Iran yaendelea kukosolewa na nchi za Magharibi
20 Januari 2026
Wairan wameendelea kushuhudia kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kwa takriban wiki mbili, hali ambayo sio tu inawazuiwa kupata taarifa kutoka nje, lakini pia inawasababishia adha kubwa kibiashara, hasa kwa wanaotegemea kuendesha shughuli zao kupitia mtandao.
Takriban wiki mbili za kuzimwa kwa mtandao wa intaneti, ndio kipindi kirefu zaidi Iran imewahi kushuhudia mawasiliano hayo yakizimwa katika historia yake.
Tangu yalipozuka maandamano makubwa ya wananchi Januari 8 ya kupinga hali ngumu ya kiuchumi na kuzimwa kwa nguvu kubwa na vikosi vya usalama, wananchi wamekuwa wakiishi katika kiza fulani cha mawasiliano ya mtandao.
Hadi sasa ni tovuti kadhaa za ndani ndizo zinazoweza kufunguka huku mtandao wa intaneti ukipatikana kwa shida sana kupata taarifa za ulimwengu wa nje.
Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Abbas Aragchi amelikosoa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia lililofunguliwa hivi leo huko Davos kwa kufuta mwaliko wake wa kuzungumza mbele ya mkutano huo wa kimataifa, akilalamika, hatua hiyo imechukuliwa kwa misingi ya kusikiliza taarifa za uwongo na shinikizo la kisiasa kutoka Israel na Marekani.
Waandaaji wa jukwaa hilo wamesema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na vifo vilivyoshuhudiwa nchini Iran kufuatia kuzimwa kwa maandamano ya hivi karibuni nchini humo.
Araghchi ameiita hatua hiyo ni undumilakuwili unaofanyika waziwazi kwa kuialika Israel baada ya kuendesha vita vikubwa katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano ya Iran yaliyosababishwa na hali ngumu ya kiuchumi mwishoni mwa mwezi Desemba yamegeuka kuwa changamoto kubwa kwa utawala wa Tehran unaoendelea kukosolewa huku ripoti zikionesha zaidi ya watu 4000 wanakhofiwa kuuwawa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel ameutolea mwito Umoja wa Ulaya kuliorodhesha jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran kama kundi la kigaidi.
"Nyuma ya hatua ya kuzimwa mtandao wa intaneti, ukandamizaji unaendelea nchini Iran. Utawala wa Ayatollah unawauwa kikatili watu wake wenyewe wakati wakipambania uhuru wao. Jeshi la Kimapinduzi limetanuwa ugaidi na ukosefu wa uthabiti katika eneo zima la Mashariki ya Kati na nje ya eneo hilo kwa miongo kadhaa.''
Ripoti za hivi punde zinasema tume ya masuala ya usalama wa taifa, bungeni ya Iran imetangaza kwamba ikiwa kutafanyika shambulio lolote dhidi ya kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei fatwa ya Jihad au vita vitakatifu itatangazwa, Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka kufuatia maandamano kote nchini Iran.Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amshutumu Trump kwa kuchochea maandamano Iran
Urusi ambayo ni muitifaki wa Iran imesema haioni sababu ya kuacha kufanya biashara na Jamhuri hiyo ya Kiislamu huku waziri wake wa mambo ya nje Sergei Lavrov akisisitiza nchi hiyo itaendelea kufanya hivyo pale inapohisi ni sahihi, licha ya Marekani kutishia vikwazo.
Januari 12 Rais wa Marekani, Donald Trump alisema nchi yoyote itakayothubutu kufanya biashara na Iran itakabiliwa na ushuru wa asilimia 25 katika bishara yoyote inayofanya na Marekani.
Wanaharakati: Waliouawa katika ghasia za Iran ni zaidi ya 3,000Wakati hali jumla ndani ya Iran ikiwa bado ni ya khofu, baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa limepanga kikao maalum cha dharura siku ya Ijumaa kuhusu hali ya kuzorota kwa haki za binadamu inayoripotiwa katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu. Mkutano huo ukiwa umeitishwa kwa niaba ya Uingereza, Ujerumani, Iceland, Moldova na Macedonia Kaskzini.