AU yapendekeza serikali ya Umoja wa kitaifa Zimbabwe | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 02.07.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

AU yapendekeza serikali ya Umoja wa kitaifa Zimbabwe

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika umekamilisha shughuli zake jana jioni huko nchini Misri kwa kutoa mwito wa kuundwa serikali ya umoja wa taifa nchini Zimbabwe. Nchi za Marekani na Umoja wa Ulaya hazijaridhika.

Mwenyekiti wa AU Jakaya Kikwete,Rais wa Tanzania

Mwenyekiti wa AU Jakaya Kikwete,Rais wa Tanzania

Kulingana na taarifa rasmi iliokamilisha kikao cha faragha, azimio la Umoja wa Afrika linawaomba rais Robert Mugabe na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai kuanza mazungumzo haraka iwezekanavyo kwa ajili ya amani na ustawi na linaunga mkono wazo na kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa huku jumuiya ya maendeleo ya nchi za kanda ya kusini mwa Afrika SADC ikiendelea na jukumu lake la upatanishi.

Azimio hilo limepitishwa baada ya saa mbili za mjadala mkali kutokana na misimamo tofauti ya viongozi waliokuwa mkutanoni juu ya mzozo wa kisiasa unaoikabili Zimbabwe. Afisa mmoja wa Umoja wa Afrika aliwaambia waandishi wa habari kuwa Senegal na Nigeria zilikuwa miongoni mwa nchi zilizopendekeza hatua kali zichukuliwe dhidi ya rais Robert Mugabe. Botswana ilifika mbali hadi kupendekeza Zimbabwe itolewe katika jumuiya ya maendeleo ya nchi za kanda ya kusini mwa Afrika SADC.

Hatimaye kauli ya wapenda mazungumzo ndiyo imepitishwa. Katika taarifa fupi serikali ya rais Robert Mugabe imekaribisha azimio hilo la Umoja wa Afrika na kuridhia na kuwa tayari kuzungumza na yeyote yule bila maelezo zaidi.

Upande wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change MDC cha Morgan Tsvangirai, wamesema watatoa msimamo wao baada ya kutafakari juu ya yaliomo katika azimio hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon licha ya kutoutambuwa uchaguzi wa kutatanisha wa juni 27 ambapo rais Mugabe alikuwa mgombea pekee, amesema atafanya juhudi kuusuluhisha mzozo wa Zimbabwe ambao unaweza kuwa na madhara makubwa na sio tu kwa Zimbabwe, bali pia kwa bara zima la Afrika.


Lakini nchi za Marekani na zile za Umoja wa Ulaya zimeonekana kutoridhika na azimio hilo la Umoja wa Afrika. Marekani imekwisha tayarisha mswada wa azimio wa vikwazo dhidi ya serikali ya rais Mugabe.

Kulingana na balozi wa marekani kwenye Umoja wa mataifa Zalmay Khalilzad, huenda mswada huo ukafikishwa mbele ya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa mnamo wiki hii.Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Bernard Kouchner ambaye nchi yake ndio mwenyekiti mpya wa Umoja wa Ulaya amesema Umoja wa Ulaya hautoitambuwa serikali nchini Zimbabwe isiyo ongozwa na kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai.

Msimamo huo wa Umoja wa Ulaya umetupiliwa mbali na rais wa Afrika ya kusini Thabo Mbeki ambaye ndiye mpatanishi katika mgogoro wa Zimbabwe.

 • Tarehe 02.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EUif
 • Tarehe 02.07.2008
 • Mwandishi Nijimbere, Gregoire
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EUif
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com