1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waturuki hawataki utawala wa sheria za Kiislamu, pia hawataki mapinduzi ya kijeshi.

30 Aprili 2007

Nchini Uturuki yaonesha kuna mushkili mkubwa baina ya serekali ya Ki-Conservative yenye kuelemea itikadi za Kiislamu ya Chama cha Haki na Maendeleo, AKP, na jeshi la nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/CHF8
Mtetezi wa urais na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Abdullah Gül
Mtetezi wa urais na waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Abdullah GülPicha: AP

Jeshi limenyosha kidole kuoya kwamba halitanyamaa kimya pindi atachaguliwa waziri wa sasa wa mambo ya kigeni, Abdullah Gül, kuwa rais wa nchi hiyo. Lakini serekali ya waziri mkuu Tayyip Erdogan yaonesha haiko tayari kulipigia magoti jeshi ambalo maisha limekuwa na ushawishi mkubwa katika nchi hiyo na kujinata kwamba ndio mlinzi wa katiba ya nchi hiyo ilioasisiwa na Kemel Atatürk baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Katiba hiyo inasema wazi kwamba dini isiingizwe katika shughuli za serekali. Tayyip Erdogan alikuwa na hakika kwamba rafiki yake, Abdullah Gül, atachaguliwa na wabunge katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo hapo wiki iliopita. Lakini sheria inasema kwa mtetezi kutangazwa kuwa mshindi wa urais, anahitaji aungwe mkono na thuluthi mbili ya wabunge katika duru ya kwanza au ya pili itakayofanywa wiki hii. Ikiwa jambo hilo halitawezekana, basi ndipo kutafanywa duru ya tatu ambapo mshindi ni yule atakayepata zaidi ya asilimia 50. Chama tawala cha AKP kina wingi wa kutosha kupata kura hizo katika duru ya tatu. Lakini mambo yamekorogeka hivi sasa kwa vile wabunge wa vyama vya upinzani wamesusia uchaguzi huo bungeni na kuwasilisha malalamiko yao mbele ya mahakama ya kikatiba kumpinga Abdullah Gül kwa hoja kwamba mkusanyiko wa bunge ulikuwa hauna washirika wa kutosha na kwamba Abdullah Gül historia yake yaonesha ni mtu mwenye kufuata itikadi kali za Kiislamu.

Nilimuuliza Mehboob Khan, Mswahili anayeishi mjini Istanbul, huko Uturuki kwa miaka mingi kama hayo ni kweli juu ya Abdullah Gül:

Mkorogano ulizidi pale jeshi nalo lilipoingilia kati na kumkumbusha Tayyip Erdogan nani aliye na madaraka nchini Uturuki.Lilisema linafuatiliza kwa wasiwasi hali ya mambo inavokwenda, lakini watu wasiwe na wasiwasi juu ya msimamo ulio wazi wa jeshi. Hapo hapo serekali ikatoa taarifa kali ikisema haikubaliki kwamba katika nchi hiyo ya kidimokrasia inayofuata mifumo ya sheria, jeshi, ambalo liko chini ya amri ya waziri mkuu, litoe taarifa dhidi ya serekali. Pia Tume ya Umoja wa Ulaya ililalamika namna jeshi la Uturuki linavojiingiza katika mambo ya siasa, na likasema huo ni mtihani kwa lile suali kama jeshi la Uturuki linaheshimu msingi uliowekwa wa uhusiano baina ya dola na jeshi.

Mabishano yalianza wiki mbili zilizopita pale maelfu kwa maelfu ya waandamanaji walipopita katika mabarabara ya mji wa Ankara. Mwisho wa wiki iliopita malaki ya waandamanaji wengine walipita katika mjia ya Istanbul wakitaka dola itenganishwe na dini. Muandamanaji wa kike alisema:

+Tumeona kwamba maisha yetu ya baadae yamo hatarini hasa sera ya Hayati Atatürk ya serekali kutoelemea sana dini. Ndio maana tuko hapa.+

Kwa mujibu wa wanajeshi ni kwamba mtu ambaye atakayekamata wadhifa huo lazima aheshimu misingi ya katiba, sio tu kwa maneno lakini pia kwa vitendo. Ama sivyo wametishia kwamba wataingilia kati. Tangazo hilo lazima lichukuliwe kuwa ni onyo kwamba kutafanywa mapinduzi ya kijeshi.

