1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hizbullah yakabiliana kijeshi na Israel

Mohammed Khelef
28 Februari 2024

Hizbullah imekabiliana kijeshi na Israel huku Qatar ikirejelea mwangwi wa kauli ya Marekani kwamba huenda makubaliano ya usitishaji mapigano ya Ukanda Gaza yakafikiwa hivi karibuni kati ya kundi la Hamas na Israel.

https://p.dw.com/p/4cwaz
Kiongozi wa Hizbullah nchini Lebanon, Hassan Nasrallah.
Kiongozi wa Hizbullah nchini Lebanon, Hassan Nasrallah.Picha: Mohamed Azakir/REUTERS

Makabilliano hayo ya siku ya Jumanne (Februari 27) kati ya Israel na Hizbullah yalitokana na mashambulizi ya anga ya Israel yaliyouwa watu wawili katika mji wa mashariki mwa Lebanon, Baalbek, siku ya Jumatatu (Februari 26), ambayo Israel ilidai kuwa yalikuwa ni kulipiza kisasi cha kuangushwa kwa droni yake.

Tangu hapo, Hizbullah ilikuwa imesema kwamba mauaji hayo ya Israel yasingelipita bila kujibiwa.

Hizbullah ilisema ilikishambulia kituo cha jeshi la anga cha Israel kwenye eneo la Meron kwa kutumia kiwango kikubwa cha makombora yaliyorushwa kutokea maeneo mbalimbali. 

Soma zaidi: Biden asema ana matumaini makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yatafikiwa wiki ijayo

Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Israel, Avichay Adraee, alisema makombora hayo ya Hizbullah hayakusababisha madhara wala maafa yoyote kweye kituo hicho cha anga.

Matokeo ya mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Lebanon.
Matokeo ya mashambulizi ya anga ya Israel mashariki mwa Lebanon.Picha: Ali Hashisho/Xinhua/picture alliance

Badala yake, Adraee alidai kuwa ndege za kivita za Israel ziliishambulia na kuiharibu vibaya miundombinu ya Hizbullah katika kujibu mashambulizi hayo.

Kundi la Hizbullah, ambalo ni mshirika mkubwa wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, limekuwa likikabiliana mara kwa mara - lakini katika kiwango cha chini - na wanajeshi wa Israel, tangu ulipotokea uvamizi wa Hamas tarehe 7 Oktoba. 

Qatar yatarajia makubaliano kufikiwa karibuni

Kwenye upande wa juhudi za kidiplomasia, Qatar, ambayo ni miongoni mwa wapatanishi wakuu wa mgogoro huo wa Mashariki ya Kati, ilisema ilikuwa ina "matumaini makubwa ya kupatikana kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya mwezi mtukufu wa Ramadhani". 

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar, Majid Al-Ansari, aliwaambia waandishi wa habari mjini Doha kwamba ingawa hakuweza kutaja tarehe maalum, lakini matarajio ni kwamba kungelikuwa na usitishwaji wa mapigano kabla ya mfungo wa mwezi huo mtukufu kwa Waislamu kuanza tarehe 11 Machi.

Majed Al-Ansari mjini Doha
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar, Majid al-Ansari, akizungumza na waandishi wa habari mjini Doha.Picha: Imad Creidi/REUTERS

Soma zaidi: Israel kushinikiza usitishwaji vita Gaza kupitia Qatar

Hata hivyo, msemaji huyo alikiri kwamba bado hali ilikuwa tete na kwamba hadi hapo hakukuwa na upande hata mmoja uliokuwa umekubali moja kwa moja kuweka silaha chini.

Kauli ya Ansari ilitanguliwa na ile ya mshirika mkuu wa Israel, Rais Joe Biden wa Marekani, ambaye alikuwa amewaambia waandishi wa habari siku ya Jumatatu kwamba kufikia Jumatatu (Machi 4) kungelikuwa tayari na makubaliano ya usitishwaji wa mapigano kwenye Ukanda wa Gaza.

Wapatanishi wa Misri, Qatar na Marekani walikutana mjini Doha siku za Jumapili na Jumatatu kwenye mazungumzo yaliyohudhuriwa pia na wawakilishi wa Israel na Hamas. 

Mazungumzo ya Doha yalitanguliwa na yale ya Paris ambayo hayakuwashirikisha Hamas, lakini ambayo msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jake Sullivan, alisema yalitowa taswira ya jinsi usitishwaji mapigano wa muda na uachiliwaji wa mateka utakavyokuwa.

Hata hivyo, Hamas imesisitiza kuwa hakikisho pekee la kuachiliwa mateka ni usitishwaji wa kudumu wa mapigano.

Vyanzo: AP, Reuters