Iran yalaumiwa kwa uvunjaji wa haki za binaadamu | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.02.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran yalaumiwa kwa uvunjaji wa haki za binaadamu

Mwanasiasa wa Upinzani nchini Iran Ebrahim Yazdi amesema kuwa wanaharakati wanaopigia upatu mabadiliko nchini humo, wanakabiliwa na hali ngumu.

default

Mamia ya waandamanaji mjini Tehran wakiadhimisha mapinduzi ya Iran ya February 1979

Kiongozi huyo wa chama kilichopigwa marufuku cha Freedom Movement akizungumza nyumbani mjini Tehran amesema kuwa serikali ya Iran imekuwa ikiendelea kuwakandamiza kwa kuwatuhumu kuwa hawayaungi mkono mapinduzi ya nchi hiyo.

Yazdi ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje katika serikali ya kwanza ya nchi hiyo, baada ya mapinduzi ya kiislam, amesema kuwa polisi wamemzuia kuitisha mkutano wa watu kati ya 20 na 30 nyumbani kwake.


Iran imekuwa ikinyooshewa kidole na mashirika ya kimataifa ya haki za binaadamu pamoja na nchi za magharibi, kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.


Wakati kiongozi huyo wa chama kilichopigwa marufuku cha Freedom Movement, Ebrahim Yazdi akisema hayo,kwa upande wake mwanasheria wa haki za binaadamu nchini humo Bi Nasrim Sotoudeh anakiri kukabiliwa na ukandamizaji huo kutoka kwa serikali ambapo Decemba mwaka jana ilimzuia kutoka nchini humo kwenda Italia kupokea tuzo aliyotunukiwa kutokana na juhudi zake katika masuala hayo.


Pamoja na kuzuiwa huko mwanasheria huyo hivi sasa anakabiliwa na mashtaka mahakamani kutokana na kazi yake hiyo ya kutetea haki za binaadamu.


Matukio hayo mawili dhidi ya wanaharakati hao wa Iran huenda yanayakinisha kile ambacho mwanadiplomasia mmoja kutoka nchi za Magharibi amekiita kuzifunga mdomo sauti ambazo hazikubaliani na sera za utawala wa Iran, kitu ambacho amesema kinaweza kuwa ni kutokuwa na uhakika katika uchaguzi mkuu wa mwezi June mwaka huu, uhakika wa uchumi pamoja na sera za utawala mpya wa Rais Barack Obama wa Marekani.


Rais Mahmoud Ahmadinejad anapanga kuwania kipindi cha pili cha miaka minne katika uchaguzi huo, pamoja na kuwepo kwa tuhuma nyingi dhidi ya uongozi wake kwa kushindwa kusimamia vyema uchumi halikadhalika kujenga mahusiano mabaya kimataifa hususani nchi za magharibi.


Rais huyo wa Iran ameweka masharti magumu ya kuweza kuwa na mazungumzo na serikali ya Rais Obama akiitaka kwanza ibadilishe sera zake dhidi ya Iran na pia kuiomba radhi kwa uhalifu ambao Marekani imeifanyia Iran kipindi kilichopita.


Wachambuzi wa siasa za Iran wanasema kuwa huenda serikali hiyo ya Iran ikachukua msimamo mkali dhidi ya wanaharakati wanaotaka mabadiliko ya kisiasa na kijamii, ikihofu ya kwamba mtizamo huo wa wanaharakati utapata uungwaji mkono mkubwa mnamo wakati huu ambapo nchi hiyo iko katika mbinyo wa kimataifa dhidi ya mpango wake wa nuklia.


Kuporomoka kwa bei ya petroli nako kunaweza kuifanya nchi hiyo inayoshika nafasi ya nne katika utoaji mafuta duniani,kuzidi kutotilia maanani vikwazo ilivyowekewa na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa dhidi ya mpango wake huo wa nuklia.


Kwa hakika wafuatiliaji hao wa siasa za Iran wanasema kuwa kile kinachoitwa uhuru wa mawazo na fikra hakuna nchini Iran wakitolea mfano hapo mwaka jana ambapo ofisi ya mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Shirin Ebadi ilifungwa kwa madai ya kwamba hana kibali ya kuendesha ofisi hiyo.


Naye Sussan Tahmasebi ambaye ni mwanaharakati wa kina mama amesema kuwa hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaharakati hao maarufu zinapeleka ujumbe pia kwa wanaharakati wengine kuwa tayari kukabiliwa na hatua hizo.


Serikali ya Teheran ilitupilia mbali shutuma na madai ya nchi za magharibi ya kwamba imekuwa ikivunja haki za binaadamu, na kusema kuwa inaruhusu uhuru wa kusema.


Msemaji wa serikali ya Iran Gholamhossein Elham wiki iliyopita alinukuliwa akisema ya kwamba wananchi wa Iran wameonja uhuru kamili baada ya kuingia madarakani kwa Rais Ahmednejad mwaka 2005 ambapo aliahidi kufufua thamani ya mapinduzi ya kiislam ya mwaka 1979 yaliyomuondoa madarakani kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani Shah.


Lakini shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch lenye makao yake makuu nchini Marekani limesema kuwa serikali hiyo ya Iran imekuwa ikitumia vibaya sheria ya usalama wa taifa kama uhalali wa kuwanyamazisha wanaharakati na kwamba kumekuwa na idadi kubwa ya wanaharakati wa kisiasa, wanazuoni na wengineo waliyokamatwa.


Iran mara kadhaa imekuwa ikizilaumu nchi za Magharibi kwa kutaka kuihujumu nchi hiyo ya kiislam kwa msaada wa wasomi na watu wengine waliyoko ndani ya nchi hiyo.


Mwezi uliyopita rubaa za mahakama zilisema ya kwamba watu wanne raia wa Iran wamekamatwa wakishukukiwa kutaka kuiangusha serikali ya nchi hiyo kwa msaada wa Marekani, tangazo ambalo wachambuzi wa siasa za nchi hiyo wanasema kuwa ni onyo kwa Marekani kutoingilia masuala ya Iran.

 • Tarehe 02.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Glq5
 • Tarehe 02.02.2009
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Glq5
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com