Waziri Mkuu wa Misri aomba radhi kwa mauaji ya waandamanaji | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.02.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Mkuu wa Misri aomba radhi kwa mauaji ya waandamanaji

Huku mbinyo wa kimataifa ukiongezeka dhidi ya serikali ya Misri, kutokana na mashambulizi dhidi ya waandamanaji walio kwenye uwanja wa Tahrir, Waziri Mkuu Ahmed Shafiq ameomba radhi kwa taifa na kuahidi uchunguzi.

Vifaru vya jeshi vikiweka uzio kati ya waandamanaji

Vifaru vya jeshi vikiweka uzio kati ya waandamanaji

Ahmed Shafiq, Waziri Mkuu wa Misri, sasa ameamua kuja hadharani, kuzungumzia msimamo wa serikali yake juu ya mashambulizi ya jana usiku dhidi ya waandamanaji waliokusanyika kwa amani kwenye uwanja wa Tahrir.

"Kama serikali na dola, ni lazima kuwalinda raia wake. Kwa hivyo, ni muhimu na lazima kwangu kuomba radhi na kuahidi kuwa tukio kama hili, halitarejewa tena." Amesema Shafiq.

Akizungumza kwa utaratibu mbele ya waandishi wa habari, Shafiq ametumia kila aina ya msamiati kuitenga serikali yake kando na matukio ya usiku wa jana, akiyapa kila jina la kuyalaani: ushenzi, ukosefu wa nidhamu, uharibifu kwa taifa, na mwisho akaahidi kuchukua kila jitihada kurudisha imani ya wananchi kwa serikali yao.

Shafiq atafuta maridhiano na wapinzani

Kijana anayetuhumiwa kufanya hujuma dhidi ya waandamanaji

Kijana anayetuhumiwa kufanya hujuma dhidi ya waandamanaji

Shafiq ametumia mkutano huu pia kuwaalika viongozi wa maandamano pamoja na makundi yote ya upinzani, likiwemo la Ikhwanul-Muslimin, kushiriki kwenye mazungumzo ya kuufundua mfundo wa kisiasa ulioikabili nchi yao.

Na japokuwa si lazima iwe kila mtu amekimeza kila alichokisema, angalau ametoa ishara kwamba shinikizo la ndani na nje, huweza kuilazimisha serikali kulegeza msimamo wake.

Huku Shafeq akizungumza na waandishi wa habari, mwendesha mashtaka wa serikali ametoa hati inayowazuia kusafiri na kuzifungia akaunti zao za benki baadhi ya wajumbe wa baraza la mawaziri lililoondoshwa madarakani hivi karibuni na Rais Mubarak.

Mawaziri wa zamani wazuiliwa

Mwandamanaji anayeipinga serikali kwenye uwanja wa Tahrir

Mwandamanaji anayeipinga serikali kwenye uwanja wa Tahrir

Kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Habib Al-Adly, waziri wa makaazi, Ahmed al-Maghrabi, na waziri wa utalii, Zuhair Garana, pamoja na kada maarufu wa chama tawala, Ahmed Ezz, ni miongoni mwa waliozuiliwa hadi hapo usalama wa taifa utakaporejea na uchunguzi dhidi yao kukamilika.

Yote haya yanakuja hata masaa 24 bado tangu Makamo wake wa Rais, Omar Suleiman, kusema kwamba serikali haitaongea na wapinzani hadi hapo wapinzani hao watakapositisha maandamano yao yanayoendelea kwa siku ya kumi sasa, na wapinzani nao kusema kuwa hawataongea na serikali mpaka Mubarak aondoke madarakani.

Waandishi wa habari washambuliwa

Al Jazeera Al Arabiya

Al Jazeera Al Arabiya

Wakati haya yakiendelea, waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binaadamu wameripoti kuendelea kushambuliwa na makundi ya wafuasi wa Rais Mubarak na maafisa wa usalama. Waandishi wa kituo cha habari cha Al-Arabiya, Al-Jazeera na wale wa kutoka nchi za Magharibi ni miongoni mwa ambao ama wajeruhiwa na au vifaa vyao vya kazi kuvunjwa.

Vodafone yalazimishwa kutumika bila ridhaa yake

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron

Kwengineko, kampuni ya Vodafone Group PLC, inayomiliki kampuni ya simu za mkononi ya Vodafone na yenye makao yake makuu nchini Uingereza, imesema kwamba serikali ya Misri iliilazimisha kutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi, unaouunga mkono serikali, wakati maanndamano dhidi ya Mubarak yakiendelea.

Katika taarifa yake ya leo, kampuni hiyo imesema kuwa serikali ya Misri imekuwa ikitumia sheria yake ya Hali ya hatari, kuilazimisha kampuni hiyo kutumika kinyume na ridhaa yake.

Nayo serikali ya Uingereza imetuma ndege ya pili leo kuwaondosha raia wake walioko Misri, huku nchi hiyo ikizidi kuzama kwenye wimbi la machafuko na maandamano. Jana Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alisema kuwa kiasi ya raia 3,000 wa nchi yake bado wapo mjini Cairo hadi sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFPAE/Reuters
Mhariri: Miraji Othman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com