Aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani amejiuzulu | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 27.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani amejiuzulu

Waziri Jung anabeba dhamana na anajiuzulu

Aliyekuwa waziri wa ulinzi na baadae kuwa waziri wa kazi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, leo amejiuzulu na sio tena waziri

Aliyekuwa waziri wa ulinzi na baadae kuwa waziri wa kazi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, leo amejiuzulu na sio tena waziri

Waziri wa zamani wa Ujerumani, Franz Josef Jung, amejiuzulu kutoka wadhifa wake wa hivi sasa wa waziri wa kazi; hivyo kutokuwa tena waziri katika serekali ya Ujerumani. Hii imetokana na ule mkasa wa ndege za kijeshi za NATO kuyashambulia malori mawili ya ya mafuta ya Wataliban huko Afghanistan ambapo inasemekana baadhi ya raia waliuwawa pia. Jana kulitolewa madai kwamba maelezo zaidi juu ya mkasa huo yalifichwa kutolewa hadharani, hivyo kupelekea pia jana mkuu wa majeshi ya Ujerumani, Wolfgang Schneiderhan kuomba aachishwe kutekeleza majukumu yakeWaziri Franz-Josef Jung amejiuzulu kuwa waziri wa kazi muda mfupi baada ya kukataa kuuwacha wadhifa huo, huku mbinyo ukiengezeka dhidi yake juu ya ule mkasa wa kushambuliwa kwa mabomu malori mawili ya kubebea mafuta katika mkoa wa kaskazini wa Kunduz nchi Afghanistan. Inaaminika madarzeni ya raia waliuwawa katika shambulio hilo.

Waziri Franz Josef Jung aliwaambia waandishi wa habari mjini Berlin:

" Leo asubuhi nimemuarifu kansela kwamba najiuzulu kama waziri wa kazi na shughuli za kijamii. Kwa hivyo nabeba dhamana za kisiasa kutokana na siasa za utoaji habari za wizara ya ulinzi ya Ujerumani kuhusiana na mkasa wa Septemba 4 huko Kunduz."

Alisema kutokana na hatua yake hiyo anataka kuisaidia serekali ya Ujerumani kufuatiliza kazi yake bila ya vizuwizi na kuepusha jeshi kuwa na sifa mbaya.

Aliendelea kusema kwamba hana cha kuengezea kuliko kile alichosema jana bungeni, na kwamba yeye aliuarifu vilivyo na vizuri umma na bunge juu ya mkasa huo. Hata hivyo, alisema yuko tayari kushiriki katika juhudi za kuweka uwazi juu ya mkasa huo. Pia alitaja kwamba jambo lilikuwa moyoni mwake sana ni kuwaunga mkono wanajeshi wa Ujerumani ambao wanaendesha operesheni ngumu kwa ajili ya amani na uhuru wa Ujerumani, na pia kuwalinda kutokana na shambulio lisilokuwa la haki.

Franz Josef Jung alikuwa waziri wa ulinzi wakati lilipofanywa shambulio hilo, na akashikilia siku mbili baadae kwamba ni tu magaidi wa Kitaliban ndio waliouliwa.

Hata hivyo, ripoti ya siri ya Shirika la NATO ilitaja mwishoni mwa Oktoba kwamba idadi ya watu waliokufa inapishana baina ya 17 na 142, na duru za mahala hapo zilitaja kwamba baina ya raia 30 na 40 walikufa.

Msimamo wa Bwana Jung ulidhoofika zaidi baada ya kutolewa madai kwamba wizara ya ulinzi ya Ujerumani ilificha ripoti nyingine juu ya mauaji ya raia na ilioashiria kwamba makamanda wa jeshi la nchi kavu hawajazifuata kanuni zilizokubaliwa, lilipokuja suala la kufanya mashambulio.

Baada ya jenerali Schneiderhan kujiuzulu jana, sauti zilizotaka waziri Jung naye ajiuzlu zilizidi kupaazwa juu.

Naye Kansela ameshindwa waziwazi kumtetea waziri wake, akisema tu kwamba uwazi kamili ni muhimu ili kupata imani juu ya operesheni za kijeshi katika Afghanistan, hasa kwa vile uchunguzi wa maoni ya raia hapa nchini unaonesha wengi wao hawaungi mkono operesheni hizo za kijeshi. Ujerumani ndio nchi ya tatu ya kigeni yenye wanajeshi wengi huko Afghanistan, alfu nne na nusu

Franz Josef Jung, mwenye umri wa miaka 60 ,akionekana kuwa si mshirika wa karibu sana wa Kansela Merkel, alihamishiwa kwenye wadhifa mpya wa waziri wa kazi miezi miwili iliopita,

Hadi leo kuna magazeti hapa Ujerumani yaliouliza kwanini Kansela Merkel anagandana na waziri Jung, kwani kuondoka kwake hakutakuwa hasara kwa baraza la mawaziri.

Mwandishi: Miraji Othman / Reuters/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 27.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kj9m
 • Tarehe 27.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Kj9m
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com