1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wadephul kuhutubia UN huku vita vya Iran vikiendelea

27 Aprili 2026

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul, anatrajiwa kuwasili New York Marekani kushiriki mkutano wa Barazala la Usalama la Umoja wa Mataifa, utakaojadili hali katika Mlango Bahari wa Hormuz.

https://p.dw.com/p/5CsRO
Deutschland Schönefeld 2026 | Wadephul
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann WadephulPicha: Sebastian Gollnow/dpa/picture alliance

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Ujerumani anatarajiwa kutoa hotuba wakati wa mjadala kuhusu usalama wa baharini, akizungumzia juhudi za kurejesha biashara ya mafuta na gesi katika ujia huo wa bahari uliogeuka kuwa mzizi wa fitna katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Wadephul, atakaekuwa Marekani kwa ziara ya siku mbili, pia atahudhuria mkutano wa mapitio ya makubaliano ya mkataba wa kuzuwia kusambaa kwa silaha za nyuklia (NPT).

Mkutano huu unakuja wakati mgumu, ambako Israel na Marekani, tayari zimeanzisha vita vyao dhidi ya Jamhuri hiyo ya kiislamu, zikisema zinataka kuizuwia nchi hiyo kumiliki silaha za nyuklia.

Mpango wa nyuklia wa Iran umekuwa kwa muda mrefu ukizua mvutano kati ya Washington na Iran. Pande hizo mbili zimekuwa zikijadiliana suala hilo tangu kuanza kwa vita vya Iran Februari 28. Katika Vita hivyo Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliuawa katika siku ya kwanza ya vita hivyo pamoja na viongozi wengine muhimu serikalini.

USA New York 2026 | Johann Wadephul  na António Guterres
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Johann Wadephul akiwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres Picha: Dominik Butzmann/photothek.de/AA/picture alliance

Iran muda wote imekuwa ikikanusha kwamba ina lengo la kutengeneza silaha za nyuklia, ikisema mpango wake ni wa amani.

Wadephul kukutana na António Guterres,

Wakati mvutano ukiendelea kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Wadephul anatarajiwa kukutana pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, na maafisa wengine wakuu wa Umoja huo, akitafuta uungwaji mkono wa Gutterres katika azma ya taifa hilo la Ulaya kutaka kuwa mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa.

Baraza hilo lililo na jukumu la kusimamia amani na usalama wa kimataifa,  ndio chombo cha kipekee cha Umoja huo chenye mamlaka ya kupitisha sheria ambazo wanaozikiuka huenda wakakabiliwa na vikwazo au hata hatua za kijeshi.

Baraza hilo linawanachama watano wa kudumu ikiwemo Uingereza,  China, Ufaransa, Urusi na Marekani na wanachama wengine 10 ambao sio wa kudumu waliochaguliwa na hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kwa miaka miwili, kabla ya kuondoka na kuchaguliwa wengine ili kila nchi ipate nafasi ya uwakilishi ndani ya Baraza hilo.