Hotuba ya Obama kwa Ulimwengu wa Kiislamu | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.06.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hotuba ya Obama kwa Ulimwengu wa Kiislamu

Maneno wazi ya Obama kwa Ulimwengu wa Kiislamu

Rais Barack Obama wa Marekani akitoa hotuba yake kwa Ulimwengu wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Kairo, Misri.

Rais Barack Obama wa Marekani akitoa hotuba yake kwa Ulimwengu wa Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Kairo, Misri.

Jana katika chuo Kikuu cha Kairo, rais wa Marekani, Barack Obama, alitoa hotuba ya kimsingi kwa Ulimwengu wa Kiislamu. Ametaka kuweko mwanzo mpya katika uhusiano baina ya pande hizo mbili.

Sio tu Rais Barack Obama, kwa msisitizo muhimu, amezigusia hisia za watu waliomsikiliza. Yaliokuwemo ndani ya hotuba yake yalikuwa wazi kabisa, nayo ni kunyosha mkono wa kuwa na ushirika pamoja na mdahalo na Ulimwengu wa Kiislamu. Obama alizungumzia juu ya thamani na dhamana za pamoja baina ya Marekani na Ulimwengu wa Kiislamu. Alitumia maneno yalio wazi kutambuwa mchango wa Waislamu duniani kote, ikiwemo Marekani yenyewe; hivyo kufuata njia ilio kinyume kabisa na ile ya mtangulizi wake, George W. Bush.

Machoni, rais huyo anatafuta kikweli kuwa na mwanzo mpya, na hatafuti msaada tu wa Aya za Koran na maneno mazuri juu ya Uislamu. Risala yake ni rahisi kuifahamu. Obama amekutana kwa heshima na Waislamu bilioni moja na nusu walio duniani. Yuko kweli tayari kuyazungumzia masuala na mitazamo yao, na alilitupia jicho la uhakiki nchi yake mwenyewe. Lakini alisema pia kile ambacho mwenyewe angetaka kukisema na kile ambacho washirika wake wa mdahalo walitarajia kukisikia kutoka kwa rais wa Kimarekani.

Aliitaka Israel ilitambuwe lile lengo la la kuundwa dola ya Kipalastina na kuachana na ujenzi wa makaazi ya kiyahudi katika ardhi za Wapalastina. Na alielezea hayo kwa uwazi, jambo ambalo lisingefikiriwa kufanyika chini ya Rais Bush. Lakini pia Obama aliweka wazi kinaga ubaga nini yeye anachokitarajia kutoka kwa Wapalastina, na hasa kabisa kutoka Chama cha Hamas. Nacho ni kutambuliwa wazi wazi kuweko dola ya Israel na kuachana na majaribio yote ya kutaka kuutanzuwa mzozo huo kwa njia ya matumizi ya nguvu. Pia hajawacha wasiwasi wowote kwamba uhusiano wa Marekani na Israel, licha ya malalamiko yote ya Marekani dhidi ya Israel, unabakia katika ngazi maalum. Na japokuwa yeye anauona mpango wa amani wa nchi za Kiarabu kuwa ni msingi mzuri wa kufanyia mashauriano, lakini hawezi kwa lazima tangu sasa kutaja matokeo ya mashauriano hayo ya baadae. Vikwazo hiyo alivovitaja havijawafurahisha watu wengi walioisikiliza hotuba yake hiyo. Lakini huo ndio ukweli. Na ukweli mwingi kama huo kutoka kwa Rais wa Kimarekani haujawahi kuonekana kwa muda mrefu.

Lakini watu walitarajia maneno yalio wazi zaidi kutoka kwa Barack Obama kuhusu hali ilivyo juu ya haki za binadamu katika nchi nyingi za Kiislamu, na zaidi juu ya maslahi ya kijeshi na ya kiuchumi ya Marekani katika nchi za Kikislamu, na vipi unavoweza kuletwa ushirikiano na tawala za nguvu uambatane na fikra za uhuru za Marekani. Lakini katika masuala mengi mengine, ilifurahisha kwamba rais huyo wa Marekani aliweka wazi. Kwa ufupi, risala ni kwamba demokrasia sio bidhaa inayoweza kusafirishwa na Marekani kupelekewa nchi nyingine, lakini demokrasia ni haki ya kimsingi ya wanadamu wote. na kwamba Marekani iko tayari, kutokana na makosa ya zamani, kujifunza kutokana na makosa hayo; lakini pia katika siku za mbele haitastahamilia ugaidi, lakini itatafuta njia ya kukabiliana na jambo hilo kwa pamoja.

Hayo ni maneno yanayojenga daraja. Nini ambacho kinabidi kifuate sasa, ni vitendo, sio tu kutoka upande wa Wamarekani.

 • Tarehe 05.06.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I44g
 • Tarehe 05.06.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/I44g
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com