Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ahojiwa tena juu ya ufisadi | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert ahojiwa tena juu ya ufisadi

Maofisa wa Israel wameemendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri Mkuu wa nchi hiyo Ehud Olmert, ikiwemo ubinafshaji wa benki moja.

Waziri Mkuu wa Israel, Ehud Olmert

Waziri Mkuu wa Israel, Ehud Olmert

Kikosi cha maofisa wa polisi wa Israel leo kimeendeleza uchunguzi wake dhidi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Bwana Ehud Olmert, kuhusiana na tuhuma za kuhusika katika ubinafsishaji wa benki moja mjini Yerusalem.

Msemaji wa polisi Micky Rosenfeld amesema maofisa wao waliingia ofisini kwa Waziri Mkuu huyo baada ya kuripoti ofisini na kumhoji maswali kadhaa yatakayosaidia kwa ushahidi ikiwa atafikishwa mahakamani.

Ziara hiyo ya maafisa wa upelelezi ni ya pili katika kipindi cha juma hili baada ya ile iliyofanyika siku ya Jumanne, ambapo polisi walimhoji kwa muda wa saa tano, wakitaka kufahamu kama alishiriki katika kubinafsisha benki ya Leumi miaka miwili iliyopita, ambayo ni ya pili kwa ukubwa nchini Israel.

Polisi wanafikiri kwamba Waziri Mkuu huyo wa Israel alishiriki kufanikisha mpango wa ubinafshaji wa benki hiyo, wakati akikaimu nafasi ya Waziri wa Fedha katika serikali ya Waziri Mkuu aliyepita, Bwana Ariel Sharon.

Benki ya Leumi ya Israel iliuzwa kwa mtu mmoja anayeitwa Frank Lowey mwenye asili ya Australia, anayesemekana kuwa rafiki wa karibu sana na Bwana Olmert, na baadaye benki hiyo iliuzwa kwa kampuni nyingine. Hiyo si kashfa pekee inayomkabiri waziri mkuu huyo wa Israel mwenye umri wa miaka 62 sasa, kwa kuwa pia ana tuhuma nyingine ya ununuzi wa nyumba ya kifahari mjini Yerusalem mwaka 2004, yenye thamani ya dola laki tatu za Marekani.

Mnamo majuma mawili yaliyopita, Mwanasheria Mkuu wa Israel Bwana Menachem Mzuz alitoa amri ya kufanyika uchunguzi kuhusu kashfa hiyo inayohusishwa na vitendo vya rushwa alivyofanya Bwana Olmert.

Wakati maofisa wa polisi wakiendelea na uchunguzi wa kashfa hizo, pia Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert anaendelea kusakamawa na watu wake kuhusiana na jinsi serikali yake ilivyohusika katika vita ya Lebanon iliyogharimu mamilioni ya pesa na vifo vya raia.

Kwa miezi kadhaa sasa waziri mkuu Ehud Olmert na ofisa wa upelelezi Micha Lindenstrauss wamekuwa wakitofautiana kutokana na kashfa hizo na Bwana Lindenstrauss ameonya ikiwa Olmert atamfukuza kazi mmoja wa wahasibu walioibua tuhuma dhidi yake.

Tayari kuna fununu kwamba huenda Wizara ya Fedha ya Israel ikamfukuza kazi mhasibu wake Yaron Zelekha, lakini maofisa wa polisi wameonya ikiwa kitendo hicho kitafanyika. Wakati Bwana Olmert akikabiliwa na tuhuma hizo, mwezi wa tano mwaka huu naye alijaribu kutumia wadhifa wake kuona kama maofisa wa polisi wanatumia nafasi zao sawasawa.

Wakati tuhuma hizo za Ehud Olmert zikiendelea, majeshi ya Israel yamemuua raia mmoja wa Palestina anayesadikika kuwa wakala wa usalama katika mapigano yaliyotokea kwenye mji wa Jenin ulioko Ukingo wa Magharibi. Hata hivyo msemaji wa jeshi la Israel hakuweza kuzungumza lolote kuhusu tukio hilo, kwa madai kwamba mpaka atakapokuwa na taarifa zaidi.

Kifo cha wakala huyo wa usalama wa Palestina, kinatimiza idadi ya watu elfu 5 na 888 waliouawa katika mashambulizi baina ya Israel na Palestina tangu machafuko yalipopamba moto mwaka 2000.

 • Tarehe 11.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7i3
 • Tarehe 11.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7i3

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com