Algeria yaipiga kumbo Misri nje ya Kombe la dunia 2010 | Michezo | DW | 19.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Algeria yaipiga kumbo Misri nje ya Kombe la dunia 2010

Ujerumani yatoka suluhu na Ivory Coast 2:2

default

Ivory Coast Vs.Ujerumani

Tiketi za mwisho za kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia 2010 nchini Afrika kusini ziligawanywa jana kanda ya Ulaya,Afrika na Amerika Kusini .Sasa ,timu zote 32 zitakazoingia uwanjani Juni 11, mwakani, zinajulikana:

Ilikua "asie na mwana aeleke jiwe jana usiku mjini Algiers, na asie na mguu alitia gongo"-mkutano mitaani na mikahawani.Kwani, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, waalgeria wote waliingia mitaani mara tu baada ya firimbi ya mwisho kulia mjini Khartoum, kushangiria sio tu kufuzu kwa Kombe klijalo la dunia, bali kwa kulipiza pia kisasi kwa mahasimu wao wakubwa -mabingwa wa Afrika, Misri, waliowatimua nje ya kombe hili hili 1989 pia kwa bao 1:0 na kwenda wao mafiraouni nchini Itali ,1990.

Taarifa kutoka Algiers, zinasema hata baadhi ya polisi walipandwa na shetani wa mpira, kwani walipiga vin'gora vyao vya magari yao ya polisi kushangiria timu yao iliofufuka kutoka mpambano wa kufa-kupona .

Umati mkubwa wa mashabiki pia ulikuwa majiani katika mji wa Oran wa mwambao wa pwani na shangwe kama hizo, zimeripotiwa katika miji na hata viviji vya Algeria nzima.

Hali ya mambo ilikua tofauti mjini Cairo na Misri nzima:Mitaa ya Misri ambayo kikawaida husheni watu, ilikuwa mitupu wakati wa mechi hiyo.Shabiki mmoja wa Misri,Khaled Hassan, aliungama ," Siku moja unashinda, nyengine unashindwa". Akigusia hapo ule ushindi wa mabao 2:0 wa Mafiraouni mjini Cairo dhidi ya Algeria Jumamosi iliopita. Katika mkahawa mmoja mjini Cairo, shabiki mmoja alizima ilipolia firimbi ya mwisho huko Khartoum na kubidi kutiwa katika Taxi hadi hospitali.

Ushindi wa Algeria, ulisherehekewa pia katika mitaa ya Paris na Marseille,Ufaransa,mkoloni wa zamani wa Algeria, hadi ukombozi 1962.

Ufaransa yenyewe lakini, ilikirimiwa tiketi yake ya Kombe la dunia 2010 kwenye sahani baada ya stadi wao Thierry Henry, kuunawa mpira kwa mkono na kumtupia William Gallas kuusindikiza wavuni mwa lango la Ireland dakika ya 103 ya kurefushwa mchezo.Ireland iliosawazisha bao la Ufaransa huko Ireland la Jumamosi iliopita ,ililalamika sana kutolewa namna hiyo nje ya Kombe la dunia 2010.

Ureno, bila ya Cristiano Ronaldo, imeitimua nje Bosnia kwa bao 1:0 na kuondoka Sarajevo na tiketi ya Afrika Kusini.Slovenia, imeitimua nje Russia wakati Ugiriki, imetamba mbele ya Ukraine.

Katika dimba la kirafiki,Ivory Coast, ikiongoza kwa mabao 2:1 la Ujerumani hadi dakika za kufidia kabla Lukas Podolski, kutia bao lake la pili na kusawazisha mchezo mabao 2:2 mjini Gelsenkirchen.Mpambano mzima ,uligubikwa na matanga ya kifo cha kipa wa Ujerumani, Robert Enke.Hata Waivory -Coast waliocheza bila nahodha wao Didier Drogba,walivaa fulana za picha ya marehemu Enke wakichangia katika maomblezi.

Mwandishi: Ramadhan Ali/afp,dpa

Mhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com