1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema itaanza kurutubisha madini ya Urani

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
7 Julai 2021

Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia duniani IAEA limesema mipango ya Iran ya kurutubisha madini ya Urani inakiuka mkataba iliotia saini 2015. Marekani yasema hatua hiyo inatia wasiwasi.

https://p.dw.com/p/3w9AN
Österreich Wien |  Atom-Konferenz
Picha: Askin Kiyagan/AA/picture alliance

Iran imeliambia shirika la Umoja wa Mataifa kwamba inakusudia kuongeza kurutubisha madini ya urani kwa asilimia 20 hatua ambayo Marekani imeiita kuwa ni uchokozi. Hatua hiyo itaifanya Iran izidi kukiuka mkataba wa nyuklia iliyoutia saini wakati wa utawala wa Rais Barack Obama mnamo mwaka 2015.

Soma Zaidi:Marekani, Iran zatofautiana katika kuyafufua makubaliano ya mpango wa nyuklia

Mkataba huo unapiga marufuku shughuli zote za urutubishaji kwa sababu hiyo ndiyo njia ya kuelekea kwenye kuunda silaha za nyuklia. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Ned Price amesema uamuzi wa Iran unaleta wasiwasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran  Mohammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad ZarifPicha: Getty Images/S. Gallup

Msemaji huyo ameeleza kuwa Iran inachukua hatua nyingine ya kusikitisha ya kurudi nyuma na hasa ikitiliwa maanani kwamba Marekani imethibitisha nia ya dhati ya kurejea kwenye mkataba na kutafuta njia za kudumu katika kuyatatua masuala ya nyuklia.

Price ameitaka Iran iachane na sera za maguvu na kurejea kwenye mazungumzo ya mjini Vienna yaliyokwama mwezi uliopita. Nchi za Ulaya nazo zimepaza sauti na kuitaka Iran iachane na nyendo za kurudi nyuma. Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimeungana na Marekani kwa kutoa tamko linaloelezea wasiwasi juu ya mipango ya Iran.

Makao Makuu ya Shirika la IAEA mjini Vienna, Austria
Makao Makuu ya Shirika la IAEA mjini Vienna, AustriaPicha: Michael Gruber/Getty Images

Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimesema hatua zinazochukuliwa na Iran zinayahatarisha mazungumzo yenye nia ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.

Nchi hizo pamoja na Marekani zilizotia saini mkataba huo, zimesema Iran haina ulazima wa kufanya utafiti huo. Hata hivyo Iran imejitetea kwa kueleza kwamba utafiti inaoufanya ni kwa ajili ya mahitaji ya tiba na pia kwa ajili ya kupata nyenzo za kufanyia utafiti kwenye kinu chake cha nyuklia.

Mkataba wa nyuklia na Iran ulienda kombo baada ya Marekani chini ya utawala wa Donald Trump kujiondoa mnamo mwaka 2018.

Vyanzo:DPA/AFP/ https://p.dw.com/p/3w7jE