Wapinzani wa ziara ya Papa wapingwa | Magazetini | DW | 21.09.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wapinzani wa ziara ya Papa wapingwa

Baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Ujerumani wamewapinga vikali wale wanaopanga kususia hotuba ya Papa Benedict XVI Bungeni, wakati kiongozi huyo akifanya ziara nchini Ujerumani katika siku chache zijazo.

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict XVI

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Benedict XVI

Gazeti la Westdeutsche Allgemeine limemnukuu Waziri wa Elimu wa Ujerumani kutokea chama cha CDU, Annette Schavan, akiwashambulia vikali wale wanaopanga kuisusia ziara ya Papa hapa Ujerumani.

"Ama jambo hili mimi siwezi kulielewa kabisa, maana sio tu Papa ni mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, lakini pia ni mwanafalsafa mkubwa wa zama hizi." Amesema Waziri Schavan.

Lakini kama Waziri Schavan wa CDU hawaelewi wanaotaka kuisusia hotuba ya Papa huko Bungeni, gazeti hilo limemnukuu mwanasiasa mwengine wa chama cha Die Linke, Gesine Lötzsch, akisema yeye anawaelewa vyema.

"Mimi ninawaelewa wale ambao hawataki kuisikiliza hotuba ya Papa. Wao wanapinga maadili ya ngono kwenye Kanisa Katoliki, taswira ya mwanamke na ukweli kuwa kanisa hilo limepiga marufuku matumizi ya kondomu." Amesema Lötzsch.

Ziara ya Rais w Uturuki nchini Ujerumani

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Abdullah Gul wa Uturuki.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel (kulia) akiwa na mgeni wake, Rais Abdullah Gul wa Uturuki.

Wakati kuna tafauti ya mawazo katika ziara ya Papa Benedict XIV itakayofanyika siku zijazo, hakuna tafauti kubwa sana katika ziara ya Rais wa Uturuki, Abdullah Gul, ambayo inamalizika hivi leo (21.09.2011) hapa Ujerumani.

"Rais Christian Wulff amempatia mwenzake Abdullah Gul mapokezi makubwa ya kifamilia na ya kiheshima, si kwenye makao makuu ya serikali huko Berlin tu, bali hata katika mji wa kwao wa Osnabrück". Ndivyo anavyosema mhariri wa la Osnabrücker Zeitung.

Na kauli aliyoitoa Rais Wulff wakati akimpa mkono wa ta'azia mwenzake kuhusiana na mashambulizi ya Ankara ni ushahidi kuwa Ujerumani na Uturuki zina mafungamano makubwa na ya ndani.

Kwa ziara hii na kwa kauli hizi, Rais Wulff ameendelea tu kuthibitisha msimamo wake wa kwamba: "Ujerumani ni nyumbani pia pa Uislamu" kama palivyo nyumbani pa dini nyengine.

Ile mijadala inayoendelea ya ujumuishaji wa wageni kwenye jamii ya Ujerumani, uvaaji wa hijabu na uwezekano wa Uturuki kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya, ni mambo yanayozua hisia kali, misimamo na hata matatizo. Lakini Rais Wulff anaichukulia kwa tahadhari na kwa uhodari, maana hakuna lisilowezekana.

Kuporomoka kwa uchumi wa Italia

Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi.

Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi.

Suala jengine lililoangaziwa ni mgogoro wa madeni barani Ulaya, katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Mhariri wa Oldenburgische Volkszeitung anasema ni jambo la kuhuzunisha lakini ndio ukweli wenyewe kuwa Italia nayo inakuwa kitoto chengine cha Ulaya, na hasa katika eneo linalotumia sarafu ya Euro, ambacho kinahitaji matunzo na kushughulikiwa.

Takwimu za uchumi zinaonesha kuwa taifa hilo linakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni, na kubwa zaidi ni kwamba, Wataliana watajikuta katika wakati mgumu, maana serikali ya Waziri Mkuu Silvio Berlusconi imechelewa sana kung'amua ukweli huu.

Vyanzo: Westdeutsche Allgemeine/Osnabrücker Zeitung/Oldenburgische Volkszeitung
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 21.09.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/12dTV
 • Tarehe 21.09.2011
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/12dTV
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com