Vikosi vya Syria vyauzingira mji wa Hama | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vikosi vya Syria vyauzingira mji wa Hama

Vifaru vya jeshi la Syria vimeendelea kuuzingira mji wa Hama ambako kiasi ya watu 100 inaarifiwa waliuawa hapo jana , huku Rais Bashar al-Assad akivipongeza vikosi hivyo kwa kupambana na wapinzani wa serikali

default

Vifaru vikivinjari katika mji wa Hama

Vifaru hivyo vya jeshi la Syria viliingia kwenye mji wa Hama hapo siku ya Jumapili ambapo pamoja na wadunguaji walishambulia makaazi ya raia

Kiasi ya watu 100 waliuawa huko Hama, ambapo taarifa pia kutoka sehemu mbalimbali zinasema vikosi vya usalama viliendesha operesheni dhidi ya waandamanaji na kwa mujibu wa mashuhuda watu kiasi ya 40 waliuawa.

Kutoka miji ya Hama,Deir al Zur au Deraa zimetolewa taarifa za kutokea kwa mauaji hayo.Mmoja wa mashuhuda kutoka mji wa Bukamal uliyoko mpakani na Iraqi aliarifu

´´Ilianza Jumapili asubuhi, walivamia mashule na misikiti, Jana saa 12 asubuhi wakaingia mjini vifaru vimeharibu au kuchoma moto .Wamechoma moto kila kitu na walishambulia kwa risasi nyumba za watu.

Mkuu wa taasisi inayotathmini masuala ya haki za binaadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman ameiita siku ya Jumapili kuwa ni siku ambayo yamefanyika mauaji makubwa kabisa tokea kuanza kwa vuguvugu la upinzani dhidi ya serikali mwezi Match mwaka huu, na kuongeza kuwa watu saba waliuawa hapo jana.

Jumuiya ya kimataifa imelaani mashambulizi hayo ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana hii leo katika kikao cha ndani kuijadili hali hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague ametaka kuongezwa kwa mbinyo wa kimataifa dhidi ya utawala wa Syria, ukiwemo kutoka mataifa ya kiarabu pamoja Uturuki.

Hata hivyo amesema kuwa hakuna uwezekano wa kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa kuingilia kati kijeshi kama lile la Libya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa umoja wa kujihami NATO Anders Fogh Rasmussen amesema kutokuwepo kwa azimio la Umoja wa Mataifa pamoja na uungwaji mkono wa mataifa ya kiarabu ina maana kuwa hali ya Syria ni tofauti na ile ya Libya.

Umoja wa Ulaya umesema unaimarisha vikwazo dhidi ya utawala wa Syria. Michael Mann ni msmemaji wa Umoja huo.

´´Tayari tumekwishaweka vikwazo dhidi ya viongozi wa utawala wa Syria, pia watu wanajihusisha na ukandamizaji dhidi ya raia na tunategemea kupitia uamuzi mwengine, ambapo watu wengine watano wanaongezwa katika orodha ya wale waliyowekewa vikwazo.Hii ina maana ni pamoja na kuzuia mali zao na vikwazo vya kusafiri´´

Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Ureno zinamatumaini ya kufufuliwa kwa pendekezo kwenye kikao cha leo cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kutolewa tamko kulaani hali hiyo huko Syria.

Hata hivyo wanadiplomasia wanasema kuwa uwezekano ni kuwa baraza la usalama litaelezea kusikitishwa kwake na hali nchini Syria lakini uwezekano ni mdogo wa kutaka baraza hilo lichukue hatua.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/ZPR

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com