Wanasiasa wa Urusi wakutana na al-Assad | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wanasiasa wa Urusi wakutana na al-Assad

Wanasiasa wa Urusi wamekutana na Rais wa Syria Bashar al-Assad, siku moja baada ya mashambulizi ya pamoja ya angani ya Marekani, Uingereza na Ufaransa nchini Syria

Vyombo vya habari vya Urusi vimesema Al-Assad ameusifu mfumo wa enzi ya Kisovieti wa kujikinga dhidi ya makombora ambao Syria inaripotiwa kutumia kuyaripua karibu makombora 70 kati ya 100 yaliyofyatuliwa wakati wa mashambulizi hayo.

Pia ameyaelezea mashambulizi hayo kuwa kitendo cha uchokozi wa nchi za Magharibi, maoni ambayo yameungwa mkono na wabunge hao wa Urusi waliomtembelea.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi TASS, Sergei Zheleznyak amesema baada ya mkutano na al-Assad kuwa kutokana na mtazamo wa rais, huu ni uchokozi na tunamuunga mkono.

UN-Sicherheitsrat in New York | Abstimmung Syrien (Reuters/E. Munoz)

Baraza la Usalama lilipinga azimio la Urusi

Warusi hao waliomtembelea wamemuelezea al-Assad kuwa katika "hisia nzuri”. Rais huyo wa Syria pia ameripotiwa kukubali mwaliko wa kuitembelea Siberia, ijapokuwa haijafahamika ni lini ziara hiyo itafanyika. Juammosi, rasimu ya azimio lililowasilishwa na Urusi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiyalaani mashambulizi hayo ya angani halikupitishwa.

Kazi ya OPCW yaanza mjini Douma

Ziara ya wanasiasa hao imefanywa katika siku moja ambayo shirika la habari la Ufaransa – AFP limeripoti kuwa wakaguzi kutoka Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Matumizi ya Silaha za Sumu – OPCW wanatarajiwa kuanza uchunguzi wao wa kubaini kama silaha za gesi ya klorini au sarin zilitumiwa dhidi ya raia katika shamubulizi hilo la Aprili 7 mjini Douma.

Wapelelezi hao waliwasili Juammosi, muda mfupi tu baada ya mashmbulizi hayo ya washirika kufanywa. Urusi na Iran ambayo ni mshirika wake anayemuunga mkono Syria ziliyalaani mashambulizi hayo ya angani yaliyoongozwa na Marekani kwa kufanywa kabla ya shirika la OPCW kufanya uchunguzi.

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiarabu kuijadili Syria

Kairo Arabische Liga Außenministertreffen Jerusalemfrage (picture-alliance/Photoshot/A. Gomaa)

Jumuiya ya Kiarabu ilikutana mwisho Machi 2017

Wakati Assad aliwaalika wabunge wa Urusi, viongozi wengine wa mataifa ya Kiarau walikutana nchini Saudi Arabia leo Jumapili kwa mkutano wao wa kilele wa kila mwaka wa Jumuiya ya Kiarabu, ambao ulikuwa umeahirishwa mwezi uliopita kutokana na uchaguzi wa Misri.

Karibu wakuu 17 wa mataifa ya Kiarabu walitarajiwa kuhudhuria mkutano huu mjini Dhaharan. Al-Assad hajashiriki katika mkutano huo wa kilele tangu 2011, wakati shirika hilo lenye nchi 22 wanachama lilipoufuta uwanachama wake.

Ujumbe wa Qatar unaongozwa na mwakilishi wake wa kudumu katika Jumuiya ya Kiarabu, badala ya afisa mwandamizi katika ufalme wa nchi hiyo – ishara kuwa mvutano wa kikanda kati ya Qatar na baadhi ya mairani zake bado ni mkubwa.

Miongoni mwa mada kuu zinazotarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo wa kilele ni pamoja na kitu kinachoonekana kuwa ni Iran kuingilia masuala ya nchi za Kiarabu, kama vile vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen na katika kuunga mkono mapigano ya Washia nchini Iraq.

Mashambulizi ya angani nchini Syria mwishoni mwa wiki na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka saba sasa nchini humo pia ni mambo yanayotarajiwa kujadiliwa.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters, AP
Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com