Wito kwa Rais wa zamani wa Chad,Hissene Habre, afikishwe mahakamani | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wito kwa Rais wa zamani wa Chad,Hissene Habre, afikishwe mahakamani

AU yalaumiwa kwa kuzubaa katika kusaidia kufikishwa Hissene Habre mahakamani

Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre, aliye uhamishoni Senegal

Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre, aliye uhamishoni Senegal

Zaidi ya miezi 30 baada ya kuiomba Senegal imshtaki mdikteta wa zamani wa Chad, Hissene Habre, Umoja wa Afrika, AU, lazima uhakikishe kwamba kesi hiyo inasonga mbele. Hayo yametakiwa na makundi matano ya kiafrika na ya kimataifa yanayopigania haki za binadamu. Viongozi wa nchi za Kiafrika watakutana mjini Addis ababa jumapili ijayo katika mkutano wao wa kilele.

Katika mkutano wa kilele uliofanywa July 2, 2006, AU iliipa jukumu Senegal imshtaki na kuhakikisha kwamba Hissene Habre anashtakiwa kwa niaba ya Afrika, na ukaitaka Tume ya Umoja wa Afrika kuipa Senegal msaada unaohitaji ili kesi hiyo ifanyike vilivyo. Hissene Habre anaishi uhamishoni nchini Senegal.

Lakini Senegal haijachukua hatua na AU haijaipa msaada nchi hiyo. Hayo yalisemwa na Jumuiya ya Chad ya Kuendeleza na Kutetea Haki za Binadamu, Jumuiya ya Chad Inayowashughulikia Watu Waliokandamizwa Kisiasa na Kufanyiwa Uhalifu, Hadhara ya Afrika kwa ajili ya Kutetea Haki za Binadamu, Human Rights Watch ya Marekani na Shirikisho la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu.

Dobian Assingar wa Shirikisho la Kimataifa la kupigania haki za binadamu, FIDH, amesema wao wanautarajia Umoja wa Afrika kuheshimu nia iliotoa kuhakikisha kwamba kesi hiyo inasonga mbele. Alisema hapa ni suala la heshima ya AU, na ni kwamba Senegal na AU zimezubaa na kuzubaa.

Hissene Habre aliitawala Chad toka mwaka 1982 hadi pale alipopinduliwa kutoka madarakani na Rais Idriss Deby mwaka 1990, na akakimbilia Senegal. Utawala wake wa chama kimoja ulijulikana kwa kuzagaa vitendo vya kikatili na kampeni ya kuyaonea baadhi ya makabila. Mafaili ya polisi wa kisiasa wa Habre, DDS, ambayo yaligunduliwa na Shirika la Human Rights Watch mwaka 2001 yalionesha majina ya watu 1,208 ambao waliuliwa au kufa wakiwa vizuizini. Jumla ya watu 12,321 walioteswa majina yao yalikuwemo katika faili hizo.

Kutokana na Senegal kutochukuwa hatua, hapo Septemba 16, mwaka 2008, watu 14 walioonewa walitoa malalamiko mepya mbele ya mwendeshaji mashtaka wa Senegal, wakimtuhumu Habre kwamba alifanya uhalifu dhidi ya uutu na pia kutesa. Wakuu wa polisi walisema hawatachukuwa hatua kutokana na malalamiko hayo hadi pale jamii ya kimataifa itakapogharimia kikamilifu, kifedha, kesi hiyo, ambayo Senegal imesema itachukuwa Euro milioni 27.4

Makundi hayo ya kupigania haki za binadamu yameashiria kwamba kesi kama hizo kwa kawaida hugharimiwa mwaka kwa mwaka, na Jumuiya ya Ulaya umeshatoa Euro milioni mbili kwa hatua za kwanza za upelelezi, lakini unangoja Senegal iwasilishe bajeti. Chad imejitolea kutoa Euro milioni tatu. Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi na Uswissi nazo pia zimekubali kugharimia kesi hiyo. Umoja wa Afrika, hata hivyo, haujatoa msaada.

Jacqueline Moudeina, wakili wa watu hao walioteswa na pia ni Rais wa Jumuiya ya Chad ya Kuendeleza Kutetea Haki za Binadamu, anasema Umoja wa Afrika na Senegal ziko katika hatari ya kuonekana kama washirkak katika juhudi za Hissene Habre kuhepa kupewa adhabu. Jambo hilo ni aibu kwa Afrika. Aliuliza jee iko nia ya kisiasa ya kumfikisha Hissene Habre mahakamani?

Akizungumza kwa niaba ya watu walioonewa, Souleymane Guengueng, muasisi wa Jumuiya ya Chad ya Watu Waliokandamizwa Kisiasa na kufanyiwa Uhalifu, alisema wao kwanza waliteswa na udikteta wa Habre na sasa kwa miaka 18 wamekuwa wakifanyiwa mzaha na viongozi wa Senegal na wa Afrika ambao wanakataa kusikiliza miito ya kuweko haki. Alisema ikiwa Senegal na AU hazitachukuwa hatua karibuni, basi hakutakuweko tena mtu yeyote kati ya wale walioteswa kuweza kufika mahakamani.

Alioune Tine, rais wa Hadhara ya Afrika ya Kutetea Haki za Binadamu, RADDHO, anasema Umoja wa Afrika unakasirika pale Waafrika wanapokabiliwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, lakini tatizo hasa ni kwamba mahakama katika Afrika hazina nguvu mbele ya uhalifu uliofanywa na viongozi wa Kiafrika. Kesi ya Habre iwe ni mfano kuonesha kwamba mahakama za Kiafrika zinaweza kutoa hukumu zilizo huru, za haki na thabiti kwa uhalifu uliofanyika Afrika.
 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gi6B
 • Tarehe 28.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gi6B
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com