Lakini mwenyewe Abdullah Gül amesema katukatu atabakia na azma yake ya kutaka kuwa rais, hivyo kuiingiza Uturuki katika mtihani mkubwa wa kupimana nguvu za kisiasa.

+Harakati bado zinaendelea. Hii ina maana sitajiondoa katika kuwania urais, kwa sababu kushiriki kwangu sio matokeo yanayotangazwa baada ya siku moja, bali itachukuwa muda wa mashauriano. Lazima sasa tuubiri uauzi wa mahakama ya katiba. Hadi hapo watu wanatakiwa wawe watulivu.+

Wasiwasi huo ulielezewa na waandamanaji wa mjini Istanbuli wakisema hawataki utawala wa sheria za Kiislamu na pia hawataki mapinduzi ya kijeshi. Tangu mwaka 1960, jeshi katika Uturuki limefanya mapinduzi mara nne, na tena sasa nchi hiyo iko katika hatari kama hiyo.

Majenerali wanadai kwamba wanaiona Uturuki ikiingia katika mfumo wa serekali ya Kiislamu tangu chama cha AKP kiingie madarakani. Kwa mfano hapo April 23, sikukuu ya taifa, serekali imepanga kufanya mashindano ya kitaifa ya hadharani ya kusoma Quran. Siku chache zilizopita, makada wa chama cha AKP katika mji wa sanliurfa walikilazimisha kikundi cha kwaya cha wasichana kujitiokeza hadharani wakiwa wamevaa mitandio na kuimba nyimbo za dini. Katika visa vingine, sherehe za za Kiislamu zimefanyika katika shule. Wanajeshi wanadai kwamba kule kuuliwa karibuni Wakristo watatu katika mji wa kusini wa mashariki wa Malatya ni mfano mwengine wa kuongezeka mkondo wa siasa kali za kidini, na kwamba kuna duru maalum zinazojitahidi sana kuizika misingi ya thamani za jamhuri ya Uturuki.

Tayyip Erdogan na Abdullah Gül, bila ya shaka, wanayaona maonyo hayo ya sasa ya majenerali kuwa ni kukaririwa ile amri iliotolewa Februari 28 mwaka 1997 na wakuu wa wakati huo jeshini dhidi ya waziri mkuu Necmettin Erbakan aliyekuwa anaelemea katika siasa za itikadi za Kiislamu. Erdogan na Gül ni warithi wa siasa za Erbakan. Wakati huo pia ilidaiwa kwamba serekali ilikuwa inawastahamilia watu wenye siasa za Kiislamu. Erbakan alilidharau onyo hilo, lakini miezi minne baadae majenerali wakamtimua kutoka madarakani. Mwaka mmoja baadae chama cha Ustawi wa jamii cha Erbakan kilipigwa marufuku kwa madai kwamba kilikuwa kikiendeshwa kinyume na katiba, na Erdogan alitupwa gerezani kwa mashtaka ya kuchochea chuki za kidini.

Kwa hivyo, sio hasha kwamba maonyo haya ya sasa ya wanajeshi hayawezi kudharauliwa. Lakini ni taabu kutambua tangao la wanajeshi lilikusudiwa kwa watu gani, hasa ilivokuwa mahakama ya kikatiba nchini humo ambayo wiki hii inatakiwa iamuwe kama uchaguzi huo wa urais unaweza ukafanyika wakati chini ya thuluthi mbili ya wanabunge watashiriki. Huenda bunge la sasa lisiweze kuchaguwa rais na hivyo kujivunja. Vyama vya upinzani vimerejea tena mwito wao kwamba uchaguzi wa mapema wa bunge uitishwe, kama njia ya kujikwamua kutoka kwenye mzozo huo. Lakini jee jambo hilo litakuwa ni kwa maslahi ya Uturuki, na jee Chama cha AKP kitaweza kurejea tena madarakani kwa wingi kama mara iliopita. Mehbood Khan kutoka Istanbul ana maoni haya:

Miraji Othman