Waziri mdogo wa afya wa Irak akamatwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri mdogo wa afya wa Irak akamatwa

Jeshi la Irak limemzuilia waziri mdogo wa Afya ambae pia ni mjumbe wa chama cha Moqtada al Sadr kiongozi wa kidini na mpinzani mkubwa wa sera za Marekani nchini Irak.Hii inafuatia msako mkubwa wa kiusalama katika mji wa Baghdad.

Kushoto waziri mkuu wa Irak Nuri al Maliki na rais wa Irak Jalal Talabani

Kushoto waziri mkuu wa Irak Nuri al Maliki na rais wa Irak Jalal Talabani

Ripoti za awali za jeshi la Irak zilisema kuwa vikosi hivyo vimemkamata afisa wa cheo cha juu katika wizara ya afya nchini humo kwa tuhuma za kuwapenyeza wapigananji wa kundi la Mehdi la mpinzani wa sera za Marekani nchini Irak mwanachuoni maarufu Moqtada al Sadr katika wizara hiyo.

Watu walioshuhudia tukio hilo la kukamatwa kiongozi huyo wamesema kuwa ni waziri mdogo wa afya Hakim Zamili ambae anatoka katika chama cha Moqtada al Sadr.

Hakim al Zamili anatuhumiwa kwa kuwasaidia wapiganaji wa Kishia na pia kuwaruhusu kuyageuza magari ya ambulesi kuendeleza vitendo vya kuwatisha na kuhatarisha usalama wa raia.

Waziri huyo mdogo anatuhumiwa kuwa ndie mfadhili mkuu wa wapinzani kwa kuwa amewaajiri wapiganaji wengi katika wizara yake ya afya.

Anatuhumiwa pia kuhusika na rushwa ya milioni kadhaa ya dola za kimarekani.

Wapiganaji wa kundi la Mehdi wanadaiwa kuwalenga raia wa Irak kwa kutumia huduma za shirika la afya kama vile magari na kadhalika ili kufanikisha utekaji nyara na pia mauaji.

Waziri mkuu wa Irak Nuri al Maliki ametoa amri ya kukamatwa wapiganaji wote wa Kishia na wa Kisunni katika operesheni hiyo inayoendeshwa katika mji wa Baghdad.

Wakosoaji hata hivyo wamesema kuwa operesheni kama hiyo haikufaulu mwanzoni kwa kuwa iliwalenga baadhi ya watu tu na kuwaacha wapiganaji wa Kishia ambao wana uhusiano na vyama vilivyomo katika serikali ya mseto ya Irak.

Waleed ambae ni kaka wa waziri mdogo huyo aliyekamatwa amekanusha tuhuma dhidi ya nduguye wakati alipozungumza na shirika la habari la Reuters na kusema kuwa wakati wowote anapokamatwa mtu kutoka chama cha Sadr nchini Irak basi imekuwa ni kawaida kulimbikiziwa tuhuma za kila aina.

Majeshi ya muungano ya Irak na Marekani yameongeza makali katika operesheni dhidi ya watu wanomuunga mkono Sadr na wapiganaji wa Mehdi ambao Marekani inawatuhumu kwa kuhusika na utekaji nyara na pia mauaji.

Msemaji wa wizara ya afya Qassim Allawi amesema kwamba leo mwendo wa saa tatu asubuhi walifika wanajeshi wa Marekani na wale wa Irak na kuamuru kila mtu alale chini katika majengo ya wizara ya afya na ndipo walipomchukuwa waziri huyo mdogo Hakim al Zamili.

Kukamatwa kwa waziri huyo mdogo kumetokea siku moja tu baada ya jeshi la Marekani nchini Irak kutangaza kuwa operesheni ya mji wa Baghdad imeanza.

Mwanachama mmoja wa chama cha Moqtada al Sadr ameitaka serikali ya Irak ichukue hatua kwa kile alichokitaja kuwa jeshi la Marekani linatafuta makabiliano kwa nguvu.

Wakati huo huo bomu lililotegwa ndani ya gari limelipuka na kuwauwa watu 20.

Gari hilo lili egeshwa kando ya soko la nyama katika mji wa Aziziyah ulio kilomita 90 kusini mwa mji wa Baghdad mji ambo unakaliwa na jimii kubwa ya Kishia.

Taarifa ya polisi pia imetaja kuwa watu 450 wamejeruhiwa katika mlipuko huo.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com