Vyama shirika vyaidhinisha mkataba wa muungano | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.10.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vyama shirika vyaidhinisha mkataba wa muungano

Wanauchumi wasifu mkataba wa muungano unaokosolewa na upande wa upinzani

default

Wakuu wa vyama shirika vya serikali mpya ya muungano:Kutoka kulia Horst Seehofer wa CSU,Angela Merkel wa CDu na Guido Westerwelle wa FDP

Wiki kama nne hivi baada ya uchaguzi mkuu,viongozi wa vyama vya CDU,CSU na FDP wanatarajiwa kutia saini mkataba wa muungano baadae leo usiku.Kabla ya hapo vyama vya CDU na CSU viliitisha kila kimoja mkutano mkuu wa dharura kuidhinisha mkataba huo.Waliberali wa FDP wameshauidhinisha tangu jana.Wanauchumi wameridhika na mkataba huo wa serikali mpya ya muungano.Lakini upande wa upinzani unaukosoa.

Bunge jipya la shirikisho litakutana kesho kwa kikao chake cha kwanza kabla ya kupiga kura jumatano ijayo kumchagua tena kansela Angela Merkel aiongoze Ujerumani kwa kipindi chengine cha miaka minne.Hiyo hiyo kesho rais wa shirikisho Horst Köhler atawakabidhi mawaziri wa serikali ya zamani hati za kukamilisha mhula wao.

Serikali mpya ya muungano imepania kuachia nakisi ya bajeti iongezeke kwa lengo la kuchochea ukuaji wa kiuchumi.Mara uchumi utakapoanza kukua,yote mengine yatafuata.Kwa mujibu wa mkakati wa washirika wepya, utaratibu unaolengwa kufuatwa utasaidia kubuni nafasi zaidi za kazi,watu zaidi na wajasiria mali watapata pesa na kulipa kodi, na hali hiyo itakasaidia kufunika pengo la bajeti,hatua baada ya hatua.

Waziri mteule wa fedha Wolfgang Schäuble amekiri hapo jana,matumaini ya kusawazisha bajeti kwa kipindi cha miaka minne ijayo ni "ndoto".Ujerumani italazimika kuchukua madeni zaidi kuweza kukimu gharama zake.Kwa mwaka huu Ujerumani inatazamiwa kukopa kiasi cha yuro bilioni 90.

Wana uchumi wanaonyesha kuridhishwa na mkakati wa serikali mpya.Mwenyekiti wa shirikisho la waajiri wa Ujerumani Dieter Hundt anasema:

"Mkataba wa Muungano unatoa ishara njema.Unafungua njia ya ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani na kwa namna hiyo kubuniwa nafasi za kazi."

Hata hivyo upande wa upinzani unaukosoa mkataba wa muungano kati ya CDU/CSU na FDP na kusema haueleweki na hauzingatii masilahi ya jamii .Mwenyekiti mteule wa chama cha SPD SIGMAR Gabriel anasema:

""Majimbo hayatakua na fedha kugharimia shule,serikali za miji hazitakua na fedha kugharimia shule za chekechea.Inamaanisha miradi yote muhimu itaachwa kando,badala yake watakaofaidika ni wale kulipwa mishahara mikubwa mikubwa ."

Mwenyekiti wa chama cha walinzi wa mazingira Cem Özdemir anasema mkataba huo hauna mpangilio kifedha.Na kiongozi mmojawapo wa chama cha mrengo wa shoto-Die Linke Dietmar Bartsch anahoji siasa ya serikali mpya ya muungano haijulikani inaelekea wapi.

Licha ya lawama hizo za upande wa upinzani,wataalam wa kiuchumi wanahisi serikali mpya ya muungano haina njia nyengine.Andreas Rees wa benki ya UNICREDIT anasema serikali mpya ya muungano imegundua kwamba kupunguza nakisi ya bajeti kuanzia mwakani katika wakati ambapo idadi ya wasiokua na kazi inatishia kuongezeka,halitakua jambo maana.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou /dpa

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 26.10.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KFfk
 • Tarehe 26.10.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KFfk
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com