Baraza la mawaziri Nigeria lavunjwa. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Baraza la mawaziri Nigeria lavunjwa.

Hatua ya Kaimu Rais nchini Nigeria Goodluck Jonathan kulivunja baraza la mawaziri, imeelezwa pia ni kuonesha zaidi nguvu aliyonayo kwenye mamlaka nchini humo, huku wachambuzi wakisema itamuwezesha kuchagua timu yake.

default

Kaimu Rais wa Nigeria Jonathan Goodluck.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri wa Habari wa Nigeria Dora Akunyili, ametangaza kuwa makatibu wakuu wa wizara watashikilia nafasi hizo mpaka pale baraza jipya litakapotangazwa.

Hata hivyo hakufafanua kuhusiana na uamuzi huo, wa Makamu wa Rais kulivunja bunge.

Hatua hiyo inayshiria kuwa Bwana Jonathan anauhakika kwamba Rais wa nchi hiyo Umaru Yar'Adua hataweza kurejea tena madarakani kutokana na kuwa mgonjwa na pia tangu Novemba mwaka jana hakuweza kuonekana hadharani, wakati alipopelekwa nchini Saud Arabia kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo na figo.

Rais Yar'Adua aliondoka nchini humo bila ya kuchukua hatua kwa mujibu wa katiba za kukabidhi madaraka kwa muda, na kuacha utata mkubwa.

Goodluck Jonathan mwenye umri wa miaka 52, ambaye alikuwa Makamu wa Rais wa Nigeria aliteuliwa kushika wadhfa huyo wa ukaimu Rais Februari 9 na bunge la nchi hiyo kutokana na kutokuwepo kwa Rais Umaru Yar'Adua madarakani kwa muda mrefu na hata baada ya kurejea nyumbani katika makaazi yake ya Rais hivi karibuni bado mpaka sasa hajasikika wala kuonekana hadharani.

Nao wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hatua hiyo ya kuvunjwa kwa bunge itamruhusu Bwana Jonathan kuchagua watu anaowataka kuliko kutegemea washirika wa Rais Yar'Adua na pia kumuwezesha kuwa na nguvu zaidi za madaraka.

Baraza hilo la mawaziri lilikuwa likionekana kugawanyika kati ya wale waliokuwa wakimuunga mkono Rais Yar'Adua na wanaomuunga mkono Jonathan . Mgawanyiko huo umezidi tangu pale tume ya uchaguzi ilipotangaza wiki iliopita kuwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo utafanyika Aprili mwaka ujao.

Wachambuzi wanasema kwa hatua hiyo Bwana Jonathan anataka kuimarisha nafasi yake hiyo katika madaraka. Lakini uimara wake utategemea ni nani watakuwemo katika baraza jipya la mawaziri, kukiwa na hatari ya kwamba wale watakaowekwa kando wanaweza kujaribu kuipinga hatua yake kwa kudai kikatiba hana mamlaka ya kuchukua uamuzi huo au kuwaondoa katika nyadhifa zao.

Hatua hiyo ya Kaimu Rais Jonathan kulivunja baraza la mawaziri, imekuja katika wakati nchi hiyo inakabiliwa na hali ya wasiwasi kufuatia ghasia za kidini zinazotokea kaskazini mwa nchi hiyo na kurejea tena kwa machafuko katika eneo la kusini lenye utajiri wa mafuta.

Kwa mujibu wa ripoti zilizotangazwa mapema jana juu ya kuendelea kwa machafuko ya kikabila na ya kidini nchini humo ambapo watu 13 wameuawa katika ghasia mpya zilizotokea katika katika kijiji kimoja cha eneo la Riyom, kilomita 30 kusini mwa Jos.

Ghasia hizo zimetokea baada ya machafuko mengine ya umwagaji damu kulikumba eneo hilo mwanzoni mwa mwezi huu, ambapo takriban watu 400 waliuawa baada ya watu wa kabila la Fulani kuvamia vijiji vinne na kuwaua wakaazi wengi wa vijiji hivyo vinavyokaliwa na Wakristo wengi.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri.Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 18.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MVm1
 • Tarehe 18.03.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MVm1
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com