Vladimir Putin wa Urusi azuru Ufaransa | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vladimir Putin wa Urusi azuru Ufaransa

Hii ni ziara yake ya kwanza nje kama Waziri Mkuu

default

Vladimir Putin, Waziri Mkuu wa Urusi.Amefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi nchini Ufaransa tangu achukue wadhifa mpya alionao kwa sasa.Akiwa mjini Paris amelaani wakosoaji wa Moscow kuhusu haki za binadamu akisema wanatia chumvi

Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin yuko nchini Ufaransa akiwa katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi ateuliwe katika nafasi hiyo wiki kadhaa zilizopita.

Bw Putin amepangiwa kukutana na vigogo mbalimbali wa sekta kadhaa nchini humo.

Rais wa zamani wa Urusi ambae sasa ni waziri mkuu wa nchi hiyo,Vladimir Putin,amepuuza ukosoaji wa hali ya haki za binadamu nchini mwake akisema kuwa hizo ni njama za kuitaka kuiwekea nchi yake shinikizo la kidiplomasia.

Akizungumza na waandishi habari baada ya kukutana, kwa mazungumzo, na cheo somo wake wa Ufaransa Francois Fillion, Putin,amesema kuwa hofu ya hali ya haki za binadamu nchini mwake inatiwa chumvi. Amewashutumu wakosoaji wa utawala wa Moscow kwa kutumia suala hilo kama chombo cha shinikizo.

Mwenyeji wake kwa upande wake amesema kuwa Ufaransa haitaki kuihubiria nchi nyingine kuhusu suala hilo.

Ufaransa ndio kituo cha kwanza cha safari ya Putin nje ya nchi kama waziri mkuu wa Urusi,na wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa hilo lilikusudiwa. Ufaransa ,baadae mwaka huu, itachukua urais wa Umoja wa Ulaya jambo ambalo Putin ameligusia akisema kuwa litasaidia kusogeza mbele alichokiita mazungumzo ya ushirika wa kimkakati.

Mataifa ya Umoja wa Ulaya, jumatatu ya wiki hii, yalipasisha mpango wa kuanzisha mazunguzo na Moscow kuhusu mikataba kadhaa ya ushirikiano, na hivyo kukomesha miaka miwili ya malumbano kuhusu suala hilo.

Putin amewaalika raia wa Ulaya kupeleka vitega uchumi nchini mwake.Pia amewaomba kulimbikiza katika sekta ya nishati,akitoa mfano wa mkataba wa kampuni mashuri ya mafuta nchini Ufaransa ya TOTAL kushughulikia mradi mkubwa wa mafuta katika bahari ya Barents.

Waziri mkuu wa Ufaransa Fillion amesema kuwa nchi yake inakaribisha, kwa mikono miwili, miradi ya Urusi,ingawa amesisitiza kuwa kuna haja ya kushughulikia urasimu wa sheria ili kufanikisha ushirikiano huo. Ameongeza kuwa usalama wa nishati barani Ulaya unategemea mno uhusiano mzuri na Urusi.

Wachambuzi wanasema kuwa waziri mkuu wa Ufaransa hapo ni kama alikuwa anagusia wasiwasi wa mataifa ya Ulaya kuwa huenda Urusi ikatumia utajiri wake wa mafuta pamoja na gesi kwa manufaa yake ya kisiasa.

Kwa mda huohuo ziara hii ya Bw Putin imetoa sura mpya kuhusu ushawisi wa kisiasa nchini Urusi.

Katika ishara inayoonyesha kama Putin baado ana ushawishi mkubwa hasa katika sekta ya sera za nje za Urusi tangu ajiuzulu urais,amekutana na rais Nicolas Sarkorzy.Pia alipangiwa kukutana leo na rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac.

Maafisa wa Urusi wamesema mjini Paris kuwa Bw Putin pia atajadilia mipango ya Marekani ya kuweka makombora yake katika bara ulaya kama sehemu yake ya kinga. Mpango huo wa Marekani unapingwa vikali na Urusi.

 • Tarehe 30.05.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E9sS
 • Tarehe 30.05.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E9sS
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com