Afrika katika Magazeti ya Ujerumani Wiki hii | Magazetini | DW | 06.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani Wiki hii

Uchaguzi mkuu wa Tanzania, mkutano wa kilele kati ya Afrika na India na hali ya mambo nchini Nigeria ni miongoni mwa mada za bara la Afrika zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii.

default

Rais mpya wa tanzania John Magufuli na makamo wa rais bibi Samia Suluhu baada ya kuapishwa

Tuanzie lakini Tanzania ambako rais wa awamu ya tano Dr. John Pombe Magufuli ameapishwa alkhamisi iliyopita licha ya zoezi la uchaguzi mkuu ulioingia ila kutokana na kubatilishwa zoezi kama hilo visiwani Zanzibar.Gazeti la kusini mwa Ujerumani "Süddeutsche Zeitung" linayataja matokeo ya uchaguzi kuwa "ya ushindani mkubwa kuliko wakati wowote ule mwengine."Chama tawala nchini Tanzania kinaendelea bila ya kutarajiwa kuwepo madarakani" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo linalozungumzia ishara kubwa iliyochomoza hapo awali ya kutokea mabadiliko.Lakini katika uchaguzi wa bunge na rais ulioitishwa jumapili iliyopita katika nchi hiyo ya Afrika mashariki,tume ya uchaguzi NEC imemtaja mgombea wa chama tawala CCM John Magufuli kuwa ndie rais mpya.Mgombea wa muungano wa upande wa upinzani UKAWA,Edward Lowassa anayabisha.Süddeutsche Zeitung linasema wasimamizi waliashiria nafasi nzuri ya kushinda upande wa upinzani -tukio ambalo lingekuwa la aina yake nchini Tanzania ambako hadi wakati huu hakuna chama chochote kilichoweza kugeuka kitisho cha kweli kwa CCM.Süddeutsche linakumbusha chama hicho kilichoundwa na mwasisi wa taifa hilo Julius Nyerere, kinaitawala nchi hiyo tangu uhuru mwaka 1961.Ingawa wasimamizi wa kimataifa wanasifu uchaguzi huo umepita kwa amani,hata hivyo wanakosoa ukosefu wa uwazi.Tume ya Umoja wa Ulaya inakikosoa chama tawala kwa kutumia raslimali ya taifa kwa masilahi ya kampeni za uchaguzi.Süddeutsche Zeitung limezungumzia pia lawama za wasimamizi kutokana na kubatilishwa zoezi la uchaguzi visiwani Zanzibar-Kinyume na tume ya uchaguzi ZEC ilivyodai,gazeti hilo linasema wasimamizi wa kimataifa wamesema zoezi la uchaguzi visiwani humo lilipita vizuri.Gazeti hilo la kusini mwa Ujerumani linahofia pasije pakatokea machafuko katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kutaja malumbano yaliyotokea mwanzoni mwa wiki kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali.

Chui wa Asia na Simba wa Afrika wanguruma

Mkutano wa kilele kati ya viongozi wa bara la Afrika na India mjini New-Delhi,nao pia umemulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii."India inataka kujijenga upya barani Afrika ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Neue Zürcher Zeitung linalozungumzia juu ya kufufuliwa upya ushirikiano baina ya nchi za kusini wenyewe kwa wenyewe.Ushirikiano wa kiuchumi umeimarishwa na biashara kati ya India na Afrika katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita imeongezeka mara kumi.New-Delhi inataka biashara hiyo iongezeke mara dufu hadi ifikapo mwaka 2022.Chui wa Asia na simba wa Afrika wananguruma namna moja linaendelea kuandika gazeti hilo la Neue Zürcher linaloashiria matumaini ya ukuaji mkubwa wa kiuchumi kwa maeneo hayo mawili makubwa ambayo gazeti linasaema takriban nusu ya wakaazi wa dunia watakuwa wanaishi katika maeneo hayo hadi ifikapo kati kati ya karne hii.

Mwanajeshi kavaa koti la kidemokrasia Nigeria

Gazeti la mji mkuu wa Ujerumani-"Berliner Zeitung" linamulika baraza jipya la mawaziri nchini Nigeria na kusema rais Muhammadu Buhari anaiongoza peke yake nchi hiyo,miezi karibu sita baada ya kuingia madarakani.Mara baada ya kukabidhiwa hatamu za uongozi,Muhammadu Buhari aliweka rekodi ya dunia.Miezi zaidi ya mitano baadae,ndio kwanza anatarajiwa kutangaza baraza lake la mawaziri.Muda wote huo bwana huyo mwenye umri wa miaka 72 alikuwa akiitawala peke yake nchi hiyo yenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika.Baadhi walikuwa tayari wakihofia kwamba bwana huyo ambae katika miaka ya 80 aliwahi kuongoza utawala wa kimabavu wa kijeshi,asingeweza kugeuka mwanademokrasia.Wafuasi wake lakini wanasema muda huo wa kusubiri haukuwa wa bure:rais na wapinzani wa rushwa walikuwa wakiwakagua mawaziri wake.Kati ya mawaziri 36 na wasaidizi wao,kuna wengi wanaojulikana,miongoni mwao wakiwemo magavana watano wa zamani wa majimbo 36 ya nchi hiyo,maseneta wanne wa zamani na majenereli wawili wastaafu.Berliner Zeitung limewaanukuu wakosoaji wakisema takriban mawaziri wote waliochaguliwa wanatokea katika sekta ya kisiasa ambayo ni mojawapo ya vyenzo vya matatizo na sio ya ufumbuzi kwa Nigeria.Jambo pekee la kustaajabisha ni kwamba safari hii wanawake sita wamechaguliwa kuwa mawaziri ikiwa ni pamaoja na mwanaharakati wa haki za binaadam Femi Falana.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com