Askari 4.500 wa Ujerumna Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.10.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Askari 4.500 wa Ujerumna Afghanistan

Baraza la mawaziri la Ujerumani limeamua kuongeza idadi ya askari wake Afghanistan hadi 4.500.

Baraza la mawaziri la Ujerumani, limeamua leo kurefusha kubaki kwa majeshi ya Ujerumani nchini Afghanistan kwa miezi 14 zaidi.Isitoshe, idadi yao itaongezwa kutoka askari 3.500 hivi sasa na kuwa 4.500.

Kama ilivyotarajiwa Baraza la mawaziri limepitisha mjini Berlin, kurefusha muda wa askari wa Ujerumani nchini Afghanistan.Ilitolewa taarifa hiyo kufuatia kikao cha leo cha Baraza la mawaziri .Mawaziri waliidhinisha pia kuongeza idadi kwa askari 1000 zaidi na kufanya jumla ya askari wa Bundeswehr Afganistan kuwa 4.500.

Hii ilihitajika baada ya Bundeswehr hapo Julai mosi kupeleka Afghjanistan kikosi cha askari 200 huko na kupindukia idadi ya awali ya askari 3.500.

Kwa mara ya kwanza pia muda wa kutumika askari wa Ujerumani nchini Afghanistan umepindukia miezi 12 .Kwa hatua hiyo, inahakishwa kabisa kwamba mwakani haitawezekana kufanya hivyo kwavile ni mwaka wa kampeni ya uchaguzi nchini Ujerumani.Kwamba muda wa kutumika huko utarefushwa tena, yadhihirika hiyo wazi tangu sasa ingawa ridhaa ya wananchi kila kukicha inapungua.

Waziri wa nje wa Ujerumani Bw.Frank-Walter Steinmeier, anapinga kwa kila hali dai la chama cha CSU kuanza tangu sasa mpango wa kuwarejesha nyumbani askari wa Ujerumani kutoka Afghanistan.

Katika mazungumzo na gazeti la Volkszeitung la Leipzig, Bw.Steinmeier alisema kupata imani ya wananchi hakutarahisishwa kwa kuwaarifu na mapema tarehe ya kuwarejesha nyumbani.

Jeshi la Ujerumani halikwenda Hindukuch bila ya sababu,bali linachangia mno kuhakikisha jukumu la usalama nchini linaingia baadae mikononi mwa Waafghani.Mengi yameshafanyika,lakini bado hali ya usalama katika maeneo mengi ya Afghanistan ni ya kutisha.Ndio maana haiwezekani kwa sasa kuyarejesha nyumbani majeshi ya Ujerumani.

Kiongozi wa kundi la wabunge wa chama cha SPD Peter Struck ameukaribisha uamuzi uliopitishwsa leo na Baraza la Mawaziri:

"Nadhani uamuzi uliokatwa wa kuongeza idadi ya askari wa Ujerumani nchini Afghanistan ni sawa. Nitapendekeza kwa wabunge wa chama changu kuungamkono idadi hiyo ya askari 4.500 endapo serikali ya Ujerumani itatoa ombi kama hilo.Nitapendekeza pia hata kuungamkono matumizi ya ndege za AWACS zinazotoa maonyo na mapema ."

Bw.Stuck amepinga pia fikra ya kurejesha wakati huu nyumbani askari wa Ujerumani.Aliongeza:

"Nadhani yatupasa kuchungua barabara hali inavyoendelea nchini Afghanistan .Natarajia pia Rais Karzai ataimarisha jeshi na kikosi chake cha polisi.Tutasaidia zaidi mafunzo ya jeshi hilo. Yafaa kutambuliwa kuwa tunatoa mchango mkubwa katika shughuli za kiraia ,lakini sizungumzii swali la kuyaondoa majeshi.Tunapaswa kila mwaka kuizingatia upya hali ya mambo na kuamua upya."

Bunge la Ujerumani-Bundestag latazamiwa baadae kulipitia kwa mara ya kwanza azimio hilo la kurefusha muda wa jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com