1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

UN: Baraza la Usalama lajadili mkataba wa nyuklia ya Iran

Daniel Gakuba
1 Julai 2021

Wakati umoja wa mataifa na wadau wengine katika makubaliano hayo ya mwaka 2015 wakizitaka Marekani na Iran kujitolea ili makubaliano hayo yafanye kazi tena, nchi hizo mbili hazikuonyesha nia yoyote ya kuusogelea muafaka

https://p.dw.com/p/3vrtx
UN-Sicherheitsrat | Nahost-Sitzung
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Altaffer

Katika kikao hicho cha baraza la usalama ambacho kilijadili utekelezwaji wa azimio la baraza hilo lililoidhinisha makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, mkuu wa masuala ya kisiasa katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo ambaye alimuakilisha katibu mkuu, alirejelea wito kwa Marekani kuitaka nchi hiyo iiondolee vikwazo Iran, na kwa Iran kujizuia kuchukua hatua zozote ambazo zinakwenda kinyume na majukumu yake chini ya makubaliano hayo.

Soma zaidi: Guterres amtaka Biden kuiondolea vikwazo Iran

Miito yake hiyo inaungwa mkono na Umoja wa Ulaya na nchi nyingi wanachama wa baraza la Usalama, ambazo pia zinazitaka Marekani na Iran kuonyesha nia njema katika kuyapa tena uhai makubaliano hayo ambayo yalikaribia kusambaratika kabisa baada ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi yake mwaka 2018, na kurejesha vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa dhidi ya Iran na kuongeza vingine vipya na vikali zaidi.

New York UN Sicherheitsrat Rosemary A. DiCarloNon-proliferation Democratic PeopleÕs Republic of Korea
Mkuu wa masuala ya siasa katika Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarloPicha: UN

Marekani yaweka masharti ya kurejea kwake

Rais wa sasa Joe Biden amesema anataka kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo, lakini kwa masharti kuwa lazima Iran iache kwanza vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na makubaliano hayo, kama kuongeza urutubishaji wa madini ya urani, na kuyafanyia majaribio makombora yake yenye uwezo wa kutoka bara moja hadi jingine. Hayo yalikaririwa kwa mara nyingine na naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Jeffrey DeLaurentis katika kikao cha jana.

Soma zaidi: Iran yailaumu Marekani kwa kuingilia masuala yake ya ndani

Akijibu hoja hizo, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht Ravanchi, alisema mzigo wa kuonyesha utashi wa kuyanusuru makubaliano hayo uko kwenye mabega ya wale walioyavunja kwanza.

''Wale waliovunja ahadi zao ndio wanaowajibika kuthibitisha ukweli wao na mitazamo yao halisi kisiasa. Ndio wao wanaotakiwa kuchukua maamuzi magumu, na hivyo hawako katika nafasi ya kuzikosoa hatua za Iran ambazo zinaruhusiwa kikamilifu katika makubaliano hayo,'' amesema Ravanchi.

Iran Reaktor Natanz
Iran imekuwa ikizidisha urutubishaji wa madini ya urani kupita viwango vilivyokubaliwaPicha: picture-alliance/abaca/SalamPix

Je, juhudi za kimataifa zitafanikiwa?

Nchi sita zinazosalia katika makubaliano hayo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Urusi, China, Ujerumani na Iran zimekuwa zikikutana mjini Vienna katika juhudi za kuondoa tofauti kati ya Iran na Marekani ili makubaliano hayo maarufu kama JCPOA yaweze kufanya kazi tena.

Soma zaidi: Mtambo wa umeme wa nyuklia wa Bushehr nchini Iran wafungwa kwa sababu za kiufundi

Baada ya mkutano wao wa mwisho mnamo Juni 20, mratibu wake, Enrique Mora kutoka Umoja wa Ulaya alisema ingawa wanakaribia muafaka, bado hawajaufikia. Naye muakilishi wa Urusi Mikhail Ukyanov alisema umefika muda wa maamuzi ya kisiasa, kabla ya mkutano unaofuata ambao unadhaniwa kuwa wa mwisho.

 

ape, rtre