Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Urussi wakutana | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Urussi wakutana

Usalama wa nishati ni suala kuu litakalojadiliwa,wakati Umoja wa Ulaya umeshaanza kuhofia juu ya kukatizwa huduma za utoaji gesi na Urusi kutokana na mvutano wake na Ukraine ulioanza kunukia

default

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Urussi katika mkutano wao uliopita nchini Ufaransa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Urussi wanatarajia kuweka msingi wa mwanzo mpya katika ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa katika mkutano wao wa kilele unaofanyika leo huko Stockholm nchini Sweden.

Rais wa Urussi Dmitry Medvedev ,rais wa tume ya umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso na waziri mkuu wa Sweden, inayoshikilia wadhifa wa kupokezana wa mwenyekiti wa Umoja huo, Fredrik Reinfeldt watahudhuria mkutano huo.

Licha ya pande hizo mbili kutofautiana juu ya masuala ya Nishati,biashara,haki za binadamu na mabadiliko ya hali ya hewa,wanatarajia kuanzisha uhusiano mpya.

Hakuna matarajio makubwa yanayotegemewa kutoka kwenye mkutano huo kwa sasa na hasa kutokana na hofu ya Umoja wa Ulaya kwamba usambazaji wa gesi kutoka Urussi upo hatarini kutokana na mzozo kati ya serikali ya Moscow na Kiev.

Hata hivyo pande hizo mbili zinatarajia alau kuepusha malumbano mapya kutokea na kuanza taratibu kuimarisha uhusiano. Waziri wa mambo ya nje wa Finnland Alexander Stubb kabla ya mkutano wa leo alisema kwamba inabidi paweko ushirikiano mzuri kati ya Urussi na Umoja wa Ulaya kwasababu ni dhahiri Umoja wa Ulaya unaihitaji Urussi kutokana na nishati yake na nchi hiyo bila shaka inazihitaji nchi za Umoja wa Ulaya kama wateja wake.

Balozi wa Urussi katika Umoja wa Ulaya mjini Brussels Vladimir Chizhov akizungumzia kuhusu kitakachopewa kipaumbele katika mkutano huo amesema-

"Kwa upande wa Urusi tunaona kuna matatizo katika kambi moja ya kimataifa.Sambamba na suala la mgogoro wa fedha na kiuchumi duniani mkutano huu wa kilele utayajadili pia masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na hivyo kuufanya kuwa tofauti na mkutano uliopita.Miongoni mwa masuala ya kimataifa yatakayozungumziwa ningependa pia kusisitiza juu ya suala hili la nishati''

Symbolisches Bild über die Unterzeichnung des Rußland Ukraine Abkommens in Moskau

Urussi na Ukraine zimekuwa zikivutana mara kwa mara juu ya suala la ulipiaji wa gesi.

Jumatatu iliyopita Urussi na Umoja wa Ulaya zilisaini makubaliano juu ya mfumo mpya wa kutoa onyo la mapema utakaosaidia kuepusha kukatizwa ghafla kwa usambazaji wa gesi katika nchi za Ulaya. Robo ya kiwango cha gesi kinachotumika kote barani ulaya kinatokea nchini Urussi,gesi hiyo zaidi ikipitia Ukraine ambayo mara kwa mara inazozana na Moscow kuhusiana na suala la malipo.

Urussi hivi karibuni imeonya kwamba Ukraine ambayo imekubwa vibaya na mzozo wa kiuchumi huenda ikashindwa kulipa deni lake la gesi katika kipindi cha msimu huu wa Baridi.

Kutokana na hali hiyo kesho alhamisi waziri mkuu wa Urussi Vladmir Putin atakutana na mwenzake wa Ukraine Yulia Tymoshenko katika mazungumzo juu ya suala hilo la nishati.

Kuhusu usalama wa nishati balozi wa Urussi katika Umoja wa Ulaya anasema pande zote mbili Urussi na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuimarisha juhudi zao kuelekea Ukraine ikiwa wanataka kuepusha mvutano juu ya suala la gesi.Vladimir Chizhov Ameongeza kusema-

"Inasikitisha kwamba Ukraine inalitumia suala hili kwa kampeini za uchaguzi.Ndiyo maaana tunauomba Umoja wa Ulaya uandae mpango wa usalama. Pia katika kugharimia kifedha huduma ya usafirishaji gesi kupitia Ukraine."

Urussi ingependelea sana kuona kwamba Umoja wa Ulaya unaisaidia Kiev kifedha kulipa madeni yake ya gesi ili kuepusha matatizo zaidi na suala hilo pia litajadiliwa katika mkutano wa leo.Hata hivyo Umoja wa Ulaya hata kabla ya mkutano huo umeshaondoa uwezekano wa kuisadia Ukraine kulipa madeni yake ya gesi kwa Urussi.

 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KZhE
 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Saumu Mwasimba
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KZhE
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com