1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brussels: Marekani na Umoja wa Ulaya kuchangiana taarifa za safari za ndege.

30 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBnE

Mawaziri wa mambo ya ndani wa Ulaya wameidhinisha mpango mpya kati ya mataifa yao na Marekani wa kutoa taarifa za abiria wa ndege wanaosafiri baina ya Ulaya na Marekani.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble na mawaziri wenzake wa Umoja wa Ulaya walikubaliana mpango huo jana.

Waziri Wolfgang Schäubel alisema shirika la upelelezi la Marekani,FBI, litaruhusiwa kuchunguza mambo kumi na tisa kuwahusu abiria, kama vile majina, nambari za simu na anwani.

Idadi hiyo imepunguzwa kutoka idadi ya maswala thelathini na manne.

Hata hivyo Marekani imeongezewa muda wa kuhifadhi taarifa hizo hadi miaka kumi na mitano badala ya muda wa sasa wa miaka mitatu unusu.

Waziri huyo wa mambo ya ndani wa ujerumani ametoa wito wa kuandaliwa mfumo wa kuhifadhi taarifa za abiria barani Ulaya.

Waziri Wolfgang Schäuble amesema ni muhimu sana kuwa na mfumo kama huo hasa wakati huu ambapo tishio la ugaidi limeongezeka.