo wanne wa Kipalestina katika mwambao wa Gaza, wakiwa wamevalia nguo maalumu za kuogelea wakiwa ndani ya boti, ambapo mmoja wa walionusurika katika shambulio hilo, Abu al- Walid, ameelezwa kuwa hawakuwa na silaha zozote ndani ya boti hilo kama mabvyo Israel imeeleza.

Akizungumza na shirika la Kifaransa la AFP, Walid amesema kuwa walikuwa katika mafunzo ya kuogelea na wengine saba, ambapo wanne kati yao waliuawa, wawili walinusurika na mmoja hajapatikana kufuatia shambulio hilo.

Israel imekuwa ikisisitiza kuwa inajihami dhidi ya kundi la Hamas, ambapo Waziri wa fedha, Juval Steinitz, amesema

Wakati hali katika ukanda huo ikiendelea kuwa tete, Iran imesema kuwa inapeleka meli tatu za misaada katika ukanda huo ikiwa ni jitihada mpya za kushinikiza kuondolewa kwa vizuizi katika ukanda huo,ambapo pia imesema kuwa itapeleka ndege iliyosheheni tani 30 za madawa nchini Misri zikiwa njiani kuelekea Gaza.

Uamuzi wa kupeleka misaada mingine huko Gaza umeelezwa kuwa moto na kuweza kuzusha machafuko mapya baada ya Iran kutangaza utayarifu wa kusindikiza meli zilizosheheni misaada ya kiutu kwa ajili ya Wapalestina zikiwa katika msafara.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/AFPE/APE

Mhariri. Miraji Othman