1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifaa vya kisasa vya kijeshi vya Urusi vyawasili Niger

12 Aprili 2024

Niger imesema kuwa wakufunzi wa kijeshi na wafanyakazi wa wizara ya ulinzi ya Urusi wamewasili nchini humo katika kile kinachotajwa kuwa ni kujenga uhusiano wa karibu na Moscow kama mataifa jirani ya ukanda wa Sahel

https://p.dw.com/p/4egqs
Urusi
Urusi inatarajiwa kuiwekea ulinzi wa anga NigerPicha: Defence Ministry Russian Federation/Tass/IMAGO

   
Televisheni ya taifa ya Niger imesema kuwa wakufunzi wa kijeshi na wafanyakazi wa wizara ya ulinzi ya Urusi wamewasili nchini Niger katika kile kinachotajwa kuwa ni kujenga uhusiano wa karibu na Moscow kama yalivyo mataifa mengine jirani yanayoongozwa kwa utawala kijeshi.

Soma zaidi. Serikali ya kijeshi ya Niger yavunja mabaraza ya miji

Mapema mwezi Januari serikali ya kijeshi ya Niger ilikubali kuongeza ushirikiano wa kijeshi na Urusi, baada ya kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wakisaidia kupambana na makundi ya itikadi kali katika mataifa kadhaa ya kanda ya Sahel.

Kituo cha utangazaji cha Tele Sahel kimeonyesha ndege ya usafiri ya Urusi ikiwasili katika uwanja wa ndege wa mjini Niamey huku chombo hicho cha habari kikiarifu kuwa ndege hiyo iliyobeba vifaa vya kisasa vya kijeshi na wakufunzi wa kijeshi kutoka wizara ya ulinzi ya Urusi imewasili.

Niger
Wanajeshi wa NigerPicha: Gazali/DW

Akizungumza baada ya kuwasili Niger, mmoja wa wakufunzi wa Urusi ambaye jina lake halikufahamika amesema wako nchini humo kuimarisha uhusiano wa kijeshi.

Soma zaidi. Niger yaitaka Algeria kuelezea mateso kwa wahamiaji

"Tuko hapa kutoa mafunzo kwa jeshi la Niger kwa kutumia zana za kijeshi ambazo zimefika hapa. Ni vifaa tofauti vya taaluma za kijeshi, kwa ajili ya kuimarisha taaluma za kijeshi. Tuko hapa kuendeleza ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Niger."amasema mmoja wa wakufunzi wa Urusi ambaye jina lake halikufahamika.

Urusi itaweka mifumo ya ulinzi wa anga Niger

Ripoti zinaeleza kuwa Urusi itasaidia kuweka mfumo wa ulinzi wa anga nchini Niger na kuhakikisha udhibiti kamili wa anga nchini humo.

Machi 26, Mkuu wa serikali ya kijeshi ya Niger, Jenerali Abdourahamane Tiani, alizungumza kwa simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin juu ya ushirikiano wa kiusalama wa pamoja na ushirikiano wa kimkakati wa kimataifa dhidi ya vitisho vinavyoendelea kwa sasa duniani.

Niger | Jenerali Tchiani
Mkuu wa serikali ya kijeshi ya Niger, Abdourahamane Tiani alizungumza kwa simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin juu ya ushirikiano wa kiusalama wa pamoja na ushirikiano wa kimkakati Picha: ORTN/Télé Sahel/AFP/Getty Images

Niger ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, ilikuwa mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi katika kupambana na makundi ya waasi katika ukanda wa Sahel lakini kwa sasa imeigeukia Urusi tangu rais aliyechaguliwa alipoondolewa madarakani mwaka uliopita.

Soma zaidi. Mkuu wa serikali ya Niger azungumzia 'ushirikiano wa usalama' na Putin

Kwa sasa Niger imeungana na mataifa jirani ya Mali na Burkina Faso ambayo pia yanatawaliwa na viongozi wa kijeshi baada ya mapinduzi kuunda kikosi cha pamoja cha kupambana na uasi wa muda mrefu katika ukanda huo.

Kuwasili kwa wakufunzi wa Kirusi kunafuatia uamuzi wa Niger katikati ya mwezi Machi wa kubatilisha makubaliano yake ya kijeshi na Marekani ambayo yaliiruhusu Marekani kufanya kazi kwenye kambi zake mbili za kijeshi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kambi kubwa ya droni iliyogharimu zaidi ya dola milioni 100. 

Marekani ina takriban wanajeshi 1,000 nchini Niger ingawa kwa sasa harakati zao zimekuwa ndogo tangu yalipotokea mapinduzi na Marekani kuzuia msaada kwa serikali ya Niger.