Iran yatangaza ujenzi wa kinu kipya | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran yatangaza ujenzi wa kinu kipya

Kinu hicho ni kwa ajili ya kurutubisha madini yake ya uranium

default

Eneo la urutubishaji wa madini ya uranium nchini Iran, ambako kuna kinu cha Natanz.

Iran imesema kuwa itaanza kujenga kinu kipya cha kurutubisha madini ya uranium, ikiwa ni sehemu ya kuupanua mpango wake wa kinyuklia, ambao umezusha hofu miongoni mwa mataifa ya Magharibi, yanayodai kuwa ni kwa ajili ya kutengeneza silaha za kinyuklia.

Novemba mwaka uliopita Iran ilitangaza mpango wake wa kupanua shughuli zake za kinyuklia kwa kujenga vinu vipya kumi na hivyo kupuuzia shinikizo la mataifa ya Magharibi la kuitaka nchi hiyo iachane na mpango wake huo. Mshauri wa ngazi ya juu wa Rais Mahmoud Ahmadinejad, Mojtaba Samareh-Hashemi ameliambia shirika la habari la ILNA, kuwa kiongozi huo wa Iran amethibitisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa kinu kipya na kwa amri yake kazi ya ujenzi itaanza.

Samareh-Hashemi amesema kuwa maeneo mapya ambako vinu hivyo vitajengwa mwaka huu, yameshapatikana na ujenzi utaanza hatua kwa hatua. Mwezi Februari mwaka huu, afisa wa ngazi ya juu wa mpango wa kinyuklia nchini Iran, Akbar Salehi aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Iran itaanza ujenzi wa vinu vipya viwili ifikapo Machi mwaka 2011.

Marekani inashinikiza Iran iwekewe vikwazo vya awamu ya nne na Umoja wa Mataifa katika wiki zijazo ili kuishinikiza nchi hiyo iachane na mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium, ambayo Iran kwa upande wake inasema ni kwa ajili ya matumizi salama. Iran imesema kuwa bado iko tayari kubadilisha madini yake ya uranium ya kiwango cha chini nje ya nchi, hatua ambayo inaweza kusaidia kuondoa hofu iliyopo kwa sasa juu ya shughuli za kinyuklia, ingawa mabadilishano hayo yanatakiwa yafanyike katika ardhi ya Iran.

Mataifa ya Magharibi yanaamini kuwa yameishawishi Iran, katika mazungumzo ya Geneva mwezi Oktoba, mwaka uliopita kuwasilisha sehemu ya akiba yake ya madini ya uranium nje ya nchi ili yakasafishwe zaidi, lakini mpango huo ukashindwa kutekelezeka muda mfupi baadae. Iran imetoa tangazo hilo siku moja baada ya kumalizika kwa mkutano wa kupunguza silaha za kinyuklia uliofanyika mjini Tehran. Katika mkutano huo uliopewa jina ''nishati ya nyuklia kwa wote, silaha za nyuklia sio kwa mtu yeyote'', Rais Ahmadinejad alitoa mwito wa kufanywa mageuzi ya Mkataba wa kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakati alipozikosoa Israel na mataifa ya Magharibi.

Aidha, kiongozi huyo wa Iran alilishutumu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Nishati ya Nyuklia-IAEA, kuwa limeshindwa kudhibiti usambazaji wa silaha za kinyuklia. Vile vile alipendekeza kuwa kundi la mataifa huru yasiyo na silaha za kinyuklia liundwe ili kufanywe marekebisho ya Mkataba wa kuzuia kuenea silaha za kinyuklia-NPT.

Katika hatua nyingine, gazeti la serikali la Jam-e-Jam limeripoti kuwa balozi wa Iran katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Nishati ya Nyuklia-IAEA, Ali Asghar Soltanieh hivi karibuni anatarajiwa kuachana na wadhifa huo kutokana muda wake kumalizika. Hata hivyo, Bwana Soltanieh hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AP)

Mhariri:Abdul-Rahman

 • Tarehe 19.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/N0Ul
 • Tarehe 19.04.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/N0Ul
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com