Viongozi wa umoja wa Ulaya wakutana leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa umoja wa Ulaya wakutana leo

Viongozi wa kitaifa na serikali wa umoja wa Ulaya wanaanza kikao chao muhimu leo mjini Brussels.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy.

Viongozi wa kitaifa wanakabiliana na maswali tete leo Alhamis iwapo wachukue uamuzi wa kuandika upya mkataba wa Lisbon, unaoweka pamoja mataifa ya Umoja wa Ulaya katika juhudi za kuzuwia mzozo mpya wa madeni.

Ujerumani inatarajiwa katika mkutano huo wa siku mbili mjini Brussels , kutoa hoja kuwa mkataba wa Lisbon unahitaji kufanyiwa marekebisho iwapo umoja wa Ulaya utalazimika kubana uendeshaji wa masuala ya kifedha katika mipaka yake ya ndani, baada ya kutokea mzozo wa madeni mwaka huu nchini Ugiriki.

Ujerumani inaungwa mkono na Ufaransa, ambayo imefanikiwa kupata maridhio muhimu kutoka kwa serikali ya kansela Angela Merkel mjini Berlin na kukubali kulegeza adhabu dhidi ya zile nchi zitakazoshindwa kutimiza malengo yaliyowekwa ya viwango vya madeni katika bajeti zao. Ufaransa inataka adhabu zisitolewe papo kwa hapo na kwamba zitolewe baada ya kupigiwa kura.

Lakini makubaliano baina ya Merkel na rais Nicolas Sarkozy wiki iliyopita yamezusha wimbi la upinzani. Hususan kuna hofu ya kurejewa kwa matatizo yaliyojitokeza na hatimaye kuhitajika kufanya kazi ya ziada kuweza kuupitisha mkataba huo wa Lisbon, ambao ulichukua miaka nane kuweza kuuidhinisha baada ya kampeni zilizoshindwa za kura ya maoni nchini Ufaransa, Uholanzi na Ireland.

Wiki hii watendaji wakuu waandamizi wa umoja wa Ulaya , kamishna wa masuala ya uchumi Olli Rehn na kamishna anayehusika na sera za mambo ya kigeni Viviane Reding, kila mmoja alipinga vikali madai ya Ujerumani.

Griechenland Finanzkrise

Kamishna wa masuala ya kiuchumi wa umoja wa Ulaya Olli Rehn.

Kuingilia kwao kati kulifuatia mlolongo wa matamshi ya upinzani kutoka mataifa mengine na hofu kuwa mipango ya kuuandika upya mkataba huo inaweza kusababisha baadhi ya mataifa miongoni mwa wanachama 27 kujitokeza katika mkutano wa leo na orodha mpya ya madai ambayo hayahusiki.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron , kwa mfano , tayari amekwisha eleza kuwa anataka kundi hilo la mataifa kuunga mkono wito wake wa kuzuiwa kabisa kwa bajeti ya umoja wa Ulaya kwa mwaka 2011.

Mabishano hayo yanaleta utata, wakati utayari wa Ufaransa kuangalia uwezekano wa mabadiliko katika mkataba huo ukijionesha.

Ufaransa pamoja na mambo mengine inataka mfuko wa fedha za mikopo ya dharura ya miaka mitatu ya muda kwa ajili ya mataifa ambayo yanashindwa kujimudu kifedha, kubadilishwa na kuwa mfuko wa kudumu unaoshughulikia mizozo ya kifedha.

Kuufanya mfuko huo kuwa wa kudumu kunahitaji mkataba huo kubadilishwa kutokana na vipengee vya katiba ya Ujerumani. Iwapo Ujerumani haitafanikiwa kupata kile inachotaka , inaweza kuleta hatari ya kuuweka katika hali ya wasi wasi muundo na sura ya mfuko kama huo wa usalama wa kifedha, unaozuwia kusambaa kwa hali ya madeni katika nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Hatari kwa Ufaransa na udhaifu wa mataifa yanayotumia sarafu ya euro kama Ireland, Ureno , ama hata Ubelgiji, ni kwamba Ujerumani haitaweza kutoa fedha nyingi tena hapo siku za baadaye hadi pale itakapopata uhakika wa kisheria inaoutaka kuweza kupambana na upinzani wa kisiasa nchini mwake.

Maoni ya wapiga kura nchini Ujerumani yameeleza upinzani mkubwa dhidi ya kugharamia makosa ya kibajeti ya mataifa washirika wa euro.

Merkel kimsingi anataka kuwatwika mzigo mdogo zaidi walipa kodi wa taifa hilo na anataka kuhusika zaidi na zaidi kwa mabenki ya binafsi.

Duru katika serikali ya Ujerumani zinasema kuwa kansela anazungumza na kila kiongozi kwa hivi sasa.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE

Mhariri : Josephat Charo.

 • Tarehe 27.10.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PqOp
 • Tarehe 27.10.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PqOp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com