1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi washambuliwa katika mji wa Misrata

Sekione Kitojo14 Juni 2011

Majeshi yanayomuunga mkono kiongozi wa Libya kanali Muammar Gaddafi yameshambulia kwa makombora kituo cha kusafishia mafuta katika mji wa pwani wa Misrata na kusitisha uzalishaji wa mafuta.

https://p.dw.com/p/11Zt3
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Guido Westerwelle pamoja na waziri wa ushirikiano wa maendeleo Dirk Niebel wakiwa Benghazi nchini Libya jana jumatatu.Picha: picture-alliance/dpa

Majeshi yanayomuunga mkono kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, yameshambulia kwa makombora kituo cha kusafishia mafuta kinachohudumia mji unaoshikiliwa na waasi cha Misrata jana, baada ya waasi kusonga mbele katika mashambulio yao upande wa magharibi kuelekea mji wa pwani wa Zlitan. Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, ameyataka mataifa ya Kiafrika kumtaka Muammar Gaddafi ajiuzulu wakati wa ziara yake ya mataifa hayo ya Afrika.

Mapigano katika mji wa Zlitan yanawasogeza waasi karibu na mji wa Tripoli, ambayo ndio ngome kuu ya kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, mji ulioko kilometa 200 magharibi ya mji wa Misrata. Mwandishi habari wa Shiriuka la Reuters karibu na mji wa bandari wa Misrata, amesema makombora sita yameharibu majenereta ya umeme katika kinu hicho cha kusafishia mafuta. Uharibifu huo umesababisha kusitishwa kwa uzalishaji, ambao, hata hivyo, ulikuwa katika kiwango cha chini na kuhudumia mji wa Misrata .

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton, ameyataka mataifa ya Afrika kumshurutisha kiongozi wa Libya Moammar Gaddafi kujiuzulu na kuchukua hatua kali dhidi ya utawala wake.

"Hakuna shaka kwamba hatua ambazo kwa bahati mbaya zikiwaathiri watu wa Libya kwa zaidi ya miaka 40 zinakwenda kinyume na wimbi la historia. Na nafahamu kuwa ni kweli kwamba katika muda wa miaka kadha Gaddafi amekuwa na jukumu la juu kabisa katika kuyapatia msaada wa fedha mataifa kadha ya Kiafrika pamoja na taasisi kama Umoja wa Afrika. Lakini imeonekana wazi kila siku kuwa amepoteza uhalali wake wa kuongoza na tunapoteza wakati tunapozungumzia iwapo abaki ama aendelee kuongoza, kwasababu kwa kadri Gaddafi atakapobaki madarakani watu wa Libya watakuwa hatarini."

Serikali ya Gaddafi imeahidi jana kuwa itatekeleza mapendekezo yaliyotolewa na mataifa ya Afrika kumaliza mkwamo huo ikiwa ni pamoja na kuandika mswada mpya wa katiba na sheria mpya kuhusu vyombo vya habari, kwa mujibu wa shirika la habari la nchi hiyo, JANA.

Mataifa ya magharibi yanasema kuwa yanaamini ni suala la muda tu kabla ya utawala wa miaka 41 wa kanali Gaddafi kumalizika chini ya mbinyo wa mashambulizi ya jeshi la NATO, vikwazo na baadhi ya viongozi kujitenga na utawala huo. Majeshi yake yakionyesha nia ya kutotaka kusalim amri , yamewapa kipigo waasi katika maeneo kadha na kulazimisha majeshi ya NATO kurefusha operesheni yao hadi mwishoni mwa Septemba.

Wakati huo huo Ujerumani imelitambua baraza la waasi la uongozi wa muda nchini Libya. Ameyasema hayo waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle wakati wa ziara yake katika eneo linaloshikiliwa na waasi la Benghazi jana.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre

Mhariri : Othman Miraji.