Bunduki zapanda bei maradufu ukingo wa magharibi. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bunduki zapanda bei maradufu ukingo wa magharibi.

Sababu kubwa ni kuongezeka kwa mahitaji , huku wakaazi wakiwa na hofu baada ya kundi la Hamas kutwaa mamlaka ya eneo la Gaza .

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

Miaka miwili iliopita, bunduki aina ya M16 ilikua ikipatikana katika eneo la wapalestina la ukingo wa magharibi kwa bei ya dola 5,400 au za Kimarekani. Lakini leo wanunuzi huko Hebron katika soko la siri au magendo hutakiwa kulipa hata mara mbili zaidi ya bei hiyo wauzaji wanasema bei imepanda kutokana na hatua kali za usalama zinazochukuliwa na chama cha Hamas kinacholidhibiti eneo la Gaza, tangu kilipowashinda wapinzani wake wa kundi la Fatah katika kinyanganyiro cha kuwania madaraka mwezi Juni.

Miezi minne baada ya chama hicho cha kiislamu cha Hamas kinachotajwa na Marekani na nchi nyengine za magharibi kuwa cha msimamo mkali, kukishinda kile cha Fatah cha Rais Mahmoud Abbas katika mapigano ya kuwania madaraka huko Gaza, kuna wasi wasi kwamba uhasama unaweza pia kuzuka katika ukingo wa Magharibi, kabla ya mkutano wa amani utakaodhaminiwa na Marekani mwezi ujao. Hofu hiyo imesababisha mfumko wa bei za bunduki na pia ongezeko la wanunuzi.

Wafanya biashara katika soko la silaha hizo mjini Hebron , mji wenye wakaazi wengi katika ukingo wa magharibi wanasema mauzo ya silaha yameongezeka kwa 70 asili mia tangu Hamas kiudhibiti ukanda wa Gaza, wakati hatua kali za kuimarisha usalama zimesababisha bei kupanda.

Katika sehemu ya kaskazini mwa mji wa ukingo wa magharibi wa Jenin, kiala risasi moja ya bunduki ya AK 47 ni kiasi ya Shekels 35 za Israel sawa na zaidi ya dola 8 za kimarekani. Katika eneo la Gaza linalodhibitiwa na Hamas risasi moja ya bunduki hiyo ni kati ya dola moja na dola moja na nusu ya Kimarekani. Lakini wakaazi wa ukingo wa magharibi wanasema wanajihisi hawana tena usalama na hofu hiyo inawafanya baadhi kununua silaha kwa lengo la kujilinda wao na familia zao.

Rais Mahmoud Abbas kutoka kundi la Fatah aliifukuza kazi serikali ilioongozwa na Hamas na kuiteuwa ile inayoungwa mkono na Fatah mwezi Juni baada ya chama cha Hamas kuchukua madaraka ya kulidhibiti eneo la Gaza.Mvutano na hali ya wasi wasi kati ya pande hizo mbili umeongezeka mno mnamo majuma ya karibuni na baadhi ya wakaazi wa ukingo wa magharibi, wana wasi wasi mzozo huo unawerza ukazagaa .

Wakati mapigano sawa na yaliotokea Gaza si jambo ambalo linaatarajiwa sana kutokea ukingo wa magharibi kutokana na kuweko kijeshi kwa Israel katika sehemu hiyo na upinzani mkubwa dhidi ya Hamas, majeshi ya usalama ya Fatah yanachukua hatua kukabiliana na uasi wa aina yoyote.

Vyombo vya usalama vimewatia nguvuni na kuwaweka ndani mamia ya wafuasi wa Hamas, vimejaribu kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya Hamas katika ukingo wa magharibi na kuziandama jumuiya za misaada ambazo zinasemekana

Ingawa msemaji wa Hamas Fawzi Barhoum ameakanusha kwamba wanaimarisha wafuasi wao katika ukingo wa magharibi, lakini baadhi ya viongozi wa chama hicho wamesema chama chao kinaweza kuzusha uasi ikiwa Rais Abbas ataendelea kuwakandamiza wafuasi wa chama hicho.

Baadhi ya wadadisi wanasema kushindwa kwa kiongozi huyo kupiga hatua ya maendeleo katika suala la kuwa na taifa la Palestina katika mkutano wa kilele utakaodhaminiwa na Marekani mwezi ujao, kunaweza kukipa nguvu zaidi Hamas na kuzusha hali ya wasi wasi katika ukingo wa magharibi.Wanasema Hamas inaweza kuitumia nafasi hiyo na kujitoa kama ndiyo uongozi unaofaa kwa kikihoji Abbas ni dhaifu kuweza kufanikisha lengo la kuwa na dola ya Palestina.

Tangu Hamas kilidhibiti kwa nguvu eneo la Gaza, mataifa ya magharibi yamekua yakitoa fedha kwa ukingo wa magharibi katika jaribio la kumpa msukumo Abbas na kukitenga zaidi Hamas huko Gaza na tayari yanawapa mafunzo polisi na wanajeshi walio watiifu kwa serikali inayoungwa mkono na kundi la Fatah.

Maoni ya wapalestina yamegawika, kuhusiana na suala la iwapo Abbas anaweza kweli kudumisha amani bila ya kufikia maridhiano na Hamas.Zingatio hilo ni miongoni mwa hofu zinazowafanya wakaazi wengi kununua silaha kwa lengo la kujilinda, na hilo kusababisha bei za bunduki kupanda mno, huku mahitaji yakiongezeka.

 • Tarehe 17.10.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hM
 • Tarehe 17.10.2007
 • Mwandishi Mohammed AbdulRahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7hM

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com