1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Alpha Conde ashinda urais wa Guinea

16 Novemba 2010

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewataka raia wa Guinea wayakubali matokeo na wasuluhishe tofauti zao kwa njia ya mahakama ili kuzuia kutokea machafuko

https://p.dw.com/p/QA8z
Alpha Conde, rais mteule wa GuineaPicha: AP

Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Guinea, Alpha Conde, ametangazwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyofanyika Novemba 7 mwaka huu nchini humo.

Tume huru ya kitaifa ya uchaguzi nchini Guinea hapo jana imetangaza kwamba Alpha Conde mwenye umri wa miaka 72 ameshinda asilimia 52.52 ya kura dhidi ya mpinzani wake waziri mkuu wa zamani, Cellou Dalein Diallo, aliyejishindia asilimia 47.48 ya kura. Asilimia 67 ya wapigaji kura walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo.

Diallo amesisitiza kwamba hatoyakubali matokeo kabla uchunguzi kufanywa kwa kile anachokieleza kuwa kiwango cha juu cha udanganyifu. Hata hivyo amewatolea wito wafuasi wake waendelee kuwa watulivu, wajiepushe na uchokozi na machafuko ya aina yoyote ile. Diallo amesema ataithibitishia mahakama kuu kwamba uchaguzi huo ulikumbwa na mizengwe na kama itakubali kuyachunguza kwa makini madai yake, ana matumaini ya kutangazwa mshindi halali wa uchaguzi huo. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Guinea, Siaka Sangare amesema tume hiyo imepokea malalamiko 31, 28 kati yao kutoka kwa muungano wa Diallo.

Mamadou Bah Diko, msemaji wa muungano unaoongozwa na Diallo amesema, "Tumekuwa na nyaraka na ushahidi sahihi wa visa vikubwa vya udanganyifu vilivyofanika pamoja na kubadilisha mfumo wenyewe wa mawasiliano. Ikiwa matokeo yatatangazwa bila ya kuzingatia malalamiko yetu, basi ni wazi kwamba hatutaweza kuyatambua matokeo yoyote."

Guinea Anhänger Alpha Conde
Wafuasi wa Alpha Conde wakishangilia ushindi katika makao yake makuuPicha: AP

Mahakama kuu inatarajiwa kuridhia matokeo hayo ya uchaguzi yanayompa ushindi Alpha Conde. Conde amesema ushindi wake ni wa kihitoria na ni mwanzo wa enzi mpya. Amewaambia wapinzani wake kuwa wakati umewadia kwa Waguinea kushirikiana kujenga taifa lililoungana na lenye maendeleo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amewahimiza Waguinea kuyakubali matokeo na wasuluhishe tofauti zao kisheria. Ameitaka jumuiya ya kimataifa kuisaidia Guinea wakati huu inapoanza enzi mpya ya kudumisha amani na maendeleo.

Taarifa ya ushindi wa Conde ilitangazwa baada ya siku ya wasiwasi ambapo mtu mmoja aliuwawa na wengine wasiopungua 20 kujeruhiwa kwenye machafuko yaliyotokea katika ngome ya Diallo katika mji mkuu Conakry, wakati wafuasi wake walipokabiliana na vikosi vya usalama.

Corina Dufka, mtafiti wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu katika eneo la Afrika Magharibi, amesema makamanda wa jeshi wanatakiwa mara moja kuvidhibiti vikosi vya usalama na kutimiza jukumu lao la kuyalinda maisha ya raia wa Guinea.

Kimsingi wagombea wote wawili walijaribu kutuliza wasiwasi kabla kufanyika duru ya pili ya uchaguzi kwa kila mmoja kuahidi mwezi uliopita kumshirikisha mwingine kwenye serikali ya umoja wa kitaifa, bila kujali nani atakayeshinda. Hata hivyo kambi hizo mbili zimekabiliana kwenye machafuko makali tangu makubaliano hayo na sasa inasubiriwa kuona kama makubaliano hayo bado yapo. Kama ilivyotokea wakati wa mizozo ya kisiasa baada ya chaguzi nchini Kenya na Zimbabwe, serikali ya umoja wa kitafia nchini Guinea itachukua muda kuundwa.

Mwandishi:Josephat Charo

Mhariri: Aboubakary Liongo