1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Uingereza lamtaka Murdoch kutoinunua BSkyB

13 Julai 2011

Bunge la Uingereza linatarajiwa kupitisha hoja binafasi ya chama kikuu cha upinzani Labour kumtaka Rupert Murdoch kujitoa kwenye zabuni ya ununuzi wa kituo cha utangazaji cha BskyB.

https://p.dw.com/p/11u1o
Wabunge wa baraza la wawakilishi nchini Uingereza "House of Commons", wakijadili mada .Picha: AP

Bunge la Uingereza linatarajiwa kupitisha hoja binafsi ya chama kikuu cha upinzani cha Labor ambayo inamtaka mmiliki wa kampuni kubwa ya vyombo ya habari ya News Corp, Rupert Murdoch, kujitoa kwenye zabuni ya ununuzi wa kituo kikubwa cha utangazaji cha BSkyB, kwa sababu ya magazeti ya Murdoch kuhusika na kashfa ya kutega simu binafsi za watu.

►Licha ya kwamba hoja hii haina nguvu za kisheria, lakini kupitishwa kwake Bungeni kutakuwa na maana kubwa dhidi ya jitihada za Murdoch kutanua himaya yake ya vyombo vya habari, ambayo tayari imengia doa.

Tayari serikali ya mseto nchini humo, imeshasema kwamba itaiunga mkono hoja hiyo, jambo litakalomaanisha kuyumba kwa uhusiano wa kiasili, kati ya Murdoch na serikali zinazoshika madaraka nchini Uingereza.

Waziri Mkuu, David Cameron, amekiri kwamba kwa hali ilipofikia, si rahisi tena kuijenga taswira ya kampuni ya News Corp, ambayo ilikuwa ikichapisha gazeti lenye mauzo makubwa kabisa duniani, la News of the World:

Großbritannien Abhörskandal Pressekonferenz Premierminister David Cameron in London
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, amekiri kuwa taswira ya kampuni ya News Corporation haiwezi tena kuwa safi.Picha: dapd

"Unapoangalia kwa upana hili tunalosikia hivi leo kuhusiana na walinzi wa kasri ya malkia ambao waliweza kutoa taarifa za watu wanaowafanyia kazi, kuhusu waziri mkuu wa zamani ambaye taarifa zake za benki zilitegwa. Mambo haya tunayoyasikia leo kwa hakika yanaogofya sana."

Waziri Mkuu wa zamani anayemzungumzia Cameron ni mtangulizi wake, Gordon Brown, ambaye ametajwa kuwa miongoni mwa wahanga wa News Corp. Simu za Brown, akaunti za benki na taarifa za kitabibu za familia yake, ziliwahi kutegwa na kunaswa. Mwenyewe ameishutumu News Corp kwa kufanya kazi ya kihalifu.

Mwanzoni, hatua ya Cameron kumgeuka Murdoch, ilikusudiwa kupunguza tu madhara ya mgogoro huu kwa heshima yake binafsi, lakini sasa imepunguza uwezekano wa bepari huyo mkubwa wa vyombo vya habari, kuchukua asilimia 61 za hisa za BSkyB, ambazo hazimiliki.

Gazeti la The Independent limewanukuu baadhi ya mawaziri wakisema kwamba, uchukuwaji wa BSkyB utakuwa "umekufa kisiasa" baada ya kura ya leo bungeni.

Chanzo ndani ya serikali ya Cameron kimeeleza kwamba, njia pekee kwa News Corp kuichukua BSkyB, ni kuyauza magazeti yake yote matatu inayoyamiliki nchini Uingereza, ambayo ni The Sun, The Times na The Sunday Times.

Kiongozi cha chama cha Labor, ambacho ndicho kinachopeleka hoja binafsi bungeni, Ed Miliband, amesema suluhu pekee kwa Murdoch ni kusahau kabisa biashara ya BSkyB:

Ed Miliband
Ed Miliband, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Labour .Picha: AP

"Kitu cha mwanzo ninachotaka kumwambia Bwana Murdoch ni, jitowe kwenye zabuni ya BSkyB. Hicho ndicho kitu muhimu ambacho anatakiwa kukifanya. Anapaswa kujua kuwa ukungu wa shutuma uliolitanda gazeti na News International unafanya isiwezekane kabisa kwa zabuni hii kuendelea."

Na katika hatua nyengine, mkasa huu sasa unatishia kuingia Marekani, ambako Murdoch anamiliki gazeti na New York Post, jarida la Wall Street na kituo cha utangazaji cha Fox.

Mwenyeketi wa kamati ya biashara, sayansi na usafiri ya baraza la Senate, John Rockefeller, ameitisha uchunguzi kubaini ikiwa News Corp imewahi kuvunja sheria yoyote ya Marekani.

Seneta Rockeffeler amesema anatilia wasiwasi unasaji wa simu za watu wa News Corp, unaweza kuwahusisha pia wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 na Wamarekani wengine, jambo ambalo amesema litakuwa na matokeo mabaya kwa kampuni hiyo.◄

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo